Unaona mambo mengi, lakini huyatii moyoni; 

Siku za Mwisho No Comments

Unaona mambo mengi, lakini huyatii moyoni;

Isaya 42:20 “Unaona mambo mengi, lakini huyatii moyoni; masikio yake ya wazi, lakini hasikii.”

Je! we ni miongoni mwa waonao mambo mengi, lakini huyatii moyoni?

Neno la Mungu linasema..

Isaya 28:22 Basi sasa msiwe watu wenye kudharau, vifungo vyenu msije vikakazwa; maana nimesikia kwa Bwana, BWANA wa majeshi, habari ya hukumu itakayotimizwa, nayo imekusudiwa, itakayoipata dunia yote pia,

23 Tegeni masikio, sikieni sauti yangu, sikilizeni mkasikie neno langu.

Katika nyakati hizi za mwisho watu wengi pamoja na kuwa wanaona kabisa kwamba tunaishi katika siku za mwisho, dalili zote zinaonyesha kuwa muda uliobaki ni mfupi, na wengine mpaka wameonyeshwa maono au ndoto kuhusu mambo yanayoenda kuikumba hii dunia..

Lakini bado hata hawashutuki, kinyume chake wanadhihaki na kudharau injili inayohubiriwa kila siku masikio mwao, hawataki kufungua mioyo yao waitafakari hukumu inayokuja, wanaona mambo mengi lakini hawatilii maanani, na hiyo ndio maana ya kufumba macho kulikozungumziwa kwenye maandiko..

Mathayo 13:14 Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona.

15 Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, NA MACHO YAO WAMEYAFUMBA; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya.

16 Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia.

Je! macho yako yanaona? Au umeyafumba.

Je! unaona dalili za kurudi kwa Yesu? Au unaona mambo mengi lakini huyatii moyoni!

Kama unaona mambo mengi lakini huyatii moyoni, unaona ishara hizi zote na bado hutaki kuelewa, unaona maasi yalivyongezeka, ushoga umeenea duniani kote na imehalalishwa, watu wanabadili njisia zao, watu wanafunga ndoa na wanyama, unaona mambo hayo machafu yalivyotapakaa duniani, manabii wa uongo na makiristo wa uongo ambao wamekuja kwa kasi, unaona na mambo mengi tu yahusuyo siku za mwisho lakini hutaki kuelewa..

Hiyo ndio maana ya kufumba macho, na maandiko yalitabiri kuwa siku za mwisho watakuwepo na kundi la watu wengi watakaokuja na dhihaka zao na kusema huyo mnayemngojea (Yesu) harudi leo wala kesho, amekufa n.k dunia haiwezi kufikia mwisho maana tangu zamani ilikuwa hivi hivi..

kwamaana wanayafumba macho yao wasione kuwa kulikuwepo na dunia ya kwanza ikaharibiwa na gharika ya maji. Je na wewe ni miongoni mwa wanaotimiza unabii huu?

2Petro 3:3 Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe,

.4 na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa.

5 Maana hufumba macho yao wasione neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu;

6 Kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia.

7 Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu.”

Fumbua macho yako, mpokee Bwana Yesu akuokoe na hukumu inayokuja!

Acha kuchezea hatima ya maisha yako, fahamu kuwa hakuna atakayekusaidia siku ile; fedha haitakusaidia, wala ushujaa wako haitakuokoa, maandiko yanasema shujaa atalia kwa uchungu mwingi (Sefania1:14-17).

Unachopaswa kufanya sasa kama hujampokea Yesu kwa kumaanisha, basi huu ni wakati wako, usisubiri wakati mwingine maana hakuna aijuaye saa wala siku ambayo Kristo atarudi, na kumbuka unyakuo ukipita hakuna nafasi tena ya kutubu.

Na vilevile hata unyakuo usipokukuta, basi fahamu pia kuzimu ipo na hujui siku wala saa ambayo utakufa, na ukifa bila kumpokea Kristo na umesikia injili moja kwa moja ni kuzimu.

Kumpokea Yesu sio kwenda tu kanisani na kusema nimempokea, bali ni kujikana nafsi yako na kuchukua msalaba wako na kumfuata yeye kila siku bila kujali gharama zozote, bila kuangalia utaonekanaje! au utatengwa.

Ukiona bado dhambi ina nguvu juu yako, basi bado hujaamua kumfuata Yesu, ukiona bado unapenda ulimwengu we bado ni wa ulimwengu, maanisha kumfuata Yesu kwa kuacha ulimwengu na dhambi zote. Na baada ya hapo tafuta kanisa la kweli ambalo utaenda kubatizwa, kumbuka ubatizo sahihi ni ule wa maji mengi na Kwa JINA LA BWANA YESU sawa sawa na Matendo 2:38.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hii njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *