Tunza Moto wa Madhabahu usizimike.

Biblia kwa kina No Comments

Tunza Moto wa Madhabahu usizimike.

Nakusalimu katika Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo, Karibu tuyatafakari maneno ya uzima ya mwokozi wetu.

Agano la Kale ni kivuli harisi cha Agano jipya, na kama tukitaka kulifahamu vizuri agano jipya ni lazima tulielewe vizuri agano la Kale itakuwa ni rahisi zaidi kupata ufahamu wa biblia nzima(kuhusu wokovu Mungu alioukusidia kabla ya kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu na akautimiliza katika Yesu Kristo).

Mungu aliwaagiza walawi moto wa Madhabahu wautunze uwake daima na usizimike, maana yake ilikuwa nini? Moto tu kila siku uchochewe kuni uendelee kuwaka daima usizime kwa nini?.

Mambo ya Walawi 6

12  Na huo moto ulio madhabahuni atautunza uwake daima juu yake, usizimike; naye kuhani atateketeza kuni katika moto huo kila siku asubuhi; naye ataipanga sadaka ya kuteketezwa juu yake, naye atayateketeza mafuta ya sadaka za amani juu yake.

13  Moto utatunzwa uwake juu ya madhabahu daima; usizimike.

Ili huo moto uendelee kuwaka ulihitaji matunzo,ilihitaji kila siku asubuhi kuhani aweke kuni kwenye moto ili huo moto uendelee kuwaka, maana yake kama hata ingepita siku nzima bila kuhani kuweka kuni kwenye moto wa madhabahuni ule moto ungezima.

Ni sawa sawa na wewe unapowasha moto ili uendelee kuwaka kwa muda mrefu lazima uongeze kuni/ikiwa ni jiko la mkaa pia ni lazima uongeze mkaa usipofanya hivyo huo mkaa au huo moto wa kuni utazima tu haijalishi ni mkubwa kiasi gani lazima utazima.

_Sasa ni jambo lipi Mungu analotufundisha?_

Awali ya yote ni muhimu sana kufahamu jambo hili kwamba sisi ni wakina na nani kwa sasa, katika agano jipya..

1 Petro 2:9
“Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme , taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu;”

Unaona hapo? Anasema “Bali ninyi ni mzao mteule, UKUHANI wa kifalme” kila mwamini ni kuhani katika agano jipya tofauti na agano la Kale makuhani walikuwa watu maalumu tu walioteuliwa na Mungu tena wakabila la Lawi peke yake. Lakini kwa sasa sote ni makuhani.

Maandiko yanasema tena hilo jambo….

Ufunuo wa Yohana 1:6
“na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.”

Yesu Kristo baada ya kufa na kufufuka akatufanya sisi kuwa ni makuhani wa Kifalme(ni nafasi ya juu mno katika ulimwengu wa Roho)

Ukisoma tena…

Ufunuo wa Yohana 5:10
“ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.”

Unaona hapo? Ametufanya kuwa ufalme (Wafalme)  makuhani hasemi “akawafanya kuwa kuhani bali MAKUHANI ”.

Sasa unapaswa kufahamu wajibu wa kuhani ni nini ikiwa hufahamu basi utakuwa ni kuhani usiyejua wajibu wako na hii ni hatari sana.

Katika Agano la Kale kuhani alikuwa na wajibu wa kutoa sadaka Soma hapo mambo ya Walawi juu,alikuwa na kazi ya upatanisho/kuwapatanisha watu na Mungu, kuwaombea wengine (taifa/wana wa Israeli) nk

Ilikuwa ni wajibu wake kufanya vile kama kuhani wa Mungu sasa katika agano jipya kuhani ana wajibu huo huo na kama asipoutimiza basi moto utazima.

Kumbuka madhabahu ya Mungu iko ndani yako yaani wewe ni kao la Mungu au hekalu la Mungu ambako ndani yake kuna mambo mengi ya kiibada yanatakiwa kufanyika.

Tambua ikiwa wewe ni hekalu maana yake shuguli zinazotakiwa kufanyika ndani ya moyo wako na nje mwilini mwako zinazo husu ibada tu. (Hekalu la Mungu ni mahali pa sara si pa biashara nk) simaanishi hutakiwi kufanya kazi la! Lakini kile kinachotakiwa kufanyika kwako ni nini?..

1 Wakorintho 3:16
“Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?”

Wajibu wako kama kuhani ni upi?.

1.kumtolea Mungu sadaka za sifa na Shukrani.

Ili moto uendelee kuwaka ndani yako lazima uwe ni mtu wa namna hii kama kuhani. Kama makuhani hatumtolei tena Mungu sadaka za Wanyama bali sifa kutoka ndani ya vilindi vya mioyo yetu.

Wakati mwingi ukiwa kazini,shuleni,nyumbani nk msifu Mungu kwa kinywa chako tafakari aliyokutendea,wema wake mshukuru ukiwa mtu wa namna moto hautazimika daima.

Waebrania 13:15
“Basi, kwa njia yake yeye, na tumpe Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake.”

2.Kuwaombea wengine.

Katika agano la Kale ilikuwa ni wajibu wa kuhani kusimama kwa ajili ya wengine yaani kuwaombea wengine.  Je unasimama mbele za Mungu kwa ajili ya wengine?(1 Timotheo 2:1)

Unapowaombea wengine unaombea mwili wa Kristo uwe imara/dhabiti na si kuomba siku  moja bali ni mwendelezo(ili moto uendelee kuwaka unahitaji uwekaji wa kuni endelevu),  kama vile moto ulivyopaswa kuwaka ndivyo hivyo hivyo unapaswa kufanya.

3.Kuhubiri injili na kumtangaza Kristo.

Kuhani katika agano la Kale kuhani alikuwa na wajibu huo kuwakumbusha watu juu ya Neno la Mungu/amri za Mungu na kuwaonya ambao wako katika njia isiyofaa wasifanye hivyo.

Tunawajibu wa kuhubiri injili na kutangaza ukuu wa Bwana Yesu na yake aliyotutendea katika maisha yetu.

1 Petro 2:9
“….mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika
nuru yake ya ajabu;”

4.Kumtumikia Mungu kwa Roho na kweli.

Huduma yako kama kuhani si ya kidini/dhehebu bali ni katika kweli ya ndani zaidi. Yohana 4:23.

Kuwa mtu wa maombi kila siku,kusoma neno moto hivi ndivyo vichochezi vya wewe kuendelea kusimama katika imani.

Ubarikiwe sana.

Maranatha.

Mawasiliano:0613079530.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *