MAANA NYINGINE YA CHACHU

Biblia kwa kina No Comments

MAANA NYINGINE YA CHACHU.

Je! Unafahamu chachu ni nini?.

Chachu kwa lugha ya sasa ni HAMIRA, na kwa kawaida ukiitazama hamira unaweza ukadhani ni unga Fulani hivi, lakini kiuhalisia ule si unga bali ni mkusanyiko wa wadudu wenye uhai kwa lugha ya kitaalamu wanaitwa YEAST, hawa wanadudu ndio wanaofanya kazi ya kumengenya ule unga, na kutoa gasi maalumu ambayo ndiyo inaufanya ule unga uumuke. Kwahiyo hamira sio kama chumvi au sukari ambavyo havina uhai ndani yake, Hamira ni kitu chenye uhai kwasababu ni wadudu wale. Na ndio maana ikiwekwa mahali inaweza kubadili maumbile ya kitu na kukifanya kuwa kingine kabisa..

Kwamfano unga wa ngano ukitiwa hamira, ukila kalmati sio sawa na utakavyokula keki, na sio sawa na utakavyokula tambi au maandazi. Yote hii inafanywa na kazi moja ya Hamira (CHACHU). Kubadilisha maumbile.

Na ndio maana Bwana alitumia Neno “chachu” kuonyesha madhara yanayoweza kumtokea mtu asipojihadhari na hayo atakayoonywa.

Tukisoma.

Marko 8:15 inasema “Akawaagiza, akasema, Angalieni, jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode”.

Mathayo 16:12 “Ndipo walipofahamu ya kuwa hakuwaambia kujilinda na chachu ya mkate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo”.

Hiyo ni maana ya kwanza ya chachu ambayo Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake wajihadhari nayo (yaani mafundisho ya uongo).

Sasa leo kwa neema za Mungu tutajifunza maana nyingine ya chachu, kwa maana Neno la Mungu ni lipya kila siku, limesafika mara saba kama dhahabu inavyosafichwa mara saba kalibuni (Zaburi 12:6). Hivyo Neno la Mungu halina mipaka.

Na maana nyingine ya chachu katika kizazi chetu ni VITU BANDIA vinavyotumika kubadilisha maumbile ya mwanadamu..ambayo tunaweza tukasema ni VIREMBESHI vinavyotumiwa leo hii na wanawake wa kidunia kujirembesha/ kubadilisha sura zao na maumbile yao.

Sasa utanielewa vizuri kwanini hizo ni chachu.

Tukirudi katika ile maana ya chachu..kama tulivyoona kuwa chachu au hamira ni wadudu ambao wakiwekwa kwenye vyakula kama unga… wanafanya ile unga uumuke hata kama ulikuwa mdogo unakuwa mkubwa…

Ndio maana ukirudi kwenye Agano la kale, ilikuwa ni MACHUKIZO kutumia hamira/chachu kwenye vyakula vitakatifu mfano wa zile zinazohusisha madhabahuni.

Mambo ya Walawi 2:11 “Sadaka ya unga iwayo yote itakayosongezwa kwa BWANA isitiwe chachu kabisa; kwa kuwa hamtateketeza chachu, wala asali iwayo yote, kuwa ni sadaka ya kusongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto.”

Na sehemu nyingi tu utaona Bwana anaagiza wana wa Israeli wasitumie chachu kwenye vyakula vya kiibada, soma kutoka 12:19, Walawi 6:16, Hesabu 28:17, kumbukumbu 16:3.

Sasa kwanini ilikuwa ni machukizo kuweka chachu kwenye vyakula vya kiibada.. sababu ni ile ile kuwa chachu ina tabia ya kubadilisha maumbile ya chakula na kuwa na umbile ambalo kwa nje linaonekana ni chakula halisi kumbe ndani hakuna kitu (chachu inadanganya).

 

Umewahi kukuta maandazi ambayo kwa nje yanavutia, yanaonekana ni makubwa kumbe ndani hakuna kitu, ulijisikiaje ulipochukua ukaenda kula?…bila shaka hukujisikia vizuri…ulisema ningejua nisingechukua.

Ndio maana Mungu alikuwa hataki mkate uliotiwa chachu, na hata sasa anachukizwa na chachu!

Ndio maana alitangulia kutuonya.. tujihadhari na chachu, sio ile ya mikate tena..Hapana ni yale mafundisho ya uongo ambayo kwa nje yanaonekana yana ukweli kumbe! ni uongo mtupu.

Na ndio maana sasa tukirudi kwenye kiini cha somo letu, utakuwa umeelewa kwamba kwanini kutumia VIJEREMBESHI kama zile mekaups, lipustiks, wanja n.k ni MACHUKIZO kwa Mungu, ni kwasababu hiyo ni sawa na chachu.

Unapotumia mekaup unaondoa mwonekano wako wa asili, unakuwa na sura ya UONGO, vile vile unapoweka rangi mdomoni kwenye lips unakuwa na lips ya uongo, unakuwa na kucha za uongo, na kope za uongo, kwa nje unaonekana ni mzuri na unavutia lakini Mungu anakuona wewe sio yule halisi aliyekuumba.

Ikiwa wewe kama mwanamke wa kikirsto..tambua kuwa wewe ni mwili wa Kristo na mwili wa Kristo ni ule mkate ambao Bwana alisema..

Mathayo 26:26 Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu.”

Umeona! Ule mkate ulikuwa ni mwili wa Kristo na haukutiwa chachu yoyote, Kristo hakutumia hizo virembeshi, Utasema ni kwasababu alikuwa ni mwanaume..sawa lakini fahamu sasa kuwa sisi tuliomwamini (kanisa) ni mwili wake pasipo kujalisha jinsia.. Utasema ni wapi tunalidhibitisha hilo kwenye maandiko.

Waefeso 1:22 “akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo

23 ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.”

Soma tena Wakolosai 1:18.

Kwahiyo mbali na kuwa miili yetu ni nyumba ya Roho Mtakatifu sawa sawa na 1Wakorintho6:19 lakini pia sisi ni mwili wa Kristo kabisa.

Mama/Dada acha kuiga mitindo ya kiulimwengu, mwili wako ni mali ya Kristo, biblia inasema..

1 Petro 3:3 “Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi;

[4]bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.

[5]Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao.”

Maandiko yanasema WACHUKIZAO sehemu yao ni lile ziwa liwakalo moto na kibiriti (Ufunuo 21:8)

Jihadhari na chachu!! Jihadhari na chachu!!

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *