
WITO WA YONA
Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe daima. Karibu tujifunze Neno la Mungu ambalo ndio mwanga wa njia yetu na Taa iongozayo miguu yetu.
Leo tutajifunza wito wa Mungu kupitia mtu mmoja katika biblia ambaye aliitwa na Mungu, lakini yeye akaamua kujiepusha na sauti ya Mungu akaenda katika njia zake, na huyu si mwingine zaidi ya Nabii Yona.
Yona alikuwa mmoja wa manabii wa Israeli wakati wa utawala wa Yeroboamu Mfalme wa Israeli, ambaye Mungu alimtumia sana kutoa unabii kadha wa kadha katika Israeli, kama tunavyomsoma katika (2Wafalme 14:21-25). Lakini ilifika wakati BWANA akataka kumtuma kwa watu wa Mataifa, Mji wa NINAWI uliokuwa mji mkuu wa Taifa la ASHURU ambalo kwa wakati ule lilikuwa ni moja ya ngome yenye nguvu duniani ndilo lililokuja baadaye kuhusika kuwachukua wana wa Israeli utumwani (2Wafalme 18:11), Mataifa mengine yakiwemo BABELI pamoja na MISRI. Kumbuka taifa la Ashuru liliyachukua yale makabila 10 na kuyapeleka Ashuru, na makabila mawili ya Israeli yaliyosalia (Yaani YUDA na BENYAMINI) Mfalme Nebukadneza, alikuja kuyachukua utumwani Babeli.
Hivyo mji wa NINAWI uliokuwa mji mkuu katika Ashuru ulijaa maovu mengi sana, mfano wa Sodoma na Gomora, mpaka kufikia wakati Bwana kutaka kuuangamiza mji wote na watu wote waliokuwepo kule, lakini Mungu alivyo wa rehema hawezi kufanya jambo lolote kabla hajawaonya kwanza watu wake, ili pengine waghahiri uovu wao wasiangamizwe, na ndivyo alivyofanya kwa kumtuma YONA nabii katika mji ule Mkubwa uliokuwa mbali sana na taifa la Israeli.
Lakini tunasoma habari haikuwa hivyo kwa nabii YONA, badala ya kwenda NINAWI mji wa ASHURU alioagizwa na Bwana, yeye akaamua kuubuni mji wake yeye alioupenda ili akakae huko, ndipo akakimbilia TARSHISHI mji uliokuwa nchi ya Lebanoni ili tu AJIEPUSHE NA MAPENZI YA MUNGU.
Kabla hatujaendelea mbele, ni vizuri kufahamu kuwa Mungu anapomuita mtu, hapo hapo naye shetani anamuita!, Yona aliposikia sauti ya Mungu inamuita aende Ninawi, labda wakati anajiuliza uliza akasikia ndani yake sauti nyingine inamwambia aende Tarshishi(mawazo yalimjia).
Kumbuka Yona alikuwa anafahamu kabisa sauti ya Mungu kwani si mara ya kwanza Mungu kusema naye, na kwakuwa alikuwa na uzoefu wa kusikia sauti ya Mungu katika mazingira tofauti tofauti… hivyo akajua kabisa akienda kule Tarshishi, hatasikia tena hiyo sauti ya Mungu..lakini hilo wazo limetoka kwanza kwa ibilisi.
Sasa Tarshishi ulikuwa ni mji gani?
Mji wa Tarshishi ni mji ambao ulikuwa mahali panapoitwa Tiro..ambapo kwa sasa ni nchi ya Lebanoni…Nchi ya Lebanoni ni nchi iliyopo kaskazini mwa Israeli, kama vile Kenya ilivyo kaskazini mwa Tanzania (Na mpaka leo hiyo nchi inaitwa hivyo hivyo Lebanoni haijabadilika, inakaliwa na Waarabu sasahivi, lakini haina tena utajiri/ushupavu uliokuwa nao wakati ule)..
Sasa wakati wa vipindi vya wafalme wa Israeli nchi hii ya Tiro (Lebanoni) ambao mji wake mkuu ni Tarshishi ndio ulikuwa ni mji wa kibiashara mkubwa kuliko miji mingine yote. Ulikuwa unasifika kwa kuwa na MERIKEBU NYINGI ZA KIBIASHARA kuliko miji mingine yote. Na ulikuwa ni mji wenye uzoefu wa ki-biashara
Biblia inasema katika kitabu cha Ezekieli…
Ezekieli 27:12 “Tarshishi alikuwa mfanya biashara kwako, kwa sababu ya wingi wa utajiri wa kila aina; kwa fedha, na chuma, na bati, na risasi, walifanya biashara, wapate vitu vyako vilivyouzwa”
Yeremia 10: 9 “Iko fedha iliyofuliwa ikawa mabamba, iliyoletwa kutoka Tarshishi, na dhahabu kutoka Ufazi,….”.
Huko Tarshishi walikuwepo pia manahodha waliobobea sana, na pia kulikuwa na watu wenye elimu ya ujenzi kubwa sana..baadhi ya wajenzi wa hekalu lile la mfalme Sulemani aliwatolea huko huko Lebanoni.
Hivyo ipo mistari mingi sana katika biblia inayoelezea ushupavu wa Tarshishi…ipo mingi sana unaweza kuipitia kwa muda wako upatapo nafasi…Kasome (Ezekieli 27: 25-27, Ezekieli 38:13, 1Wafalme 22: 48, ).
Sasa kwa kuielewa sifa ya Huu mji wa wa Tarshishi tunaweza kujua ni kwanini Yona alikimbilia huko…Na kwanini alipanda merikebu…Kumbuka kutoka Israeli mpaka Tarshishi(huko Lebanoni) kulikuwepo na njia ya nchi kavu nzuri tu..lakini yeye alikwenda kupanda merikebu. Ni sawa leo mtu atake kwenda Tanga..aache kupanda basi achague kutumia ferry/meli pale bandarini Dar es salaam aende Tanga. Ni lazima anayo sababu ya kufanya hivyo.
Na ni wazi kuwa sababu yenyewe si nyingine Zaidi ya biashara…Yona pengine alikuwa na mizigo yake anakwenda kufanya biashara.. Tarshishi haukuwa mji wa kitalii..ulikuwa ni mji wa kibiashara..hivyo alipoisikia sauti ya Mungu ikimwambia aende Ninawi kuhubiri yeye akaona njia pekee ya kuipotezea hiyo sauti ni kuzama kwenye biashara zake…wala hakuchagua kukimbilia miji mingine kama Misri, au Moabu ambayo angepata pumziko..yeye alikuwa na sababu ya kwenda Tarshishi.. Angalau apate riziki kidogo.
Nini tutajifunza hapa, wito wa shetani siku zote ni kumpeleka mtu Tarshishi, na njia atakayomptisha ni baharini. Labda unajiuliza Tarshishi ni wapi na bahari ni nini?
Biblia inatoa tafsiri ya bahari kuwa ni jamaa na makutano na mataifa (kwa ufupi ni ulimwengu).
Ufunuo wa Yohana 17:15 “Kisha akaniambia, Yale maji uliyoyaona, hapo aketipo yule kahaba, ni jamaa na makutano na mataifa na lugha”.
Kwahiyo shetani akimuita mtu..moja kwa moja anampeleka baharini (ulimwenguni), ili akafanye biashara Tarshishi asisikie sauti ya Mungu (masumbufu ya maisha).
Luka 8:14 Na zilizoanguka penye miiba ni wale waliosikia, na katika kuenenda kwao husongwa na shughuli na mali, na anasa za maisha haya, wasiivishe lo lote.
“Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na MASUMBUFU YA MAISHA HAYA; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo;
[35]kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima”.(Luka21:34)
Lakini kumbuka huko baharini ndiko alipo yule mnyama aliyemmeza Yona!!.
Ufunuo 13:1 Kisha nikaona mnyama akitoka katika bahari, mwenye pembe kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru.

Ndugu, leo hii Mungu anapokuita umtumikie Usiikimbie sauti ya Mungu, Mungu anapokuita uokoke…tii wito wa Mungu, kumbuka usipoitii..shetani yupo hapo hapo kwenye mawazo yako ili akugeuzie baharini uende Tarshishi, usiidharau sauti ya Mungu unayoisikia kila siku kupitia injili ya kweli, hata hapa yamkini Mungu anasema na wewe tii hiyo sauti. Kumbuka ni kama bahati tu Yona alipata neema mipango yake ilikatishwa katikati haikukamilika…..angeweza kuachwa aende huko anakokwenda na Mungu akamtafuta mtu mwingine wa kwenda Ninawi kuhubiri na watu wa Ninawi wakaokoka lakini Yona huko alikokimbilia akafanikiwa na utajiri wake lakini akafa na huku hajalitimiza kusudi la Mungu aliloletewa duniani, na mwisho wa siku kupotea katika ziwa la moto milele.
Hivyo leo isikie sauti ya Mungu lipo kusudi la wewe kuwepo hapa duniani la kufanya mapenzi ya Mungu.. usilikimbie kusudi hilo.
Tubu leo leo maanisha kuacha dhambi na ulimwengu, mgeukie Bwana Yesu akufanye kuwa chombo chake cha heshima na hayo mengine ya ulimwengu huu utayapata ndani ya YESU.
Kumbuka tunaishi ukingoni mwa nyakati, parapanda imekaribia kulia sana.
Bwana Yesu akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618