LITAZAME JIWE HILI

Biblia kwa kina No Comments

LITAZAME JIWE HILI

Jina la Mkuu wa Uzima (YESU KRISTO, Mwamba wa Milele), libarikiwe.

Biblia inasema lipo Jiwe moja la gharama sana, na gumu sana, na lililo hai, linalokua na kuzaa..

Kwa kawaida Mawe, hayaishi, ni vitu visivyo na uhai. Lakini biblia inasema lipo Jiwe moja la kipekee ambalo LINAISHI!!.. Hilo ni tofauti na mawe mengine, mawe mengine ni magumu lakini hayaishi, ni mazuri kimwonekano lakini hayana uhai, ni ya gharama sana, lakini hayana uzima, hayakui, hayazai, hayaongezeki.

Na jiwe hilo si jingine zaidi ya YESU KRISTO.

1Petro 2:3 “ikiwa mmeonja ya kwamba Bwana ni mwenye fadhili.

4 Mmwendee yeye, JIWE LILILO HAI, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima”.

Jiwe hili lilianza dogo sana, katika tumbo la Bikira Mariamu.. likazidi kukua katika uweza na nguvu. Mpaka kufikia miaka 33 na nusu, liliongezeka nguvu, na thamani baada ya kushinda mauti, na sasahivi limeunuliwa juu sana, na siku moja litarushwa kutoka juu mpaka chini duniani na kuvunja vunja falme zote za ulimwengu, na litakuwa Mlima mkubwa, na litazaa milima mingine mingi, ambayo ndiyo sisi.

Danieli 2:34 “Nawe ukatazama hata jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe hilo likaipiga sanamu miguu yake, iliyokuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande……………………

36 Hii ndiyo ile ndoto, nasi tutaihubiri tafsiri yake mbele ya mfalme.

44 Na katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni ATAUSIMAMISHA UFALME AMBAO HAUTAANGAMIZWA MILELE, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali UTAVUNJA FALME HIZI ZOTE VIPANDE VIPANDE NA KUZIHARIBU, NAO UTASIMAMA MILELE NA MILELE.

45 NA KAMA VILE ULIVYOONA YA KUWA JIWE LILICHONGWA MLIMANI bila kazi ya mikono, na ya kuwa lilivunja-vunja kile chuma, na ile shaba na ule udongo, na ile fedha, na ile dhahabu; basi Mungu aliye mkuu amemjulisha mfalme mambo yatakayokuwa baadaye; na ndoto hii ni ya hakika, na tafsiri yake ni thabiti.”.

Jiwe hilo lililo hai ni YESU KRISTO. Linaishi, ndio maana unaona hapo katika maandiko, linaonekana kukua na kuwa mlima mkubwa, na hatimaye kuzaa mawe mengine na hayo mawe kuwa milima mingine mingi… na milima hiyo ndio sisi tuliomwamini, ambao tutakaokuja kutawala pamoja naye katika utawala wa miaka elfu.

1Petro 2:5 “NINYI NANYI, KAMA MAWE YALIYO HAI, MMEJENGWA MWE NYUMBA YA ROHO, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo”

Lakini wote ambao hawatamwamini Yesu katika maisha haya, Jiwe hili litakuja kuwaponda ponda..

1Petro 2:6 “Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika.

7 BASI, HESHIMA HII NI KWENU NINYI MNAOAMINI. BALI KWAO WASIOAMINI, JIWE WALILOLIKATAA WAASHI, LIMEKUWA JIWE KUU LA PEMBENI.

8 TENA, JIWE LA KUJIKWAZA MGUU, NA MWAMBA WA KUANGUSHA, KWA MAANA HUJIKWAZA KWA NENO LILE,WASILIAMINI,NAO WALIWEKWA KUSUDI WAPATE HAYO”.

Litumainie hili jiwe lililo hai, mengine yote yana thamani lakini hayana uzima, Wafalme wa dunia wana thamani lakini hawana uhai, ni mawe yasiyoishi, Wakuu na wenye mamlaka ni mawe magumu kama almasi yenye thamani nyingi lakini hayana uhai…(kwasababu almasi ijapokuwa ni ya thamani kuliko mawe yote, lakini si kitu kinachoishi). Lakini Yesu ni Jiwe lililo hai, tena lenye thamani, na linaloharibu. Hilo ndilo la kulitumainia na kulitafuta.

Zekaria 3:8 Sikiliza sasa, Ee Yoshua, kuhani mkuu, wewe na wenzako waketio mbele yako; maana hao ni watu walio ishara; kwa maana, tazama, ninamleta mtumishi wangu, aitwaye Chipukizi.

[9] MAANA, LITAZAME JIWE HILI nililoliweka mbele ya Yoshua; katika jiwe moja yako macho saba; tazama, nitachora machoro yake, asema BWANA wa majeshi, nami nitauondoa uovu wa nchi ile katika siku moja.

Mtazame Yesu Kristo jiwe lililo hai.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *