Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?

Uncategorized No Comments

Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?

Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze maneno ya uzima.

Kabla hutujaendelea mbele hebu tafakari haya..

>Je! tumaini lako lipo wapi?

>Je! uzima wako upo wapi?

>Je! Hazina yako ipo wapi?

>Je umejitajirisha kwa nani?

Bila shaka majibu unayo mwenyewe..

Lakini hekima ya Mungu inatushaurije..

Luka 12:16-21 “Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana;

[17]akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu.

[18]Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu.

[19]Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi.

[20]Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! NA VITU ULIVYOJIWEKEA TAYARI VITAKUWA VYA NANI?

[21]Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.

Ni kweli ni vizuri kuweka akiba…ni vizuri kujitajirisha, ni vizuri kuzijaza ghala zetu, na masanduku yetu ya hazina, lakini jiulize swali moja, siku ukifa ghafla, hivyo ulivyojiwekea akiba vitakuwa vya nani? Hayo mashamba yatakuwa ni ya nani?..na wewe utakuwa wapi?

Mfalme Sulemani, ambaye alikuwa Mfalme Tajiri kuliko wote katika historia, kuna wakati ulifika alivichukia vyote alivyokuwa anavihangaikia, baada ya kufikiri siku atakayokufa…aliwaza na kuona mambo yote aliyoyahangaikia ni ubatili.

Mhubiri 2:17 Basi, nikauchukia uhai; kwa sababu kazi inayotendeka chini ya jua ilikuwa mbaya kwangu; yaani, mambo yote ni ubatili na kujilisha upepo.

[18]Nami nikaichukia kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo chini ya jua; maana sina budi kumwachia yeye atakayenifuata.

[19]Naye ni nani ajuaye kama huyo atakuwa mwenye hekima au mpumbavu? Hata hivyo atatawala juu ya kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo, ambamo ndani yake mimi nimeonyesha hekima chini ya jua. Hayo nayo ni ubatili.

[20]Kwa hiyo nikageuka kukata tamaa moyoni mwangu juu ya kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo chini ya jua.

Mfalme Sulemani, ambaye alipata vyote, mwisho wa siku alivichukia vyote..na akahitimisha kwa kusema maneno haya..

Mhubiri 12:13 Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa;ย Mche Mungu, nawe uzishike amri zake,ย Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.

[14]Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.

Kumcha Mungu na kuepukana na uovu, ndio utajiri tunaopaswa TUUTAFUTE!.. Ndiyo hazina tunayopaswa tujiwekee, ambapo hata tukiondoka ghafla katika haya Maisha huko tuendako tunakuwa na uhakika wa uzima wa milele.

Lakini leo hii usipomcha Mungu na kuepukana na uovu, na huku unajitumainisha katika vitu ulivyo navyo, au kwa vitu utakavyokuwa navyo, nataka nikukumbushe kuwa utakufa, na utaviacha hapa, na kule kuzimu hautavikuta, na wala hutarudi tena duniani kuvipata ulivyoviacha, utakuwa umepotea milele.

Ayubu 7:9 Kama vile wingu likomavyo na kutoweka,ย Ni vivyo huyo ashukaye kuzimuni hatazuka tena kabisa.

[10]Hatarudi tena nyumbani kwake,ย Wala mahali pake hapatamjua tena.

Hivyo huu ni wakati wa kutubu dhambi na kuokoka, ni wakati wa kuukataa ulimwengu, kwasababu ulimwengu na mambo yake yote unapita, lakini Neno la Mungu litadumu milele (1Yohana2:17).

Kama hujaokoka, basi leo ni vizuri ukafanya uamuzi wa kumgeukia YESU, wala usingoje kesho.

Ikiwa upo tayari kuokoka leo, na unahitaji huo msaada basi wasiliana nasi kwa namba zilizopo chini ya makala hii nasi tutakusaidia bure kabisa.

Bwana akubariki.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *