NINI HILI ULILOLIFANYA?

Biblia kwa kina No Comments

NINI HILI ULILOLIFANYA?

Nakusalimu katika jina kuu sana lipitalo majina yote la Bwana wetu Yesu Kristo, Nakukaribisha katika kujifunza maneno ya uzima.

Tunasoma, kitabu cha mwanzo baada ya Adamu na Hawa kwenda kinyume na maagizo ya Mungu kwa kulila lile tunda, tunasoma Mungu aliwatembelea bustanini wakati wa jioni kama ilivyokuwa kawaida yake, Lakini siku hiyo akawakuta wamejificha, Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia uko wapi? Lakini Adamu akajibu nilisikia sauti yako nikaogopa kwa kuwa nipo uchi. Mungu akaendelea kumuhoji ni nani aliyekuambia upo uchi? Akasema..

Mwanzo 3:11 “Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale?

[12]Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.

Sasa nataka tuangalie na kutafakari kwa umakini mstari unaofuata..tuone hili swali ambalo BWANA alimuuliza Hawa, maana kuna jambo leo tutaenda kujifunza hapo kwa neema za Mungu.

13 BWANA Mungu akamwambia mwanamke, NINI HILI ULILOLIFANYA? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala”.

BWANA anamuuliza Hawa Nini hili ulilolifanya. Yaani kwa maana nyingine umefanya nini!! Neno hili ni kubwa sana ukiitafari kwa umakini.

Kosa moja alilolifanya Hawa kusikiliza yale mahubiri ya nyoka na kukubalianaye (kula tunda), ilisababisha mambo yote kuharibika, yaani kwa kosa lile tu mfumo wote ambao Mungu alikuwa ameweka kwa Adamu na vizazi vyake viliharibika. Ilikuwa ni hasara kubwa sana. Ndiyo maana Mungu alimuuliza kwa huzuni NINI HILI ULILOLIFANYA?

Umewahi kufanya jambo Fulani ambalo wewe ulilichukulia ni jambo la kawaida tu, labda tuchukulie mfano umeingia kwa mtu kama mgeni, na ukapewa maagizo ya kula vyakula Fulani, lakini ukapewa tahadhari usile chakula Fulani. Lakini wewe kwa kutaka kujua ladha ya hicho chakula ukachukua ukakionja..halafu mwenye nyumba anarudi baadaye anakukuta umeanza kupata shida katika mwili wako, anakuambia je! umegusa hichi chakula nikichokuambia usiile? wewe ukajibu kwa wepesi tu ndiyo. Na yule mtu akashutuka, akakuuliza tena akikuhuzunikia ni nini hichi ulichokifanya? Chakula hicho ulichokila kina sumu kali!! Na madhara yake ni makubwa mno..hayataondoka leo hata ukitibiwa, utabakia na hayo madhara siku zote za maisha yako na zaidi hata watoto wako utakaowazaa watakuwa na madhara hayo. NINI HICHI ULICHOKIFANYA? umeharibu kila kitu!!

Ndicho kilichowatokoea wazazi wetu Adamu na Hawa, wao waliona ni kosa dogo tu walilolitenda kula lile tunda. Hawakujua kupitia kosa lile maisha yao yote yangeharibika, hawakujua kuwa baada ya kufanya hivyo kila kitu kitakuwa kimeathirika mpaka wanyama, ndege, ardhi, n.k, Hawa aliharibu mfumo wote wa maisha.

BWANA kumuuliza umefanya nini? Sio kwamba alikuwa hajui alichokifanya, lakini alikuwa anaona madhara yatakayotokea baada ya hilo kosa moja tu. Alikuwa anaona vifo, taabu, huzuni, mateso, mauwaji, kusalitiana, kuchukiana, magonjwa, na mambo yote mabaya tunayoyaona leo tayari Mungu alikuwa ameshaiona kupitia lile kosa hayo yote yatakuja kutokea.

Jambo ambalo kurudisha kila kitu kikae sawa kama hapo mwanzo sio rahisi kama Adamu na Hawa walivyokuwa wanafikiri, ilimgharimu tena Mungu amtengeneze mwanadamu tena kwa upya, autengeneze tena mwili mwingine usio na shida, atengeneze tena mbingu mpya na nchi mpya isiyo na shida.

2Petro 3:13 “Lakini, kama ilivyo ahadi yake, mnatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake.

Soma pia Isaya 65:17 & Ufunuo 21

Na hapa ndipo linalokuja suala la kuzaliwa mara ya pili! Usipozaliwa mara ya pili huwezi kuona hiyo mbingu!!

Yohana 3:3 “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu”.

Kwanini bila kuzaliwa mara ya pili hatuwezi kuingia wala kuona, jibu ni kwasababu ya lile kosa alilolifanya Hawa na Adamu. Ni lazima tutengenezwe tena upya, na haya matengenezo yanaanzia katika roho na kisha baadaye mwili. Ni lazima tutengenezwe utu wetu wa ndani ulioharibika kupitia dhambi ya Adamu, na pia utu wetu wa nje/miili yetu ifanywe upya tena, tuvikwe miili mingine tena kwasababu tayari hii imeharibika, haina kigezo cha kuingia katika mbingu mpya na nchi mpya..maandiko yanasema

1Wakorintho 15:50 Ndugu zangu, nisemayo ni haya, ya kuwa nyama na damu haziwezi kuurithi ufalme wa Mungu; wala uharibifu kurithi kutokuharibika.

[51]Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,

[52]kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.

[53]Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa.

[54]Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda.

Umeona hapo, nyama na damu (hii miili) haiwezi kurithi ufalme wa Mungu, ni lazima tupewe miili mingine isiyo na uharibifu, isiyo na tamaa, isiyo na mauti, isiyoumwa.. ndivyo Adamu na Hawa walikuwa wanaishi pale Hedeni kabla hawajaharibu kila kitu kwa lile kosa moja tu.

Lakini, nini kikubwa tunaweza kujifunza katika habari hii; tunachoweza kujifunza hapa katika siku ya leo ni kwamba kosa moja tu linaweza kuharibu maisha yetu yote mpaka ya umilele.

Ikiwa umeokoka kweli kweli yaani umezaliwa mara ya pili kwa mbegu isiyoharibika (Neno la Mungu), basi ni lazima siku zote uchukue tahadhari usije ukafanya kosa alilolifanya Adamu/Hawa.

Na moja ya dhambi ambayo inaweza ikaharibu maisha yako yote, huduma yako, karama yako, upendo wako, amani yako, furaha yako, ikaharibu mahusiano yako na Mungu na hata ukapoteza uzima wa milele ni dhambi ya UZINZI/UASHERATI.

Hii ndiyo dhambi iliyosababisha mambo yote kuharibika na kuwa kama hivi leo ilivyo, ndiyo chanzo cha dhambi zote na matatizo yote kwa mwanadamu na viumbe vyote, ndiyo chanzo cha mauti ya nje mpaka ya ndani.

Utauliza je! tunda walilokula Adamu na Hawa walifanya uzinzi? Ndiyo walifanya uzinzi!,

Maana ya kula tunda kama inavyoonekana pale ni kusikiliza na kutafakari na kukubadiliana na jambo Fulani unaloambiwa..kwamfano Leo hii mwanaume mwasherati anapotafuta mwanamke wa kuzini naye atakwenda kumwambia(kumlisha) maneno ya kumuhadaa kama vile kumwahidi kumuoa, atamfanya kuwa malkia wake, atampa vitu vya kifahari na maisha mazuri n.k..lakini nia ya yule mwanaume Ni kuzini nae tu kisha akishamaliza aachane naye kwahiyo ni lazima atumie njama hizo ili kumpata vinginevyo hatampata. Kwahiyo hicho kitendo cha mwanamke kusikiliza na kushawishika na hayo maneno ya hadaa ndio kulishwa tunda. Hivyo hivyo ndivyo ilivyotokea kwa hawa na nyoka. Kitendo cha hawa kusikiliza hadaa za nyoka aende kinyume na maagizo ya Mungu kule ndio kula tunda hasaa na uasherati na mambo mengine yote yakafuata mbele.

Kwahiyo ni muhimu kufahamika tunda lililolika pale sio tunda kama apple au mengine kama wengi wanavyodhani, kula apple au peas hakuwezi kumfanya mtu ajione kuwa uchi, na kama kula apple lilikuwa ni kosa lililomsababisha mwanadamu aanguke ingekuwa mpaka leo wanadamu wanaanguka kwa kula ma-apple, lakini ni dhahiri kilichofanyika pale ni uasherati, ni dhambi ambayo Mungu anaichukia tangu kile kipindi mpaka leo, hiyo ndiyo dhambi ya asili.Na ndio dhambi inayowaangusha watu wengi hata leo, na hilo tunda mpaka leo bado watu wanalila kila siku.

Hivyo ndugu/dada uliyezaliwa mara ya pili kwa kuoshwa dhambi zako kwa damu ya Yesu na ukamua kujikana nafsi na kumfuata Bwana Yesu kwa utakatifu wote wa ndani na nje (mwili na roho), JIHADHARI na dhambi hii, Neno la Mungu linasema kwamba tuikimbie zinaa, sio tuishi nayo, au tuikemee!..bali tuikimbie (Soma 1Wakorintho 6:18 )…kama vile Yusufu alivyoikimbia mbele ya mke wa Potifa, na sisi tunapaswa tuikimbia hivyo hivyo, Yusufu hata hakukubali kuzungumza na Yule mwanamke..

Kumbuka miili tuliyonayo sasa zimebeba tamaa, hivyo tujichunge sana, tusiikaribie vichoche vyovyote vya uzinzi, tukae mbali na picha chafu, mavazi yanayochochea uzinzi, mitandao na makundi ya wazinzi…na mahusiano ya kiholela hole yasiyo rasmi(girl friend/boyfriend). Kumbuka leo hii shetani anaweza akakuhubiria uzini mara moja tu, na wewe bila kufikiri matokeo yake ukakubaliana na hayo mahubiri, lakini kumbe ndio unaenda kuharibu maisha yako yote kupitia hicho kitendo cha dakika kadhaa tu. Tuwe makini sana.

Na kama hujaokoka, au umeokoka kidini ni heri tu ukamua kuokoka leo ingali bado una nafasi, kumbuka baada ya kufa au baada ya parapanda hakuna nafasi nyingine tena ya kuokoka. Hivyo ikiwa unahitaji msaada wa kuzaliwa mara ya pili leo .. wasiliana nasi kupitia namba uzionazo chini ya makala hii nasi tutakusaidia bure.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *