
HUKUMU IKAWEKWA NA VITABU VIKAFUNGULIWA.
Danieli 7:9 “Nikatazama hata viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao.
[10]Mto kama wa moto ukatoka ukapita mbele zake; maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake; HUKUMU IKAWEKWA, NA VITABU VIKAFUNGULIWA”.
Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze tena maneno ya Mungu.
Kama wengi wetu tunavyojua kuwa, siku ya Bwana inakuja, siku ya hukumu yake ambapo Bwana atauhukumu ulimwengu kwasababu ya ubaya wake..(Isaya 13:11 inasema hivyo)
Na katika siku ya Mwisho,wafu wote watafufuliwa na Kiti cheupe cha Hukumu kitawekwa na Yesu Kristo ataketi juu yake, na kila mtu, mmoja baada ya mwingine atasimama mbele yake atoe hesabu ya mambo yake yote aliyoyafanya tangu siku alipozaliwa mpaka siku aliyokufa, yote hayo yatamulikwa katika kioo kikubwa sana, na kuonekana mbele ya watu wote na hapo ndipo kila mtu atapata sifa yake, au aibu yake. (1Wakorintho 4:5)
Litaonekana tendo moja baada ya lingine, liovu au la haki litaonekana pale…kama mtu alikuwa ni mwasherati yataonekana matukio yote aliyoyafanya ya uasherati, siku aliofanya, mtu aliyefanya naye, mwaka, mwezi, mpaka dakika na sekunde alizokuwa anafanya…na watu wote wataona hakutakuwa na siri, kama mtu aliyafanya tendo Fulani la haki nalo pia litaonekana mwaka, siku, mpaka sekunde ya tendo hilo. Iwe alifanya kwa siri au kwa wazi yote yatakuwa bayana.
Na ni kwanini Mungu anataka watu wote waone?..Ni kwasababu yeye ni muhukumu wa haki na hivyo asitokee mtu yeyote atakayesema Yule kaonewa au Yule kapendelewa, watu wote watashuhudia matukio ya yaliyokuwa yanaendelea miongoni mwa watu.
Yohana 5: 28 “Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake.
29 Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, NA WALE WALIOTENDA MABAYA KWA UFUFUO WA HUKUMU”.
Unaona hapo, kila mmoja atahukumiwa sawa sawa na matendo yake, rejea tena katika..
Danieli 12:2 Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele.
Je! unaweza tena ukasema maneno hayo yameandikwa kwa bahati mbaya? Danieli aliona siku hii ya hukumu jinsi itakavyokuwa, na Bwana Yesu naye anakuja kuthibitisha jambo hili. Lakini hebu tusome tena shahidi mwingine wa tatu.
Ufunuo wa Yohana 20:11 Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana.
[12]Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; NA VITABU VIKAFUNGULIWA; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.
[13]Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.
[14]Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto.
[15]Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.
Hivyo ndugu yangu, siku ya hukumu inakuja, ambayo kila mtu atahukumiwa sawa sawa na matendo yake. Katika siku hiyo vitabu vitafunguliwa, na hukumu itawekwa, hivi vitabu kama tunavyosoma hapo juu vipo viwili. KITABU CHA UZIMA na VITABU VINGINE,. Hapo unaona kitabu cha uzima kinaonekana ni kimoja tu!. Lakini pia kuna vitabu vingine, ikiashiria ni vingi.
Hivi vitabu vingine ni VITABU vinavyoelezea habari za wanadamu kulingana na biblia inavyosema. kila mwanadamu anacho cha kwake, kikimwelezea maisha yake jinsi alivyoishi hapa duniani kwa muda wote aliopewa hapa duniani kuanzia kuzaliwa kwake mpaka kufa kwake. Na vitabu hivi vina kurasa, ambazo ni hatua unazopitia hapa duniani, Lakini hivi vitabu vyote havina uzima ndani yake, kitabu cha UZIMA ni kimoja tu, na ndio maana hivi vyote vinakitegemea hicho cha UZIMA kutoa hatma ya mwanadamu.
Kwahiyo kile kitabu cha UZIMA kinaelezea kanuni na taratibu za mwanadamu anavyopaswa aishi hapa duniani ili aupate huo uzima uliondikwa ndani yake, hivyo basi kama wanadamu tunaoandika vitabu vya maisha yetu tunapaswa tuviandike vifanane na kile cha UZIMA ambacho si kingine zaidi ya BIBLIA, kuanzia utoto wetu mpaka kuondoka kwetu duniani vitabu vyetu vinatakiwa vifanane na cha UZIMA, na huko ndiko KUONEKANA KWA MAJINA YETU KATIKA KITABU CHA UZIMA.
Hivyo ndugu kitabu chako unakiandikaje? angalia muda unavyokimbia! usiseme nitampokea Kristo au nitaishi maisha matakatifu nifikisha umri fulani au nikishapata kitu fulani. Jua mpaka sasa kitabu chako kinaendelea kuandikwa na ndivyo kurasa zinavyozidi kufunguka na kufunga, muda unavyozidi kwenda ghafla utajikuta kitabu chako kimefungwa kinasubiriwa kufunguliwa kwenye ILE SIKU YA HUKUMU.
Na siku ile ya Hukumu kile cha UZIMA kitafunguliwa na cha kwako pia kitafunguliwa, vitalinganishwa, kama vinafanana au la! ‘”HUKO NDIKO KUHAKIKIWA JINA LAKO”. Kama Jina lako halikuonekana inamaanisha kitabu chako (maisha yako), Hayaendani na kile cha UZIMA (yaani Biblia, NENO LA MUNGU). Hivyo basi kwa kuwa hauna UZIMA ndani yako sehemu yako itakuwa katika lile ziwa liwakalo Moto na kibiriti.
Kama mkristo maisha yetu kila siku tunapaswa tuyalinganishe maisha yetu na biblia, je! tukifanyacho kinaendana na kitabu cha uzima?. unafahamu kabisa waasherati, wazinzi, walevi, watukanaji, waabudu masanamu, waongo, wasengenyaji, mashoga, wasagaji, wavutaji sigara, wafanyaji wa mustarbation, watazamaji wa pornography, waizi, mafisadi,waendaji kwa waganga na wapiga ramli, wala rushwa, wauaji, nk, watu wa dizaini hii maisha yao yapo mbali na kile kitabu cha UZIMA, unategemea vipi uonekane katika kile kitabu, kumbuka majina yanayozungumziwa pale sio John, Yohana au Mary bali ni maisha yako, Jihakiki ndugu komboa wakati siku hizi ni za mwisho.
Maombi yangu ni wewe umgeukie Mungu. Anza kukiandika kitabu chako vizuri katika muda wako wa maisha uliobakiza hapa duniani, kila siku kifananishe kitabu chako na cha UZIMA ili siku ile ikifika JINA LAKO LIONEKANE. UIEPUKE HUKUMU.
Mungu akubariki!
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.