
KUBALI KUIPOTEZA NAFSI YAKO ILI UIPATE
Shalom. Karibu tujifunze hekima ya kiMungu, Neno lake lililo taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu (Zaburi 119:105).
Ukichunguza kwa umakini zaidi jinsi mambo yalivyo, utagundua kuwa hekima ya dunia inavyoenenda ni tofauti kabisa na wakristo wanavyopaswa kuenenda. Ndio maana Bwana Yesu alituambia maneno haya ambayo tunayasoma katika..
Mathayo 20:25 “Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha.
26 LAKINI HAITAKUWA HIVYO KWENU; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu;
27 na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu;”
Hii Ikifunua kuwa hekima ya dunia hii ni kinyume na hekima ya Mungu…Hekima ya dunia hii, mdogo anamtumikia Mkubwa…lakini Hekima ya kimbinguni mkubwa ndiye anayemtumikia mdogo….
Hekima ya kidunia inasema ukimbilie ukubwa ili usiwe mtumwa…lakini hekima ya kimbinguni inasema ukimbilie udogo ili uwe mkubwa…
Hekima tena ya kidunia inasema…Mpende akupendaye na umchukie anayekuchukia…lakini hekima ya kimbinguni inasema “mpende adui yako mwombee yeye anayekuudhi”..adui yako akiwa na njaa mlishe, akiwa na kiu mnyweshe…(Soma Mathayo 5:44 na Warumi 12:20).
Lakini sasa tukirudi katika kiini cha somo letu hekima ya dunia hii inasema ukiipatia nafsi yako kila kitu chema cha ulimwengu huu ndio maana ya maisha…lakini hekima ya Mungu inasema “aipataye nafsi yake ataipoteza na aipotezaye kwa ajili ya Kristo ataipata”……
Mathayo 16:25 “Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.
26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?
Kwahiyo karibia mambo yote ya huu ulimwengu yanakwenda kinyume na hekima ya Mungu…Ndio maana inakuwa ni ngumu mtu wa kidunia kumwambia kwamba kuna siku hii dunia tunayoishi itafikia mwisho na kwamba mwisho huo umekaribia sana na siku moja hili jua tunaloliona litatiwa giza…atakuona ni mtu wa ajabu kwasababu yeye anaona dunia mbona bado ni mahali salama?..itawezekanikaje jambo hilo..kwamba eti siku moja jua litiwe giza?..Atakuona kuna kau-pumbavu Fulani kapo kichwani mwako..
Ndio maana biblia ikasema katika..
1 Wakorintho 1:18 “Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.
19 Kwa kuwa imeandikwa, Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, Na akili zao wenye akili nitazikataa.
20 Yu wapi mwenye hekima? Yu wapi mwandishi? Yu wapi mlete hoja wa zamani hizi? Je! Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa ni upumbavu?
21 Kwa maana katika hekima ya Mungu, dunia isipopata kumjua Mungu kwa hekima yake, Mungu alipenda kuwaokoa waaminio kwa upuzi wa lile neno linalohubiriwa.”
Unaona?..Hebu leo hii itafute hii hekima ya Mungu..ambayo imekataliwa na watu wengi..kubali kuipoteza nafsi yako ili uipate.
Biblia inasema..”heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka”. (Luka 6:21), hii ikiwa na maana kama leo unapitia huzuni, kwa ajili ya Imani yako, unachekwa na kudharauliwa na kuonekana kuwa wewe ni takataka kwasababu umeamua tu kumfuata Kristo basi ujue kuwa hapo mbeleni kuna kuheshimiwa na kuogopwa, na kutukuzwa kwa ajili ya Jina la YESU KRISTO.. Hiyo ndiyo kanuni..
Ukiona leo umeacha kila kitu, umekuwa tayari kupoteza hata kazi yako, au biashara yako, au mali zako, au elimu yako au hadhi yako kwa ajili ya Yesu au kwa ajili ya Injili ya Kristo isonge mbele,.. basi fahamu kuwa kupata mara 100 ya hivyo ulivyovipoteza ipo mbele yako..haijalishi itachukua miaka 5,10 au 20 au 50 lakini kabla haujafa Mungu atahakikisha amelitimiza hilo neno lake juu yako.
Mathayo 19:27 “Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?
28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.
29 Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele”.
Vivyo hivyo tukiona sisi wakristo tumeupoteza ulimwengu wote.,kwa ajili kumtazama Kristo na ufalme wake wa milele, mpaka tunaonekana kama vile watu tusiostahili kuwepo katika ulimwengu huu, basi tujue kuwa,.. Huu huu ulimwengu tutaupata, maana biblia inasema dunia hii itarithiwa na wenye upole( watakatifu)..Na hiyo itatimia katika utawala wa miaka 1,000 unaokuja huko mbeleni.
Mathayo 5:5 “Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi”.
Lakini kinyume chake pia ni kweli, ukiona sasa umeupata ulimwengu wote, basi ujue tayari umeshaupoteza,..Ukiona kila aina ya ouvu duniani unaokuja wewe ni wako, disko ni zako, uzinzi ni wako, ulevi ni wako, starehe zote ni zako, rushwa ni yako,… wizi ni wako, dhuluma ni zako, tamaa za ujanani ni zako, vimini na suruali ni zako, ulevi ni wako, starehe zote ni zako, rushwa ni yako,… wizi ni wako, dhuluma ni zako, tamaa za ujanani ni zako, vimini na suruali ni zako, viduku, na milegezo ni yako..uzinzi ni wako, fashion ni zako…Basi ujue kuwa safari yako ni fupi hapo mbeleni, nyakati za shida zinakuongojea..
Hivyo usifurahie kuwa unayo afya nzuri sasa na huku upo mbali na Kristo,.. usifurahie unayo elimu kubwa na huku hujazaliwa mara ya pili, unacho hichi aunacho kile, ni mrembo, ni mzuri,..fahamu kuwa Mungu ameruhusu faraja yako ikujie sasa ili wakati wa wenzako kufarijiwa wewe uwe unalia na kusaga meno..
Zaburi 62:7 “Wasio haki wakichipuka kama majani Na wote watendao maovu wakistawi. Ni kwa kusudi waangamizwe milele”
Kama wewe upo nje ya Kristo utajisikiaje usikie unyakuo umepita leo na wewe umebaki?., wakati wenzako wanafarijiwa milele mbinguni katika ile karamu ya mwana kondoo wewe upo hapa chini ukisubiri ziwa la moto wa milele. Ni majuto kiasi gani, ukikumbuka kuwa ulishahubiriwa injili mara nyingi na ukapashupaza shingo yako.
Embu leo sema Bwana Yesu usinipite, ninakukaribisha maishani mwangu tangu sasa. Sema hivyo ukimaanisha kabisa kutoka katika moyo wako kuwa kweli kuanzia leo umeamua kumfuata yeye..Ukiwa umepiga magoti yako mwombe akusafishe dhambi zako zote kwasababu hapo ulipo yupo ili kukusikia,.. tubu kabisa hata kwa machozi, na yeye hapo ulipo atakusamehe na kukupa amani ya ajabu ndani ya moyo wako..
Ukishaona hivyo, na amani imekuja ndani yako ujue amekusamehe,..unachopaswa kufanya usihangaike hangaike na huu ulimwengu bali haraka tafuta kanisa zuri la kiroho linalomuhubiri Kristo,.. uende pale, vilevile ukiwa hukubatizwa ipasavyo unapaswa ufanya haraka sana kutimiza agizo hilo muhimu Bwana Yesu alilotupa kwa kila mtu atakayeokoka, Kwamba wote tubatizwe katika ubatizo mmoja kwa jina lake..
Zipo batizo nyingi duniani ambazo si za kimaandiko lakini ubatizo sahihi ni ule wa kuzamishwa katika maji mengi (Yohana 3:23), na uwe ni KWA JINA LA YESU KRISTO sawasawa na Matendo 2:38..
Baada ya hapo Roho Mtakatifu atakutia muhuri na atakuwa kiongozi wako milele kukuongoza na kukulinda mpaka ile siku ya Unyakuo itakapofika ikiwa bado utakuwa hai.
Bwana akulinde, Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.