
Je! Udongo umwambie yeye aufinyangaye; Unafanya nini?
Isaya 45:9 “Ole wake ashindanaye na Muumba wake! Kigae kimoja katika vigae vya dunia! Je! Udongo umwambie yeye aufinyangaye; Unafanya nini? Au kazi yako, Hana mikono?
Udongo unaozungumziwa hapo ni sisi wanadamu, na Mungu ndiye mfinyazi/muumbaji.
Yeremia 18:1-6 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, kusema,
[2]Ondoka, ukashuke mpaka nyumba ya mfinyanzi, na huko nitakusikizisha maneno yangu.
[3]Basi nikashuka mpaka nyumba ya mfinyanzi, na tazama, alikuwa akifanya kazi yake kwa magurudumu.
[4]Na chombo kile, alichokuwa akikifinyanga, kilipoharibika mkononi mwake yule mfinyanzi, alikifanyiza tena kuwa chombo kingine, kama alivyoona vema yule mfinyanzi kukifanya.
[5]Ndipo neno la BWANA likanijia, kusema,
[6]Ee nyumba ya Israeli, je! Siwezi mimi kuwatendea ninyi vile vile kama mfinyanzi huyu alivyotenda? Asema BWANA. ANGALIENI, KAMA UDONGO ULIVYO KATIKA MKONO WA MFINYAZI, NDIVYO MLIVYO NINYI KATIKA MKONO WANGU, Ee nyumba ya Israeli.
Kwasababu hiyo basi, Neno la Mungu linasema ”Ole wake ashindanaye na Muumba wake..”
Je! udongo umwambie yeye aufinyangaye/aumbaye Unafanya nini? Kwanini kuniumba hivi?. Ni wazi kuwa hilo haliwezekaniki kabisa.
Lakini sisi, tunashindana na Muumba wetu aliyetufinyanga kwa jinsi apendaye. Utauliza ni kwa namna gani tunashindana naye?
Tunapobadilisha ule muonekano wa miili yetu tuliyoumbiwanayo, kwa mfano unapobadilisha rangi ya ngozi yako, kucha zako, nywele zako tayari unashindana na Muumba wako? Na kumwambia kwanini kuniumba hivi.!!.
Warumi 9:19-21 “Basi, utaniambia, Mbona angali akilaumu? Kwa maana ni nani ashindanaye na kusudi lake?
[20]La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwani kuniumba hivi?
[21]Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?
Yeremia 13:23 Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya.
Hebu angalia leo, je! hiyo rangi ya ngozi uliyonayo ni ile uliyopewa na Mungu kweli?, na rangi ya kucha zako, na nywele je ni zile za Mungu au tayari umebadilisha? Je hizo alama ulizochora katika mwili ni za nini? Na hayo masikio uliyotoboa na kuweka mabangili je ni kwamba Mungu alikosea au alisahau kukuumbia?
Isaya 29:16 Ninyi mnapindua mambo; Je! Mfinyanzi ahesabiwe kuwa kama udongo; kitu kilichofinyangwa kimnene yeye aliyekifinyanga, Hakunifinyanga huyu; au kitu kilichoumbwa kimnene yeye aliyekiumba, Yeye hana ufahamu?
Hebu leo badilika ingali bado mlango wa rehema haujafungwa.
Acha kushindana na Muumba wako? Ondoa mapambo yote katika mwili wako, acha kutafuta uzuri mwingine zaidi ya uliyopewa? Kwani unataka umpendeze nani zaidi? Huoni kuwa shetani anakudanganya ili ukatupwe kwenye ziwa la moto kama yeye.
Unaposikia Neno la Mungu na hutaki kugeuka hapo tayari unashindana na Muumba wako pia? Neno la Mungu limekuambia usivae mavazi yasiyopasa jinsia yako (kumbukumbu22:5), lakini hutaki kusikia, “OLE WAKE ASHINDANAYE NA MUUMBA WAKE.”
Neno la Mungu limekuhubiria utubu dhambi zako na kuziacha kisha ukabatizwe kwa jina la Yesu (Matendo 2:38) lakini hutaki kusikia. Unashindana na Muumba wako? Utaepukaje hukumu ya jehanumu?
Umeambiwa vaa mavazi ya kujistiri (1Timothea2:9) na kama mwanamke funika kichwa chako ukiwa Ibadani (1Wakorintho11:3), lakini hutaki kusikia. Acha kushindana na Muumba wako, kumbuka wewe ni udongo!!.
Amua leo kutii injili hii na mgeukie Muumba wako, mpokee YESU ili upate ondoleo la dhambi.
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.