
Mavazi ya kujistiri ni yapi?
Biblia inatufundisha tuvae mavazi ya kujistiri na kuwa na adabu nzuri.
1Timotheo 2:9 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;
[10]bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu”.
Sasa ili tufahamu mavazi ya kujistiri ni ya aina gani, hebu tuangalie muonekano wa Bwana Yesu alipomtokea Yohana katika kisiwa cha Patmo.
Ufunuo 1:9-18
[9]Mimi Yohana, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na subira ya Yesu Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu.
[10]Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu,
[11]ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika chuo, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba: Efeso, na Smirna, na Pergamo, na Thiatira, na Sardi, na Filadelfia, na Laodikia.
[12]Nikageuka niione ile sauti iliyosema nami. Na nilipogeuka, niliona vinara vya taa saba vya dhahabu;
[13]na katikati ya vile vinara nikaona mtu mfano wa Mwanadamu, AMEVAA VAZI LILILOFIKA MIGUUNI, na kufungwa mshipi wa dhahabu matitini.
[14]Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe, kama theluji; na macho yake kama mwali wa moto;
[15]na miguu yake kama shaba iliyosuguliwa sana, kana kwamba imesafishwa katika tanuru; na sauti yake kama sauti ya maji mengi.
[16]Naye alikuwa na nyota saba katika mkono wake wa kuume; na upanga mkali, wenye makali kuwili, ukitoka katika kinywa chake; na uso wake kama jua liking’aa kwa nguvu zake.
[17]Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho,
[18]na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.

Sasa huu muonekano wa Bwana Yesu una ufunuo wake kwa kanisa, lakini nataka uone hilo vazi alilovaa. Ni vazi lililofika mpaka miguuni…hii ni kuonyesha mavazi ya wacha Mungu yakoje.
Mkristo wa kweli hawezi kuvaa mavazi ya nusu uchi au makaptula halafu akajiona amevaa mavazi ya kujistiri, atajiona anajiabisha.
Bwana Yesu hapo hakuonekana amevaa nusu uchi, wala hakuvaa kaptula..bali alivaa vazi lililostiri mwili wake mpaka miguuni.
Jiulize wewe unayesema umeokoka na Yesu ni Bwana, kama Bwana wako anavaa kwa kujistiri, kwanini wewe unavaa vimini, na nguo za kubana. Hujui hayo ni mavazi ya kikahaba na ni machukizo kujiita mkristo na huku unavaa kikahaba.
Mtume Petro alipomuona Bwana akiwa uchi alijitupa bahari kustiri kifua chake mbele za Bwana, yakupasaje wewe mwanamke wa Kikristo kujistiri mbele za Bwana ikiwa Petro ni mwanaume lakini aliona ni afadhali ajitupe majini kuliko kubaki vile na mavazi yake ya kuvulia.
Yohana 21:7
[7]Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro, Ndiye Bwana. Naye Simoni Petro, aliposikia ya kwamba ni Bwana, akajifunga vazi lake, (maana alikuwa uchi), akajitupa baharini.
Kama kweli umeokoka na unaye Roho Mtakatifu, huwezi kuvaa mavazi ambayo kila mtu akikuona anazini na wewe kwa kukutamani, huwezi kuvaa suruali mwanamke ukajiona umevaa nguo. Kama kweli unaye Roho Mtakatifu yule ninayemjua mimi, hawezi kuruhusu uvae suruali kabisa, kwani unapovaa suruali mwanamke, kutokana na maumbile yako suruali inachora makalio yako na hivyo unakuwa unahubiri uzinzi pasipo kujua au kwa kujua. Ndio maana Neno la Mungu linasema..
“Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; kwa maana kila afanyaye mambo hayo ni machukizo kwa BWANA, Mungu wako”.(Kumbukumbu 22:5)
Halikadhalika ukiwa umeokoka kweli kweli huwezi kuvaa modo (nguo za kubana), au nguo za kisanii (crazy), Roho Mtakatifu hawezi kukuruhusu uvae namna hiyo.
Kwahiyo, kwa hitimisho ili ujue kuvaa kwa kujistiri kama iwapasavyo wakristo, ni lazima uwe na Roho Mtakatifu ambaye atakuongoza na kukufundisha namna ya kuvaa kama mkristo.
Na biblia inasema wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu (Warumi 8:14), na mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake. (Warumi 8:9)
Hivyo usiishie tu kusema umeokoka na unaenda kanisani na huku hauna Roho Mtakatifu!. Haitakufaidia kitu.
Na ishara inayokutambulisha kuwa hauna Roho Mtakatifu bali una roho nyingine ni hayo mavazi ya kikahaba unayoyavaa na hauoni hata haya kupita barabarani, huku unajifariji na kufarajiwa kuwa Mungu haangalii mavazi anaangalia roho.
Acha kujidanganya na kudanganywa, amua leo kubadilika na kuokoka kweli kweli upokee Roho Mtakatifu ili usije ukapata majuto ya milele utakapojikuta upo jehanumu. (Kumbuka kule hakuna atakayekusaidia majuto yako na kukufariji tena, kwani kila mtu atakuwa na majuto yake mwenyewe).
Matendo ya Mitume 2:37-39
[37]Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?
[38]Petro akawaambia, TUBUNI MKABATIZWE KILA MMOJA KWA JINA LAKE YESU KRISTO, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
[39]Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.
Maran atha. (Bwana Yesu anakuja).
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.