
LAKINI USIKU WA MANANE PAKAWA NA KELELE.
Kama wewe ni mfuatiliaji wa unabii wa biblia na mwenye kujua nyakati na majira tunazoishi…basi bila shaka unajua kuwa kuja kwa Bwana wetu YESU KRISTO kumefananishwa na wale wanawali kumi waliokuwa wakingoja kumlaki Bwana wao atakapokuja waende naye arusini, Na tukisoma tunaona ilipofika usiku wa manane wote waliishiwa nguvu, na kusinzia kwa kuona Bwana wao anakawia kwa kungojea sana, Lakini ghafla usiku ule ule pakawa na ”KELELE kubwa ikisema Tazama! Bwana arusi anakuja.
Mathayo 25:1 “Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi.
[2]Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara.
[3]Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao;
[4]bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao.
[5]Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi.
[6] LAKINI USIKU WA MANANE, PAKAWA NA KELELE, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki.
[7]Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao.
[8]Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika.
[9]Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie.
[10]Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa.
[11]Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie.
[12]Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi.
[13]Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa”.
Hizo kelele zinazozungumziwa hapo sio zile zisizo na maana!! Bali ni uamsho wa kumuamsha bibi-arusi (kanisa) lijaandae kumlaki Bwana arusi. Na kama tunavyosoma ilikuwa ni usiku wa manane, ikimaanisha wakati wa giza kuu (giza la rohoni).
Kwahiyo kitendo kile cha zile kelele kuwaamsha hawa wanawali 10 kutoka usingizini huo ndio ule ‘Mwaliko’ unaozungumziwa kwenye 1wathesalonike 4:16-1.
1wathesalonike 4:16-17 “Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na MWALIKO, na SAUTI YA MALAIKA MKUU, na PARAPANDA YA MUNGU; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele”.
Hapo anasema “Bwana atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko” sasa hili neno “mwaliko” kama linavyozungumziwa hapo halimaanishi ule mwaliko wa kama mtu anaalikwa kwenye sherehe fulani hapana! Bali inamaanisha Kelele za nguvu zinazoambatana na nderemo na vifijo kuashiria kuwa mtu fulani wa kipekee anakaribia kuwasili mfano, Raisi, Bwana arusi n.k,… Hii ni kwa kusudi la kumfanya mtu anayemngojea kujiweka tayari kumlaki atakapofika langoni mwake, ili isiwe ghafla ghafla.
Ili kuelewa vizuri tusome tena kifungu hichi katika tafsiri nyingine ya biblia.
1Thessalonians 4:16 KJV ” For the Lord himself shall descend from heaven with a shout, with the voice of the archangel, and with the trump of God: and the dead in Christ shall rise first”:
Sasa Hapo neno ‘Shout’ linamaanisha ni kupaza sauti kuu za kelele kwa nguvu, ili kumfanya mlengwa aamke au awe makini kujianda na tukio linalokwenda kutokea mbele… linganisha na ule mstari katika Mathayo25 unaosema USIKU WA MANANE PAKAWA NA KELELE,
Kwahiyo zile kelele ni kwa lengo la kuwaamsha/kuwaalika wale wanawali 10 wakamlaki Bwana arusi. Na ndivyo ilivyo katika tukio la kurudi kwa Bwana kuja kuchukua bibi arusi wake (kanisa lake) biblia inasema, Bwana atashuka pamoja na mwaliko… ni kwa dhumuni la kumwamsha bibi arusi ili ajiweke tayari kwa kwenda kumlaki Bwana wake. Na kama huo mwaliko usingepita kwanza hakuna mwanawali yoyote angeweza kutambua kuja kwa Bwana wake, wote ingewajia kama mwivi, Hivyo jambo hili kutangulia ni mahususi ili kumfanya aamke usingizini na kuaacha mambo yake anayoyafanya yote aanze kuiweka taa yake sawa, kwasababu muda waliokuwa wanauongojea umewasili.
Na mwaliko huu ulianza wakati Kanisa lilipokuwa limelala, katikati ya usingizi mzito (usiku wa manane), kama tunavyosoma katika historia kanisa limepitia kipindi cha giza kuu kwa muda mrefu (dark age) katika nyakati ya kanisa la tatu hadi la nne, baada ya roho ya mpinga Kristo kuliharibu, kwa mafundisho ya upotofu pale ukristo ulipooana na upagani na kuendelea hivyo kwa muda mrefu sana wa mamia ya miaka (312AD-1520AD).
Sasa muda wote huo ulikuwa ni muda kanisa lilikuwa limelala, Lakini ulipofika wakati wa Bwana kushuka kulijilia kanisa lake tena, hakuja ghafla, kwasababu hakuna ambaye angestahili kwenda naye, alianza kwanza na kutanguliza Mwaliko wake, ni ujumbe wa kumwamsha kwanza bibi arusi kutoka usingizini yaani (mwaliko) na kumfanya aiweke tayari taa yake na ahakikishe pia inayo mafuta ya ziada (mafuta ni Roho Mtakatifu na mafuta ya ziada ni ufunuo wa Roho wa Mungu).
kwahiyo huu MWALIKO ni UAMSHO wa Roho ambao unatangaza ujio wa Bwana Yesu kulichukua kanisa lake na watu wajiweke tayari kumpokea Bwana wao. Kama tulivyoona katika (Mathayo 25:6..na ilipofika usiku wa manane pakawa na ”KELELE Bwana arusi anakuja”).
Sasa huu mwaliko ulianza na Martin Luther mjumbe wa kanisa la tano, ukaendelea hivyo hivyo na John Wesley mjumbe wa kanisa la sita, Na mwisho Bwana aliutoa tena kwa kupitia mjumbe wa kanisa la saba (William Branham), Bill Graham, Oral Robert na wengineo.
Kumbuka sauti hiyo ya mwaliko ilianza kusikika kutoka mbali, na ilivyokuwa inazidi kukaribia ndivyo ilivyozidi kuwa kubwa zaidi, Hivyo sauti ya mwaliko wa kanisa hili la mwisho la Laodikia ni kali, kuliko ilivyokuwa kwa kanisa la tano au la sita. Kwasababu Bwana yupo mlango kufika amtwae Yule mwanawali mwerevu aliyeitii sauti ya mwaliko. Kumbuka ndugu Ujumbe tulionao sasa hivi ni KUTOKA kabisa katika mifumo ya dini na madhehebu na kuanza kuishi maisha ya utakatifu, kama mtu anayemngojea Bwana wake, Huko ndiko kuzitengeneza Taa zetu.
Biblia inasema..Luka 12: 35 “Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na TAA ZENU ZIWE ZINAWAKA
36 nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, ATAKAPORUDI KUTOKA ARUSINI, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara.
36 nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, ATAKAPORUDI KUTOKA ARUSINI, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara.
37 Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia”.
Unaona hapo?..MWALIKO wa kuja kwa Bwana ulishaanza tangu wakati wa kanisa la tano, na la sita, na unaendelea na la saba.
Hizi ni nyakati za mwisho kweli kweli na Bwana yupo mlangoni, je! bado unafanya mzaha na haya maisha?? bado unaupenda ulimwengu unaokwenda kuisha, unaendelea kuwa mwasherati, mlevi,mwongo,mwizi, mlafi, msengenyaji, unaendelea kuvaa vimini, mawigi na mahereni, na kupaka wanja, lipstick, na fashion??
Bado unaendelea kuwa mlevi,na mtazamaji pornography, bado unaendelea kuwa msagaji, mlawiti na mfanyaji masturbation? Bado unaendelea kuwa mtukanaji, Kuzimu! Ipo usidanganyike!Tafuta Roho Mtakatifu Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, Muda umeenda sana. Leo hii tubu kisha ukabatizwe katika ubatizo sahihi kwa jina la Yesu Kristo, kisha Bwana mwenyewe atakupa ahadi ya Roho Mtakatifu aliyowaahidia waitakayo.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.