
TAFUTA VAZI LA ARUSI UNYAKUO UPO KARIBU!
Awali ya yote tukumbuke kuwa lengo la kunyakuliwa sisi ni ili kwenda kula karamu ya arusi ya mwanakondoo mbinguni, aliyoiandaa Yesu Kristo kwa ajili yetu, kama alivyosema katika Yohana 14:1-4 na Ufunuo 19:9. Hivyo kama tunavyojua hakuna sherehe yoyote isiyokuwa na mwaliko. Hakuna mtu anayejikuta tu kwenye arusi ya mtu bila kualikwa, hakujawahi kuwa na utaratibu huo. Na ndivyo Yesu naye, kabla ya kutupelekea huko mbinguni alipotuandalia vinono, ni sharti kwanza atualike. Hapo ndipo akatumia mfano mmoja wa Mfalme aliyemfanyia mtoto wake karamu kubwa. Lakini katika kuwaalika watu wake, kukawa na mwitikio tofauti tofauti,
Embu tuisome habari hiyo tupate kuielewa vizuri; (Soma kwa utulivu) kwasababu hapa ndipo palipo na msingi.
Mathayo 22:1 “Yesu akajibu, akawaambia tena kwa mithali, akisema,
2 Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi.
3 Akawatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja arusini; nao wakakataa kuja.
4 Akatuma tena watu kwa wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng’ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini.
5 Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake;
6 nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua.
7 Basi yule mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao.
8 Kisha akawaambia watumwa wake, Arusi i tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili.
9 Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini.
10 Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni.
11 Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, AKAONA MLE MTU MMOJA ASIYEVAA VAZI LA ARUSI.
12 Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa.
13 Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
14 Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.
Ukitafakari hapo, utajiuliza, iweje mfalme akualike kwenye sherehe yake halafu usiende?..Ni heri angekuwa mtu wa kawaida, lakini walioalikwa hawakulijali hilo, kwamba yule ni mfalme na sio mtu wa kawaida, hawana budi kuahirisha shughuli zao waende, kwani wamepewa heshima kubwa, lakini kwao mambo yalikuwa tofauti, wakapuuzia na kibaya zaidi wakawapiga na kuwaua baadhi ya watumwa wake.
Sasa hawa wanalinganishwa na wayahudi, ambao ndio waliokuwa wa kwanza kupewa mwaliko huu ya injili, lakini waliwaangamiza, manabii wengi wa Mungu, mpaka ikafikia hatua ya Kristo akawakataa kabisa, akawakatilia mbali (Soma Mathayo 23:37-39). Hivyo Mungu akahamishia mpango wake wa wokovu kwa watu wa mataifa, ambao ndio mimi na wewe.
Ambao tunalinganishwa sasa na hao waovu, na vilema, waliookotwa huko mabarabarani wakaalikwa kwenye karamu. Maandiko yanatuambia kundi hilo halikukataa mwaliko kama lile la kwanza. Bali lilikubali lote, LAKINI SASA ndani ya ukumbi, akaonekana mmoja ambaye alikuwa tofauti na wenzake, yeye hakuwa na “vazi la arusi”. Utajiuliza ni kwanini akose vazi lile? Ni kwanini asifanane na wenzake? Utagundua kuna jambo alilipuuzia, ambalo angepaswa alifanye kabla, ili akidhi vigezo vya yeye kuila karamu.
Sasa kabla hatujatazama vazi hilo ni nini? Maana ya mfano huo ni mwaliko wa wokovu ambao tunahubiriwa sisi sote. Ukweli ni kwamba leo hii lipo kundi kubwa la watu katika kanisa “wanaokiri wokovu”, wengi wao wamebatizwa, wanashiriki ibada kama kawaida kanisani, wanatoa zaka, wote wanakiri kuwa wanamsubiria Yesu aje kuwanyakua. Lakini je! Ni wote watakaonyakuliwa? La! Bwana anasema..Siku ile Mmoja atanyakuliwa mmoja ataachwa!(Mathayo 24:40-41) .. Maana yake ni kwamba hupaswi kuridhika tu kuitwa mkristo, lipo jambo la ziada unapaswa ufanye ili ukidhi vigezo vya kuiila karamu ya mwanakondoo mbinguni. Usiridhike tu kusema mimi ni mshirika, mimi ni muumini, acha kabisa hayo mawazo, katika siku hizi za mwisho tunazoishi, yule mtu aliketi kabisa ukumbini, akaona vinono vyote lakini hakula hata kimoja.
Tukirudi katika hiyo habari, ni kwamba yule mtu ambaye hakuwa na mavazi ya arusi, hakuisikia/aliipuzia sauti ya mjumbe aliyesimama pale mlangoni kuwapa maelekezo ya namna ya kukubaliwa katika karamu. Wakati wenzake wanamsikiliza, walipoambiwa wakaoge, wabadili mavazi yao ya kihuni, ya ki-utupu, ya ki-zinzi, ya ki-dunia. Wavae mavazi meupe ya sherehe, yeye akaona ule ni mzigo mzito sana, anamnyima uhuru wake, akataka kwenda kipekee pekee na staili zake, maadamu ameshapewa heshima ya kualikwa na mfalme. Hawezi kuzuiliwa. Hivyo akaendelea kustarehe vilevile pale ukumbini, akimsubiria mfalme, kuja kuwapongeza wageni wake waliomtii. Lakini alipofika kwake, akidhani, sasa ni wakati wa kupongezwa, akashangaa amebadilikiwa uso, badala ya kupongezwa, ndio kwanza anafungwa Kamba kama vile vibaka, kisha anatupwa nje!
Unajua ni kwanini mpaka biblia inasema ndipo kutakuwa na kilio na kusaga meno, maana yake ni kuwa huyu mtu ambaye alikuwa ameshaweka mawazo yake katika kusheherekea, ghafla anajikuta yupo nje, ni wazi kuwa yeye ndio atakayeumia Zaidi kuliko wale ambao hawakuwahi kualikwa kabisa.
Hivyo kundi hili linafananishwa na watu wote, wanaoitwa wakristo walio kanisani, lakini hawana mavazi ya arusi. linadhani maadamu tayari limeshakuwa mshirika wa kanisa basi hiyo inatosha, maadamu linatoa zaka, basi inatosha, maadamu linaimba kwaya inatosha, hakuna haja ya kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi, hakuna haja ya kuishi maisha matakatifu, hakuna haja ya kuomba, hakuna haja ya kujikana nafsi na kumfuata Kristo, hakuna haja ya kuhakiki ni nini kimpendezacho Bwana, na ni kipi hakimpendezi, lenyewe halina mzigo wowote na dhambi, linachopenda ni kuhubiriwa mafanikio tu, na kubarikiwa, lakini likigusiwa habari za toba halipendi.
Kufanya uzinzi ni kitu cha kawaida kwao, kuvaa nguo za nusu uchi si jambo ajabu pia, kuvaa suruali (wanawake) linaona ni sawa, kunywa pombe ni sawa, kwenda disko ni sawa, kukaa kwenye kampani za kidunia hakuna shida yoyote..
Sasa hawa katika ulimwengu wa roho, ni kweli walialikwa arusini lakini hawakuwa tayari kulitwaa vazi jeupe la harusi ambalo ndio kama tiketi ya kuingia karamuni. Na vazi la Arusi ni UTAKATIFU. Maandiko yanasema hivyo.
Ufunuo 19:7 “Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari.
8 Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni MATENDO YA HAKI YA WATAKATIFU.
9 Naye akaniambia, Andika, Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo. Akaniambia, Maneno haya ni maneno ya kweli ya Mungu.
Unaona?, hiyo kitani nzuri, ing’arayo safi ya kuingia karamuni ni matendo ya haki ya watakatifu…Hivyo na sisi hatutaingia mbinguni kwenye karamu ya mwanakondoo kama matendo yetu hayatakuwa ya haki hata kama tutajiita tumeokoka vipi… Haijalishi Bwana Yesu alitutokea, au tuliona maono, au tulitubu mwanzoni na Mungu akasikia toba yetu, kama hatutajizoeza kuishi maisha matakatifu biblia inasema hatutaweza kumwona Mungu pasipo huo (Waebrania 12:14)
Zingatia: unyakuo upo karibu sana kuliko watu wengi wanavyojua..ni muda wowote, kwani dalili zote zinaonyesha kuwa wakati wowote Yesu anarudi, Je! umejiandaaje?
Leo hii unasema umeokoka na unamsubiri aje akupongeze, lakini angalia hauna vazi la arusi. Utajibu nini leo Bwana akija na kukuliza rafiki uliingiaje humu na huna vazi la arusi? (Ilikuwaje kuwaje ukawa umeokoka na hauishi maisha ya utakatifu?)
Utakuwa kama wale wanawali watano wapumbavu ambao nao walikuwa wakimgojea Bwana arusi aje awapongeze lakini kumbe hawana mafuta ya ziada, wakaishia kufungiwa nje wakati wenzao wanafurahi na Bwana arusi kule ndani (Mathayo25), ndivyo itakavyokuwa kwa wale wote wanaojiita ni wakristo kumbe ni wazamiaji tu.
Wakati ni mchache sana tunaishi katika dakika za nyongeza tu, Tengeneza maisha yako sasa, huu sio wakati wa kuhubiriwa injili ya kubembelezwa, ni wewe mwenyewe uone uhalisia utubu. Yesu yupo mlangoni.
Maran atha. (Na uje Bwana Yesu)
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.