
KWANINI KIZAZI HIKI HAKITAPITA !!
Kwasababu Bwana mwenyewe alisema..
“Amin, nawaambia, KIZAZI HIKI HAKITAPITA, hata hayo yote yatakapotimia.
35 Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe”. (Mathayo24:34-35)
Hichi kizazi alichokizungumzia Bwana hapa sio kile kizazi cha akina Petro… kwasababu kile kilishapita miaka 2000 iliyopita.
Hivyo kizazi alichokuwa anazungumzia hapa ni kile kilichoshuhudia mtini kuchipuka na dalili zote za siku za mwisho. Hebu turudi nyuma kidogo.
Mathayo 24:32-35 ” 32 Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu;
33 nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni.
34 Amin, nawaambia, KIZAZI HIKI HAKITAPITA, hata hayo yote yatakapotimia.
35 Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Baada ya Bwana kueleza dalili kadha wa kadha za kurudi kwake na mwisho wa dunia.. ambayo alisema katika siku za mwisho kutatokea vita na matetesi ya vita (mathayo 24:6), kutakuwa na njaa (mwilini na rohoni), matetemeko ya nchi, kutakuwa na magonjwa mengi, mambo ambayo tumekuwa tukiyaona kila kukicha matetemeko kila mahali, magonjwa mapya yanazuka kila siku((kama cancer, kisukari,presha,zika,ukimwi,ebola,sars,kimeta, n.k) ambayo hayakuwepo katika vizazi vya zamani,
Jambo lingine alilolisema ni kuwa manabii na makristo wengi wa uwongo watatokea na kuwadanganya wengi, Kila mtu anafahamu kama tunavyowaona leo mafundisho mengi ya uwongo yamezagaa kila mahali, alisema pia upendo wa wengi utapoa, ni dhahiri kabisa upendo(shauku) ya watu kumpenda Mungu na kupendana wao kwa wao imetoweka,na tamaa mbaya za ulimwengu huu zimewasonga watu na kumsahau Muumba wao, alisema pia watu watakuwa wakijipenda wenyewe, wakisalitiana na kuchukiana.
Ndipo akamalizia na kusema “Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu;
33 nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni.
34 Amin, nawaambia, KIZAZI HIKI HAKITAPITA, hata hayo yote yatakapotimia.
35 Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe”.
Alisema kwa mtini jifunzeni, “Mtini” siku zote kwenye biblia unawakilisha Taifa la Israeli,(soma yeremia 24), na aliposema utazameni mtini na miti mingine,hii miti mingine ni mataifa mengine, sasa aliposema mtini utakapoanza kuchipua alikuwa na maana Taifa la Israel kuzaliwa tena upya baada ya kukaa katika mataifa mbalimbali kwa muda mrefu. Tunaona jambo hili lilitimia mwaka 1948 pale Israeli waliporejea katika nchi yao wenyewe kama ilivyotabiriwa na Bwana, hiyo ndiyo maana ya kuchipuka kwa mtini (Israeli). Hivyo basi kuanzia huo mwaka wa 1948 mpaka sasa tunaona mataifa mengi yalianza kupata uhuru wao ikiwemo mataifa karibu yote ya Afrika, baadhi ya Asia na Marekani ya kusini hii inatimiza ule unabii Yesu aliosema mjifunze pia kwa miti mingine (miti mingine ni sisi mataifa mengine mbali na Israeli).

Sasa baada ya mtini kuchipuka(Israeli) hapo ndipo Bwana aliposema “Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita hata hayo yote yatimie. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.”
Unaona, ni kizazi kilichoshudia kuchipuka kwa mtini na miti mingine.
Na kizazi kilichoshuhudia hayo ni kuanzia watu waliozaliwa mwaka 1948 na kuendelea hadi sasa, kwahiyo tumeshafahamu kuwa kizazi cha wale waliozaliwa mwaka 1948 Bwana Yesu ndicho alichosema hakitapita. Na tunajua kizazi mpaka kitoweke kabisa katika dunia ni miaka 100,kwa dunia ya sasa, tukiangalia tangu mwaka 1948 hadi leo ni miaka 77 imeshapita, na hapa Bwana Yesu alisema kizazi hiki hakitapita, hakusema kitatimia ndio mwisho uje bali alisema hakitapita, kwahiyo hii ina maanisha hapa hapa katikati kabla ya kufikia hicho kipindi cha kizazi kutoweka Bwana Yesu Kristo atakuwa ameshakuja, aliweka msisitizo kabisa akasema “Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita hata hayo yote yatimie. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.”
Na baada ya hapo ndipo Bwana Yesu aliposema mtakapoona hayo yanaanza kutokea tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu, kwa hiyo ndugu tambua hilo wewe unayesema bado sana Yesu kurudi, wewe ambaye unasitasita kwenye mawazo mawili, maneno haya yanaonyesha wazi kabisa kuwa kuja kwa Bwana kuko mlangoni.
Bwana Yesu Kristo hakutoa muda wala saa ya kuja kwake lakini alitupa majira kwamba yatakapokuja yasitujie kama mwivi au kama mtego unasavyo.
Tunaishi katika wakati ambao muda wowote mambo yanaweza kubadilika, Parapanda italia muda wowote na Unyakuo utapita!! Hata leo au sasahivi unaposoma ujumbe huu parapanda itaweza kulia. Kumbuka ikitokea imelia sasa hivi na haujawa tayari unabakia na hakutakuwa na nafasi nyingine tena ya kuokolewa, kilichobaki ni kujiokoa tu mwenyewe kwa damu yako au kupokea chapa ya mpinga-kristo na baadaye kutupwa katika ziwa la moto!!
Na mpinga-Kristo tayari yupo hapa duniani, na mfumo wake wa kutawala dunia ameshaiweka tayari..kinachomzuia tu asijitokeze wazi ni kanisa, lakini hivi punde baada ya watakatifu kunyakuliwa, ataanza kazi yake rasmi na watu wote watamjua na kumkubali wakidhani ni mtu wa amani atakayeleta amani ya dunia, anayejali watu wote na mwenye upendo, wasijue ndiye shetani mwenyewe ndani ya mwili wake.
Hivyo, huu ni wakati wa kuhakikisha tumeokoka kweli kweli na tumejawa Roho Mtakatifu. Kama bado unaendelea na mambo yako ya kidunia, na unajifaraji kuwa Yesu harudi leo, nataka nikuambie una bahati mbaya sana. Na utakuja kujuta sana…leo umepata kujua haya ili uamue kuchukua uamuzi wa kuokoka leo leo kabla hujachelewa maana muda umeisha, we mwenyewe unashuhudia jinsi maovu yanavyozidi kuongezeka kwa kasi ulimwenguni, na jinsi mambo yanavyokwenda. Kizazi hiki hakitapita!!
Bwana Yesu anarudi.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.