FAHAMU KUHUSU UFUFUO WA UZIMA NA WA HUKUMU.

Biblia kwa kina No Comments

FAHAMU KUHUSU UFUFUO WA UZIMA NA WA HUKUMU.

Shalom, Mtu wa Mungu karibu tujifunze Injili, uweza wa Mungu uuletao wokovu. Bwana Yesu alisema maneno haya..

Yohana 5: 25 “Amin, amin, nawaambia, SAA INAKUJA, NA SASA IPO, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai.

26 Maana kama vile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake.

27 Naye akampa amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana wa Adamu.

28 Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini WATAISIKIA SAUTI YAKE.

29 Nao watatoka; wale waliofanya MEMA KWA UFUFUO WA UZIMA, na wale WALIOTENDA MABAYA KWA UFUFUO WA HUKUMU”.

Kama wengi wetu tunavyofahamu kuwa kuna ufufuo utakaokuja baada ya maisha haya kuisha ambapo wale wote waliotenda haki watafufuliwa na kuurithi uzima wa milele, na wale wote waliotenda mabaya watafufuliwa kwaajili ya hukumu, na kila mmoja atahukumiwa kulingana na matendo yake na wale waovu watatupwa katika lile ziwa la moto, lenye moto usiozimika, waangamie milele.

Soma tena..Danieli 12:1-3

“[1]Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo; na wakati huo watu wako wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile.

[2]Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, WENGINE WAPATE UZIMA WA MILELE, WENGINE AIBU NA KUDHARAULIWA MILELE.

[3]Na walio na hekima watang’aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele.

Ukiutafakari kwa makini maneno hayo utakuja kugundua kuwa Kumbe Ufufuo sio tija. Kwasababu watu wote watafufuliwa, waovu na wema..kinachojalisha ni sababu ya kufufuliwa kwako. Kama mtu alikuwa mcha Mungu basi ufufuo kwake utakuwa wa maana, lakini kama alikuwa mwovu basi ufufuo kwake utakuwa ni laana.

Na ufufuo maana yake, ni “kukirudishia tena uhai au maisha ya kitu kile kilichokuwa kimekufa”..hiyo ndio maana ya ufufuo.

Sasa kuna ufufuo wa roho ambao unaendelea sasahivi, ambapo watu wote WANAISIKIA SAUTI YA MWANA WA ADAMU, na wanafufuka kutoka kwa wafu katika roho, zingatia hilo neno alilolisema “SAA INAKUJA, NA SASA IPO” maana yake ufufuo unaendelea hata sasa ukiachilia mbali ule wa siku za mwisho.

Na sauti ya mwana wa Adamu ni Habari njema inayohubiriwa duniani kote leo, habari za msalaba na wokovu uliopo katika Kristo Yesu, sasa wapo ambao wanafufuka kwaajili ya uzima wa milele na wapo ambao wanafufuka kwaajili ya hukumu.

Wako ambao pindi tu wanapoisikia injili macho yao yanafumbuliwa (wanafufuka katika roho), hii inatokea pale ambapo wanachomwa dhamiri zao ndani ya mioyo yao, na kujijua kuwa njia zao sio sawa, hivyo kwa moyo mnyoofu wanaitii injili na kuokoka kikamilifu,wanaacha njia zao mbaya za kale, na kuzaliwa mara ya pili wakati huo huo na kuwa viumbe vipya.

Na wapo pia ambao wanapoisikia tu injili macho yao yanafunguka (wanafufuka) na kujua kabisa ndani ya mioyo yao Neno la Mungu ni kweli, na Roho Mtakatifu anawashuhudia kabisa kuwa Njia ya wokovu ni hii, na njia wanayoiendea wao sio sawa…Roho anawafufua katika roho zao, lakini kwasababu wanapenda giza kulika Nuru wanaikataa ile njia ya kweli,..na kwa makusudi, hawataki kugeuka na kutubu, wanaendelea na njia zao mbaya, hawa ndio wanaofufuliwa sasa kwa ajili ya hukumu. Wanayafumba macho yao kwa makusudi ingawa wamepewa neema ya kuona..Wanafahamu kabisa hata wakifa sasa hivi wanastahili Jeahanum ya Moto, lakini bado hawataki kutubu. Hawa wamefufuliwa kwa ajili ya Hukumu.

Kwahiyo ndugu unayesoma ujumbe huu, usifurahie tu Roho wa Mungu anapokushuhudia ndani yako kuwa KRISTO ndiye njia ya kweli na uzima, huo ni ufufuo tu! Ambao hata waovu wanapewa…hata waovu katika nyakati hizi za mwisho wanapewa neema hiyo mioyoni mwao kujua kuwa Kristo ni njia ya kweli na uzima, na kwamba hakuna uzima wowote nje yake yeye..Hiyo ni neema ya ufufuo ambayo watu wote wanapewa waovu na wema..Lakini swali ni je! Unafufuliwa kwa sababu gani?.

Kama unaisikia injili kila siku inayokuambia ulevi, uasherati, utukanaji, rushwa,uvaaji mbaya ni dhambi, mustarbation, usagaji, na pornography…na ndani ya moyo wako unajua kabisa ni kweli ni dhambi kufanya mambo hayo..fahamu tu! Ufufuo uliopewa ni wa hukumu na sio wa uzima wa milele, haijalishi unayajua maandiko kiasi gani, au umezungumza na malaika kiasi gani,au umemwelewa Kristo kiasi gani, au umeponywa na Yesu kiasi gani,

Mtume Paulo kwa uwezo wa Roho aliandika habari za watu hawa wafanyao dhambi kwa makusudi huku wakijua kabisa wanayoyatenda sio sawa…Wameisikia injili (wakapata ufufuo katika roho zao)..lakini ufufuo wao ukawa ni wa mauti.

Warumi 1: 18 “Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu.

19 Kwa kuwa mambo ya Mungu yanayojulikana yamekuwa dhahiri ndani yao, KWA MAANA MUNGU ALIWADHIHIRISHIA.

20 Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; HATA WASIWE NA UDHURU

21 kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza.

Unaona Biblia inasema..”kwa maana walipomjua Mungu hawakumtukuza” na inasema “Mungu aliwadhihirishia ndani yao”..ikiwa na maana kuwa watu hawa, nuru ya haki iliwazukia ndani yao, au kwa lugha nyepesi tunaweza kusema ufufuo ulipita ndani ya roho zao, wakaiona kweli na kuiamini lakini walipoiamini hawakuifuata!..Hilo ndio jambo la kuogopesha, mtu anauona ukweli lakini haufuati…Nimewahi kuona madaktari bingwa ambao wanajua elimu yote ya biolojia ya ini na figo, na ni washauri wazuri wa kushauri watu wasitumie pombe na sigara kwani ni hatari kwa afya zao, lakini wao ndio watumiaji wakubwa wa mambo hayo, na wanakufa kwa magonjwa hayo hayo…Na ukiwauliza kwanini wanafanya hivyo na hali wanajua kwa kina na mapana madhara ya hivyo vitu katika mwili, zaidi hata ya watu wengine wanavyojua…wanakujibu basi tu! Nimeamua na nimependa kufanya hivyo, na atazidi kukuambia yupo tayari kufa na wala haogopi.

Sasa watu wa namna hii pia wapo katika Kanisa la Kristo, wanajua kanisa uzinzi ni dhambi, kwamba waasherati wote sehemu yao ni katika lile ziwa la moto, na wengine wamepewa maono na ndoto za jehanamu wameonyeshwa mahali wanawake wanaovaa vimini na suruali walipo lakini hao hao utawakuta wanaendelea kufanya hivyo bila uoga wowote. Ni kwasababu gani wanafanya hivyo? Ni kwasababu wapo katika ufufuo wa hukumu. Mpaka unaweza ukasema kwanini Mungu awafunulie mioyo yao waiamini injili halafu na bado wasiifuate si ni bora asingewapa kabisa neema hiyo..kuliko kuwapa halafu wasiifuate?..Jibu ni rahisi… kila mtu lazima aisikie sauti ya mwana wa Adamu na kutoka kaburini aliko”.

Je! Umesikia sauti ya Mwana wa Adamu? Na je baada ya kusikia umepata ufufuo gani?

Kama hujampa Yesu Kristo maisha yako…usikawie kawi tena, Hapo ulipo tubu, dhamiria kuacha dhambi zote ulizokuwa unazifanya nyuma, Fufuka sasa katika ufufuo wa Uzima katika jina La Yesu, na sio ufufuo wa Mauti, mfanye Bwana kuwa tumaini lako kuanzia leo na kuendelea.. Na baada ya kutubu katafute ubatizo kwani ni wa umuhimu sana kukamilisha wokovu wako na ni maagizo ya Bwana mwenyewe aliyoyatoa kwamba ni lazima kila mtu aliyempokea yeye akabatizwe, na ubatizo sahihi ni wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kulingana na

Matendo 2:38, na Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi na kukuongoza katika kuijua kweli yote ya maandiko.

Kumbuka Unyakuo upo karibu sana.. wakati wowote parapanda italia na watakatifu walio lala watafufuliwa wataungana na walio hai na wote watanyakuliwa kumlaki Bwana Yesu mawinguni. Jiulize ikiwa ni leo au kesho utakuwa wapi?

Bwana atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *