
NI INJILI GANI UNAZOZIPENDA KUZISIKILIZA?
Siku hizi za mwisho kuna injili nyingi sana, kuna injili ya kweli lakini pia ipo injili ya uongo. Injili ya kweli ni ile inayopeleka mtu uzimani na ile nyingine inawafanya watu waupende huu ulimwengu ambao unaenda kuisha hivi karibuni.
Na cha kuhuzunisha, watu wengi wanaikimbilia injili hizi za uongo zisizo na uhai, watu wanasema manabii wa uongo wamekuwa wengi sana siku hizi, wasijue ni kwasababu pia ya ongezeko la wakristo wa uongo na watu wasiompenda Mungu, wanaopenda kutabiriwa tu mafanikio ya huu ulimwengu na kuambiwa maneno malaini malaini ili waendelee kuishi katika uovu wao. Mtaji mkubwa wa manabii wa uongo ni wakristo wa uongo, bila wakristo wa uongo kusingekuwapo na kundi kubwa la manabii wa uongo.
Yeremia 5:31 “Manabii wanatabiri uongo, na makuhani wanatawala kwa msaada wa hao; NA WATU WANGU WANAPENDA MAMBO YAWE HIVYO. Nanyi mtafanya nini mwisho wake?
Ndugu jiulize injili unazozisikia mara kwa mara, JE! ZINAKUJENGA PANDE ZOTE AU UPANDE MMOJA TU WA MAFANIKIO YA KIMWILI?…Unafahamu kuwa haya maisha yatakuwa na mwisho?..ulishawahi kulitafakari hilo?, kama unyakuo hautakukuta basi ujue siku yoyote unaweza ukaondoka hapa duniani, na huko uendako je! utakuwa mgeni wa nani? Huko uendako umejiwekea hazina gani?..BWANA YESU ANASEMA ITAKUFAIDIA NINI UUPATE ULIMWENGU MZIMA, NA HUKU UMEPATA HASARA YA NAFSI YAKO?, upate nyumba nzuri, upate gari, upate umaarufu, upate ukubwa na kila kitu na huku unapata hasara ya nafsi yako kwa kumkosa Kristo moyoni mwako??
Siku ile utakapokufa utasema laiti ningejiwekea huku hazina, nisingekuwa mahali hapa pa taabu, Leo hii unafurahia injili ya kuburudishwa na vichekezo na comedy kwenye madhabahu, na huku unajua kabisa umefarakana na Mungu moyoni mwako, na hata ukifa leo unakwenda kuzimu, hujui kuwa kizazi unachoishi ndio kizazi kilicho katika hatari kubwa sana kuliko vyote vilivyotangulia, ni kizazi kilicho katika hatari ya kuuona uharibifu utakaoijilia dunia nzima, hujui kuwa kulingana na kalenda ya kimbinguni tunaishi katika lile kanisa la Mwisho lijulikanalo kama Laodikia ambalo ndilo litakaloshuhudia kurudi kwa pili kwa Kristo?.
Hufahamu kuwa hatua za Unyakuo zimeshakwisha anza, na wewe huna habari, haujui kuwa kazi za mpinga-kristo sasa zipo dhahiri na kiti chake kinajulikana sasa mahali kilipo, wewe upo buzy kukimbilia injili za vichekesho, na kufarijiwa, na huku unadhani upo sawa…Kaa mbali na hao viongozi! Na hizo injili ambazo zimekosa uwiano. Tunaonywa tuwe makini, huu ni wakati wa kutafuta kwa bidii mahusiano yetu binafsi na Mungu, kupata maarifa ya kina juu ya mapenzi yake kwetu sisi wanadamu.
Kama hujampa Bwana maisha yako kihakika, au unasita sita katika mambo mawili, au umezamishwa katika hizi injili za mafanikio zisizokuwa na uwiano za kuchuja mbu na kumeza ngamia, hebu tenga muda jaribu kuweka mambo yote kwenye mizani, jaribu kulitilia mkazo lile lenye uzito mkubwa zaidi na hayo mengine yafuate baadaye.
Kumbuka injili ya kweli inapokufikia hapo ulipo ni neema kubwa sana, ni heri ufungue moyo wako na kuamua kumpa Yesu maisha yako na kuliishi Neno lake, Kwani muda umeisha kweli kweli… muda wowote mlango wa neema utafungwa.
BWANA YESU ANARUDI!!
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.