AKAWAULIZA, BASI MLIBATIZWA KWA UBATIZO GANI?

Biblia kwa kina No Comments

AKAWAULIZA, BASI MLIBATIZWA KWA UBATIZO GANI?

Matendo ya Mitume 19:1-5 “Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko;

[2]akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? WAKAMJIBU, LA, HATA KUSIKIA KWAMBA KUNA ROHO MTAKATIFU HATUKUSIKIA.

[3] AKAWAULIZA, BASI MLIBATIZWA KWA UBATIZO GANI? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana.

[4]Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu.

[5]WALIPOSIKIA HAYA WAKABATIZWA KWA JINA LA BWANA YESU”.

Ndugu mkristo, kuna mambo hayawezi kuja ndani yako PASIPO UBATIZO SAHIHI. Na moja ya jambo ambalo huwezi kupokea pasipo ubatizo sahihi ni Roho Mtakatifu, na hivyo huwezi kuwa mkristo wa kweli.. kwasababu anasema “..Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake”. (Warumi 8:9).

Unaweza ukasema mbona wengine wamejazwa na Roho Mtakatifu pasipo huo ubatizo? Ni kweli huwenda wamejazwa na wakanena kwa lugha mpya, lakini ni vizuri kufahamu Utendaji kazi wa Roho Mtakatifu ni kama ufuatavyo..

Mungu anapomchagua mtu aliye dhambini, huwa anamtumia Roho wake mtakatifu kumvuta mtu yule ndio hapo mtu huyo anaanza kusikia kuhukumiwa dhambi zake moyoni, na hatimaye anafikia toba, sasa huyo ni Roho Mtakatifu siku hizo zote anakuwa anamvuta mtu yule, anakuwa anatembea na yule mtu kama rafiki yake wa pembeni, lakini bado hajaingia ndani yake, ni kama mwanamume anapokuwa katika hatua za awali za kumchumbia mwanamke, anakuwa anaweza kuwa karibu naye, kumpa zawadi chache chache, kuzungumza naye maneno mazuri, kumwonyesha vitu vyake n.k, hayo yote mwanamume anayafanya ili tu kumvuta yule mwanamke, lakini bado yule mwanamke sio mali yake mpaka siku atakayoamua kumkubalia na kufunga naye ndoa, ndipo siku hiyo atakuwa milki halali ya yule mwanamume.

Na Roho Mtakatifu ndio hivyo hivyo, katika hatua za awali, Roho Mtakatifu anaweza akazungumza na mtu, wakati mwingine akampa hata maono, kumfanikisha katika mambo yake n,k lakini akawa bado hajaingia ndani yake, yote hayo Roho Mtakatifu anayafanya ili kuzidi kumshawishi kuielekea njia sahihi ya wokovu……Na kama mtu yule bado atakuwa hajachukua hatua ya kumkaribisha ndani ya moyo wake kwa kutubu kabisa kwa kumaanisha kuacha dhambi zake na kwenda kubatizwa katika UBATIZO SAHIHI, ataendelea kumshawishi ndani yake mpaka siku atakapokubali..

Sasa siku yule mtu atakapoamua kubatizwa katika ubatizo sahihi, siku ile ile yule Roho Mtakatifu ambaye alikuwa anatembea naye anaingia ndani yake na kuwa milki halali ya Roho Mtakatifu mwenyewe, wanakuwa ni kama wamefunga ndoa na Roho Mtakatifu, kwasababu ubatizo ndio kibali cha Roho Mtakatifu kuingia ndani ya mtu, ni ishara ya dhambi za mtu kuondolewa kwa damu ya Yesu, na ni muhimu sana na ndio maana Bwana aliyaagiza, sasa baada ya hapo ndipo Roho Mtakatifu anakuja kufanya makao ndani ya yule mtu. Biblia inasema Roho Mtakatifu ndio Muhuri wa Mungu, kama unavyojua barua yoyote isiyokuwa na muhuri halisi hiyo ni batili. Roho Mtakatifu ni kama Pete ya ndoa kwa wanandoa.

Waefeso 4: 30 “Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi”.

2Wakorintho 1: 22 “..naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu”. 

Na akishaingia ndani ya yule mtu anaanza kupitishwa madarasa mengine ya kiroho zaidi, na huyo mtu shetani hawezi kumpata tena kwasababu ni kama kashakatiwa leseni mbinguni kuwa milki halali ya Roho mtakatifu.

Je! Ubatizo sahihi ni upi kulingana na biblia?

Ubatizo sahihi kulingana na Neno la Mungu ni ule wa maji mengi na kwa JINA LA BWANA YESU KRISTO, huu ndio ubatizo sahihi tofauti na huu mwingine ni batili.

Sasa kwa undani zaidi kuhusu huu ubatizo sahihi tembelea tovuti yetu ya wingulamashahidi.org uweze kuelewa kwa upana.

Je! Umemwamini Yesu ipasavyo? Umepokea Roho yake? Unafahamu kuwa hizi ni siku za mwisho na parapanda italia muda wowote na watakatifu watanyakuliwa na kisha huu ulimwengu utaharibiwa vibaya.

Amua leo kutubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha kabisa kabisa na kutafuta ubatizo sahihi upokee Roho Mtakatifu, ili uweze kumlaki Bwana Yesu.

Maran atha. (Bwana Yesu anarudi)

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *