ISRAELI NI SAA YA MUNGU

Siku za Mwisho No Comments

ISRAELI NI SAA YA MUNGU

Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe sana, karibu tuyatafakari maandiko, ili tuone jinsi mwisho ulivyokaribu sana kuliko wengi tunavyodhania.

Maandiko yanasema hakuna mtu aijuaye Siku na saa ya kurudi kwa Bwana, hata malaika mbinguni hawajui. Lakini leo nataka nikuonyeshe katika maandiko hayo hayo, kuwa kalenda ya Mungu kuhusu siku za mwisho imewekwa wazi, na saa inajulikana. Hapa sizungumzii saa kama saa, nazungumzia taifa la Israeli kama saa ya Mungu na kalenda ya siku za mwisho.

Ndugu yangu, muda umeisha kweli kweli.. parapanda italia muda wowote? Siku za kuharibiwa kwa huu ulimwengu zimefika!!

Kama wewe ni msomaji mzuri wa biblia utagundua kuwa tangu kipindi cha wana wa Israeli walipokuwa Babeli , Mungu alimfunulia mtumishi wake Danieli muda wa siku zilizobakia mpaka dunia kuisha, ukisoma Danieli 9 utaona kuwa Nabii Danieli aliambiwa muda wa MAJUMA 70 umewekwa kwa watu wake (yaani Waisraeli), mpaka kila kitu kitakapokamilika. Na kumbuka juma moja ni sawa na miaka 7 kibiblia, hivyo ukipiga hesabu utaona jumla yake ni miaka 490 [70×7=490] tu, tangu ule wakati walipotoka Babeli mpaka ulimwengu kuisha.

Lakini ukisoma pale utaona hayo majuma 70 yaligawanywa katika vipindi vitatu, yaani majuma 7 ya kwanza, halafu na majumba 62, kisha juma 1 la mwisho , kukamilisha majuma yote 70. Hatuna muda wa kueleza kwa urefu juu ya migawanyiko hiyo lakini biblia inasema lile juma la 69 litaishia na masihi (YESU KRISTO) kusulibiwa.

Danieli 9: 26 “Na baada ya yale majuma sitini na mawili, MASIHI ATAKATILIWA MBALI, naye atakuwa hana kitu; na watu wa mkuu atakayekuja watauangamiza mji, na patakatifu; na mwisho wake utakuwa pamoja na gharika, na hata mwisho ule vita vitakuwapo; ukiwa umekwisha kukusudiwa.”

Kisha linakuwa limebakia juma moja, ambalo ni sawa na miaka 7 tu ili kila kitu kiwe kimeisha.

Lakini juma hili la mwisho ukichunguza halikuendelea mara baada ya Kristo kusulibiwa, kwasababu kama lingeendelea basi mwisho ulipaswa uwe umeshafika miaka 7 tu mara baada ya kifo cha BWANA YESU, Lakini sasa tunaona imepitia takribani miaka 2000 na mwisho bado haujaja.

Jambo ambalo halikuwahi kuonekana katika unabii wowote katika agano la kale. Jambo ambalo manabii wa Mungu hawakuliona wala kufunuliwa.

Na ndio maana hatupaswi kuacha kushukuru neema ya Kristo, kwasababu wokovu huu tunauona sasa ulipaswa uwe kwa WAYAHUDI tu peke yao watu wa Mungu. Jaribu kutengeneza picha kama mwisho ungefika ule wakati Kristo anaondoka duniani sisi wengine leo hii tungekuwa wapi?

Lakini ashukuruwe Mungu neema ile haikutupita ambayo ililetwa na BWANA YESU KRISTO, ambaye katika ule wakati wa kusulibiwa kwake aliusitisha muda wa WAISRAELI kwanza, usiishe ili atukomboe sisi watu wa mataifa, kwa neema yake, Alituhurumia sisi kwa kulitenga lile juma moja kwanza lililosalia mpaka dunia kuisha, ili hapo katikati atukomboe sisi watu wa mataifa. Na ndio hii miaka 2000 sasahivi tuliyopo ya hii neema. Kwamba kwa kipindi cha miaka takribani 2000 tuingie ndani ya safina sisi watu wa mataifa.

Lakini ndugu fahamu pia hii neema haitadumu milele, tupo ukingoni sana na leo hii tutaona ni jinsi gani ilivyokaribu kuondoka kushinda hata sisi tunavyofikiri, na ikiondoka Mungu anamalizia lile juma 1 moja la mwisho lililobakia (yaani miaka 7) kwa wayahudi WATEULE wake tu!! kisha mwisho wa dunia unawasili.

Ndugu ukilijua hilo hutafanya mchezo na wokovu wako sasa.Mungu aliwapiga upofu makusudi wayahudi(Waisraeli) wasiupokee wokovu tangu wakati ule Kristo kusulibiwa ili sisi tuupate, kwasababu kama wangeupokea wokovu wa KRISTO wakati ule basi dunia ingekuwa imeshakwisha. Mungu aliwajeruhi wayahudi kwa ajili yetu, na ndio maana unaona sasa hivi wengi wao hawamwamini Yesu kama ndiye yule masiya waliokuwa wanamtazamia.. Ni kwasababu gani?, ni kwasababu Mungu alipiga mwenyewe upofu ili tu sisi tuokoke, Mungu aliwatia mwenyewe jeraha sio kwasababu wao walikuwa na dhambi nyingi kushinda sisi hapana, kinyume chake sisi ndio tuliokuwa na dhambi nyingi kuliko wao, lakini Mungu alifanya vile kutuhurumia sisi (yaani mimi na wewe) tufikilie wokovu. Soma kitabu cha Warumi sura ya 11 yote utaona jambo hilo.

Lakini pamoja na hayo tunasoma miaka mingi iliyopita Mungu aliwaahidi kuwarudia watu wake wateule wayahudi, baada ya kipindi fulani mbele, na kuwaimarisha tena. Na Ndio sasa tunasoma katika kitabu cha Hosea, yeye anasema:

HOSEA 6:1 Njoni, tumrudie Bwana; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu. 2 BAADA YA SIKU MBILI ATATUFUFUA; SIKU YA TATU ATATUINUA, NASI TUTAISHI MBELE ZAKE.

3 Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua Bwana; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi.

Umeyaelewa maneno hayo?, Huo unabii unawahusu wayahudi tu! {yaani waisraeli}, Hosea anasema njoni tumrudie Bwana, akiwaambia wayahudi wenzake katika Roho, baada ya SIKU MBILI atatufufua na siku ya tatu atatuinua, nasi tutaishi mbele zake.

Kama ukisoma biblia katika kitabu cha 2Petro 3:8 utafahamu kuwa kwa Mungu SIKU MOJA NI SAWA NA MIAKA 1000, Hivyo hapo utaona kuwa unabii unaweza ukatafsiriwa hivi “Njoni, tumrudie Bwana; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu. baada ya miaka 2000 atatufua na mwaka wa 3000 atatuinua”.

Miaka ya hivi karibuni tutaanza wa 3000, na huo mwaka wa 3000 utakuwa ni milenia ya ule utawala wa miaka 1000 wa Yesu Kristo duniani (Ufunuo 20:4). Sasa kama hapo anavyosema atatufufa, atafunga jeraha zetu na kutuponya, hiyo inamaanisha kuwa huo ndio utakuwa ule wakati wa wayahudi kurudiwa na Mungu wao, kumaliza lile juma moja la mwisho lililokuwa limesalia (yaani miaka 7) ili dunia kuisha. Utakuwa ni wakati wa Israeli kurudishiwa ufalme kama walivyomuuliza Bwana siku ile kabla ya kupaa kwake.

Matendo 1:6 “ Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, JE! BWANA, WAKATI HUU NDIPO UNAPOWARUDISHIA ISRAELI UFALME?

7 Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe.

8 Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.

9 Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, AKAINULIWA, WINGU LIKAMPOKEA KUTOKA MACHONI PAO.”

Ndugu neema ikishalirudia Taifa la Israeli, unyakuo wa kanisa utakuwa umeshapita, kitakachokuwa kimebakia katika mataifa yote ulimwenguni ni MAJUTO NA MAOMBOLEZO, fikiri Bwana ametuhurumia kwa kipindi kirefu hichi chote ili mtu tu yeyote asiangamie lakini bado unaichezea hii neema iliyopo kwa kitambo tu. Bwana aliposema kutakuwa na kilio na kusaga meno, alimaanisha kweli wala hakutudanganya. Miaka 2000 hii inaisha!!

Taifa la Israeli linazidi kunyanyuka siku baada ya siku, tena Bwana akasema “Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hata hayo yote yatakapotimia…mbingu na nchi zitapita lakini maneno yangu hayatapita kamwe”. (Mathayo 24:34), hapo anazungumzia kizazi kilichoshuhudia mtini kuchipuka tena..yaani Taifa la Israeli kupata uhuru wake mwaka 1948 baada ya kukaa miaka mingi bila kuwa taifa huru. Kizazi hicho hakitapita mpaka kurudi kwa Yesu na mwisho wa dunia kufika.!! Na kumbuka kizazi ni miaka 100 tu kwa dunia ya sasa.  Hebu piga tadhimini tangu Israeli kuwa Taifa huru linalojitegemea hadi leo ni miaka mingapi imepita? Bila shaka huu ni mwaka wa 78. Kizazi hicho hakitapita hata hayo yote yatimie, mwenye masikio na asikie.

Ule mwisho umefika, je! Umejiwekaje tayari sasa?. Kwanini bado unaichezea hii neema ya msalaba ambayo sisi hatukistahili kuipata?. Utajibu nini siku ile?. Au utajitetea vipi?.

Waebrania 2: 3 “SISI JE! TUTAPATAJE KUPONA, TUSIPOJALI WOKOVU MKUU NAMNA HII? AMBAO KWANZA ULINENWA NA BWANA, KISHA UKATHIBITIKA KWETU NA WALE WALIOSIKIA;”

Hizi ni saa za majeruhi kama hujakamilishwa katika wokovu fanya bidi sana, utubu, ubatizwe katika ubatizo sahihi wa maji tele na katika Jina la Yesu Kristo, upate ondoleo la dhambi zako, kisha udumu katika ushirika wa Kristo na mafundisho ya biblia angali siku ile inakaribia.

Kwasababu moja ya hizi siku dunia itakuwa imekwisha kabisa. Usikubali kudanganywa na mafundisho ya uongo yanayokufanya uendelee kuupenda ulimwengu na uone kuwa mwisho bado sana. Badilisha leo mtazamo wako, muda umeisha na unyakuo upo karibu sana!! Dalili zote zilizotabiriwa zimekwisha timia.

BWANA YESU ANARUDI 

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *