TUPENI MAFUTA YENU KIDOGO, MAANA TAA ZETU ZINAZIMIKA.

Biblia kwa kina No Comments

TUPENI MAFUTA YENU KIDOGO, MAANA TAA ZETU ZINAZIMIKA.

Jina kuu lipitalo majina yote mbinguni na duniani, jina la YESU KRISTO WA NAZARETHI litukuzwe daima.

Karibu tujifunze habari njema, Neno la Mungu lililo taa na mwanga wa njia zetu.

Leo kwa msaada wa Roho Mtakatifu tutajifunza uhalisia wa mambo yalivyo miongoni mwa wakristo wa leo, Bwana Yesu kabla ya kuondoka kwake hapa duniani, alieleza hali ya kanisa itakavyokuwa karibu na kurudi kwake, akitumia mfano wa wanawali kumi, alielezea makundi mawili ya wakristo watakaotokea siku za mwisho”. Tusome…

Mathayo 25:1 “Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi.

[2]Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara.

[3]Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao;

[4]bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao.

[5]Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi.

[6]Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki.

[7]Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao.

[8]Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika.

[9]Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie.

[10]Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa.

[11]Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie.

[12]Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi.

[13]Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa”.

Kama habari inavyoelezea, kwamba wote walikuwa ni wanawali ikiwa na maana kuwa wote ni wakristo wanaomngojea Bwana. Na yale mafuta waliokuwa nayo wote ni “Roho Mtakatifu”. Lakini wengine walionekana kuwa na mafuta ya ziada, na wengine hawana.

Na ndivyo ilivyo katika nyakati hizi, leo hii kuna kundi kubwa la wakristo wanaorudi nyuma kiimani, hawa ni wale wanawali wapumbavu. Mwanzoni walianza vizuri, waliamini wakatubu dhambi zao, wakabatizwa kwa usahihi na wakapokea Roho Mtakatifu (mafuta), lakini hawakuweza kushikilia ile imani na kudumu katika wokovu mpaka mwisho kwasababu walimzimisha Roho (hawakuwa na mafuta ya kutosha).

Kumbuka sio kwamba hawakuwa na mafuta kabisa, walikuwanayo lakini hayakutosha kuwafikisha mbali, na Bwana arusi alipokuja taa zao zikashindwa kuwaka, ndipo wakawaambia wale wengine ”Tupeni mafuta yenu kidogo, maana taa zetu zinazimika”. Wakajibu sivyo, hayatatutosha sisi na ninyi.

Unaona, wakati wengine wanajaza taa zao vyema, wao waliona hakuna sababu ya kujiangaisha, hakuna sababu ya kugharamika na kujitoa sana. Wakadhani kuwa maadamu tu tumechaguliwa kuwa wanawali na kupewa taa na mafuta kidogo inatosha. Hawakujua kuwa iliwapasa wajiongeze wenyewe wafanye bidii kuongeza mafuta.

Leo hii mtu ameoka kweli na amepokea Roho Mtakatifu lakini hajui kuwa kupokea Roho Mtakatifu hakukutoshi tu kushikilila wakovu, anapaswa azidi kutafuta ujazo wa Roho Mtakatifu kila siku kwa kukaa uweponi mwa Mungu na kuomba. Kwamaana Bwana mwenyewe alisema..

Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni HATAZIDI SANA KUWAPA ROHO MTAKATIFU HAO WAMWOMBAO? (Luka 11:13)

Anasema, HATAZIDI SANA kuwapa, maana yake ni jambo endelevu, la kila siku kadri tuombavyo. Lakini leo hii mkristo anakwepa maombi ya mkesha, maombi ya mfungo, hata yeye mwenyewe hana ratiba yake binafsi ya kuomba hata lisaa limoja kwa siku. Halafu anategemea kukua kiroho, kushinda dhambi, naye anamngojea Bwana Yesu aje amchukue angie katika karamu yake.

Ndugu, usifikiri kuwa wanawali wapumbavu ni wale wakristo jina ambao hata kusikia kuna Roho Mtakatifu ndani yao hawajawahi kusikia, wanawali wapumbavu ni wakristo wa kweli waliopokea Roho Mtakatifu lakini wakazimia njiani kutokana na kupungukiwa na ujazo wa Roho Mtakatifu ndani yao.

Hivyo, huu ni wakati wa kuhakikisha kuwa hatumzimishi Roho Mtakatifu kama biblia inavyotuagiza kuwa “Tuzimzimishe Roho” (1Wathesalonike5:19), wala tusimhuzunishe (Waefeso 4:30).

Kama unataka kwenda katika karamu ya Bwana, Tafuta ujazo wa Roho Mtakatifu kila siku, usikubali kubaki pale pale siku zote, kamwe usiridhike. Fanya bidii Roho Mtakatifu azidi kujaa ndani yako na kuwaka kila siku, usikwepe maombi wala usikubali kupunguza muda wa kuomba (Ombeni bila kukoma). Na maombi yako sana sana yawe ya kujijenga kiroho zaidi ya kuombea mahitaji ya mwilini.

Mathayo 25:11 “Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie.

[12]Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi.

[13]Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa.

Bwana Yesu yupo mlangoni.. unyakuo upo karibu sana muda wowote parapanda italia.

Maran atha. (Na uje Bwana Yesu)

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *