
MAOMBI YA KUTANGAZA
Shalom. Karibu tujifunze somo la Maombi.
Maombi yamegawanyika katika sehemu kuu tatu 1) kushukuru 2) kuwasilisha mahitaji kwa Mungu 3) Kutangaza.
Leo tutajifunza kuhusu Maombi ya KUTANGAZA. Maombi ya kutangaza ni yapi?
Haya ni maombi ya kimamlaka…Maombi haya yanakazi moja tu nayo ni KUTUEPUSHA NA MAJARIBU.
Sasa kabla ya kuingia kujifunza juu ya jambo hili hebu kwanza tujifunze ulinzi wa kiMungu juu ya mtu aliyezaliwa mara ya pili.
Mtu anapozaliwa mara ya pili, na kuishi Maisha yanayompendeza Mungu asilimia zote, kunakuwa kuna ulinzi Fulani wa kiujumla ambao Mungu anauachilia juu yake, kiasi kwamba huyo mtu hata iweje hawezi kupotea, shetani hawezi kumtoa mkononi mwa Mungu, labda tu huyo mtu kwa hiyari yake mwenyewe aamue kujiuza kwa shetani, lakini kwa namna nyingine yoyote hawezi kutoka mikononi mwa Mungu, anakuwa analindwa kuanzia unywele wake mpaka unyayo wako, na anakuwa amevuka kutoka mautini kuingia uzimani, …Lakini pamoja na huo ulinzi wa kiujumla kuna sehemu ndogo sana ambayo Mungu kamwachia shetani aimiliki..na hiyo ni kutokana na kwamba bado tupo katika miili hii ya dhambi, sehemu yote ya ulinzi wa kiMungu tutakuja kuipata baada ya ukombozi wa miili yetu pale tutakapovaa miili mipya ya utukufu.
Ndio maana unaona sasa japokuwa umeokoka na unaishi Maisha ya kumpendeza Mungu kwa asilimia zote lakini bado utapitia wakati mwingine wa viudhaifu vya hapa na pale, utaumwa kichwa, utajisikia kichefuchefu, mafua yatakusumbua, wakati mwingine itakubidi umeze Panadol kupunguza maumivu au uende hospitali n.k. Sasa hiyo yote ni kuonesha kuwa Mungu hajaipa miili yetu hii asilimia 100 ulinzi…ingawa hivi viudhaifu haviwezi kutuathiri kiasi cha kututoa kwenye Imani, kwasababu Mungu hawezi kuruhusu tujaribiwe kupita tuwezavyo, alisema hivyo katika Neno lake.
1Wakoritho 10: 13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili”.
Kwahiyo haya majaribu madogo madogo ni lazima yaje! Na ni wazi kuwa yanaletwa na shetani kututesa tu! Na kutuhangaisha…Kwahiyo shetani anachokifanya ni kutumia hii nafasi aliyopewa ya sehemu ndogo ambayo Mungu kaiacha, kutujaribu…Na kwasababu anajua hawezi kumjaribu mwamini kwa asilimia zote, atahakikisha kuwa hiyo sehemu ndogo aliyopewa anaitumia ipasavyo.
Sasa swali? Anaitumiaje?
Anaitumia kwa KUTANGAZA, Anawatumia watu kutamka maneno Fulani Fulani juu yako, ambayo hayo yanaweza kutokea kama walivyozungumza, kwasababu Mungu alivyomuumba mwanadamu akizungumza kitu kwa Imani ni lazima kitokee hata kama mtu huyo sio mchawi. Ndio maana wazazi hata kama ni waabudu sanamu wanao uwezo wa kumbariki mtoto au kumlaani, na hizo baraka au laana zikampata huyo mtoto hivyo hivyo kama alivyozisema. Kwasababu hiyo basi shetani anaweza kutumia watu au wachawi au mapepo yake KUTANGAZA mambo Fulani mabaya juu ya mtu.
Kumbuka tena kwa msisitizo..kama umezaliwa mara ya pili na kuishi Maisha yampendezayo, haijalishi ni mambo gani makubwa watayatangaza juu yako, hayatatimia yote kwasababu kuna asilimia kubwa ya ulinzi wa kiMungu kwenye Maisha yako, lakini pia yapo baadhi madogo madogo yanayoweza kutimia na hiyo ni kwasababu hatujapewa dhamana wa ulinzi wa miili hii asilimia zote kama tulivyotangulia kusema..(huu ni msingi mkubwa ambao unahitaji kuelewa) Na sio kwamba Mungu kashindwa kutufunika asilimia zote, hapana ni kwasababu tu ndivyo imempendeza iwe hivyo…kwamba tujue kwamba bado tupo duniani?, tujue kuwa sisi bado ni wadhaifu mbele zake, na tujifunze kumtegemea yeye na kumwomba ulinzi…na pia tujue kuwa vita bado vinaendelea…mpaka siku tutakapovaa ile ya utukufu, ndipo vita vitaisha.
Sasa ili kupunguza nguvu za shetani kwa majaribu yake anayoyatumia kwa NJIA YA KUTANGAZA…Na sisi tulioamini tuna wajibu huo huo, wa kuingia kwenye maombi ya kuzipunguza hizo nguvu ndogo ndogo za shetani zinazofanya kazi kwenye Maisha yetu…Na maombi hayo hatuyafanyi kwa kupeleka mahitaji mbele za Mungu, bali kwa KUTANGAZA kama yeye anavyotangaza..Ndio hapo sasa Kila siku kabla ya kuianza siku unatamka baraka katika siku hiyo, unalaani na kufuta kila kazi zote za Adui zilizopangwa katika siku hiyo kwa jina la YESU, Unalaani vidhiki na vijaribu vidogo vidogo vilivyopangwa na shetani…Na unatamka kwa maneno yanayosikika kabisa, kwasababu maneno yanaumba, kwa Mungu aliiumba dunia kwa Neno, Unatamka kwa kutangaza kuziharibu nguvu zote na kufuta maneno yote yaliyozungumzwa na watu, wachawi, au mapepo katika siku nzima…unalaani nguvu zote za giza zilizoachiwa siku hiyo zitakazokufanya uikane Imani, au upate hasara ya jambo Fulani, au zitakazokufanya ulumbane au ugombane na watu, unalaani kwa kinywa chako kila nguvu zote za giza zilizoachiwa na yule adui kukufanya usipate muda wa kusoma Neno,na kila ratiba isiyoeleweka iliyopangwa kuzimu kinyume chako na ndugu zako…Unahikikisha unagusa kila kipengele katika Maisha yako, afya yako,familia yako, kazi yako na Imani yako. Usiache kitu!, kwasababu na yule adui anajua anaomlango mdogo juu ya Maisha yako hivyo anakaza kuutumia vizuri.
Mithali 18:21 “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.”
Kwa kufanya hivyo utakuwa umeharibu mipango yote midogo midogo ambayo shetani alikuwa amepanga kukusumbua katika siku hiyo na wiki hiyo. Na hivyo utakuwa umejiongezea Ulinzi wa kiMungu kwa asilimia nyingine kadhaa mbele. Kama alikuwa akuletee viugomvi, viugonjwa, unashangaa siku inaisha bila hivyo vitu, kama alikuwa amekusudia kukuletea vitabu vya hapa na pale visivyoeleweka vinatoweka.
Kwa hiyo ni maombi ya Muhimu sana na kila Mwamini anatakiwa aombe. Na ni moja ya silaha 6 tulizopewa katika biblia..(Waefeso 6:18)
Kwa kumalizia kumbuka kuwa muda wa chini Bwana Yesu aliotuamuru tusali kwa siku ni LISAA LIMOJA.
Mathayo 26: 40 “Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? 41 Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.”
Umeona hapo, roho zetu zipo tayari kuomba lakini miili ndio inayokataa, hivyo mambo mengine ni unalazimisha, kama Bwana asiyekuwa na dhambi aliomba Zaidi ya lisaa limoja, unafikiri inatupasaje sisi wenye dhambi?..unakataa usingizi na uvivu wa kuomba, unalazimisha mambo, utashangaa dakika za kwanza unapata shinda lakini baaada ya dakika 10-15 mbeleni unashangaa kuna nguvu Fulani inakuvaa unajikuta unazama kwenye maombi…Na kwa vipengele hivyo vitatu ukianza na kushukuru, kisha kupeleka maombi na kutangaza baraka..huwezi kuacha kumaliza lisaa na Zaidi..
Lakini ikiwa bado upo nje ya Kristo, hautaweza kutangaza jambo lolote, bali wachawi, mapepo na mashetani ndiyo watakutangazia mambo mabaya tu siku zote katika maisha yako na yatakupata. Lakini kama leo upo tayari kumkaribisha Bwana Yesu katika Maisha yako, basi uamuzi unaoufanya ni sahihi..hautakuja kujutia kamwe.
Fahamu kuwa tunaishi ukingoni mwa nyakati na Yesu Kristo yupo mlangoni…wakati wowote parapanda italia.
Mwenye masikio na asike.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.