WENYEJI WETU UKO MBINGUNI.

Biblia kwa kina No Comments

WENYEJI WETU UKO MBINGUNI.

Shalom mtu wa Mungu, Karibu tujifunze Neno la Mungu ambalo hilo ndilo linalotufanya tuishi mpaka sasa hivi mimi na wewe.

Wafilipi 3:20 “Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo;

[21]atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake”.

Je! u mwenyeji wa mbinguni? Biblia inatufundisha kuwa sisi wenyeji wetu uko mbinguni, hapa duniani tupo kama wageni, wasafiri.

Unajua tunasoma habari ya Ibrahimu ambaye tunamwita Baba wa Imani, kutokana na Imani tunayoiona aliyokuwa nayo kwa Mungu wake..licha ya kukaa kwa muda mrefu bila kupata mwana Mungu aliyekuwa amemuahidia akizingatia na huku umri umeshakwenda yeye na mke wake, hakukata tamaa kumwamini Mungu badala yake aliendelea kusubiria mpaka Mungu alipotimiza alichomuahidia na hata alipopata mwana, zaidi ya yote tunasoma katika uzee ule Mungu alimjaribu tena amtoe mwanawe kuwa sadaka ya kuteketezwa, Nalo hilo Ibrahimu halikumtikisa bali alidhubutu kumtoa, ndipo Mungu akavutiwa sana na Imani ya Ibrahimu..

Lakini hilo pekee tu pekee lingetosha Mungu kumfanya Ibrahimu kuwa baba wa imani na mtu wa kuigwa kwa vizazi vyote? Watu watakaokuja kumwamini yeye baadaye?..Lipo jambo lingine la ndani zaidi tunapaswa tulijue ambalo ndilo tutaligusia siku ya leo.

Tukisoma kitabu cha Waebrania tunapata kuona tabia nyingine tofauti ambayo Ibrahimu aliionyesha kwa Mungu wake. Tunasoma:

Waebrani 11:8 “Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako.

9 KWA IMANI ALIKAA UGENINI KATIKA ILE NCHI YA AHADI, KAMA KATIKA NCHI ISIYO YAKE, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.

10 Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu”

Sasa ukiyachunguza hayo maandiko kwa makini utaona kuwa Ibrahimu alikuwa na jicho lingine la mbele zaidi hata ya lile alilokuwa ameahidiwa na Mungu katika mwili..Na ndio maana siku zake zote maisha yake yote hakusumbuliwa na mambo yanayopita, hukusumbuliwa na kukawia kwake kupata mtoto,hakusumbuliwa na hata kutoa mwanawe Isaka kuwa sadaka kwa Mungu wake…

Embu Soma tena hapo anasema. 9 KWA IMANI ALIKAA UGENINI KATIKA ILE NCHI YA AHADI, KAMA KATIKA NCHI ISIYO YAKE,..Kumbuka Mungu alimtoa Ibrahimu nchi ya mbali sana huko Uru ya Ulkadayo na kumleta Kaanani, mahali ambapo Mungu alimwahidia kumpa kila kitu ambacho ni chema, alimwahidia kuwa atamfanya kuwa taifa kubwa sana, atamfanya kuwa uzao hodari, uzao ambao utamiliki malango yote ya adui zake wote..Atamfanya kuwa taifa tajiri, na lenye nguvu sana..

Sasa embu jaribu kutengeneza picha ingekuwa hiyo nafasi umepewa wewe, Mungu anakuambia utakuwa na uzao hodari katika nchi fulani na kwa kupitia wewe mataifa yote duniani yatabarikiwa, hivi utajisikiaje?…Ni wazi kuwa utajiona kuwa ni mtu wa kipekee mbele za Mungu kuliko wengine wote, utatanua mbawa kidogo, utajiona kuwa wewe ni mtu muhimu sana mbele za Mungu kuliko wengine..Hata ukifika katika hiyo nchi Mungu aliyokuahidia utaimiliki pengine kwa kiburi fulani, utaishi kama mfalme fulani au chief fulani hivi kwani Mungu tayari ameshakuridhia na kukupa wewe..hata watu wote wa huo mji wakitaka kupigana na wewe hutaogopa, kwasababu Mungu alishakupa wewe milki hiyo.

Lakini kwa Ibrahimu haikuwa hivyo, alikuwa na jicho la mbali zaidi, hakutazama Baraka hizo Mungu alizomwahidia za kitambo tu, hakutazama wingi wa uzao atakaokuwa nao duniani, hakutazama ukuu wa taifa atakalolizaa duniani, hakutazama utajiri wa kimwilini, kwa hili jicho la kimwilini, bali aliyatafakari maisha yake kwa utulivu sana, akiangalia jinsi Mungu alivyomtoa Nchi ya Ulkadayo na kumleta pale Kaanani, na jinsi Mungu alivyomwepusha katika taabu zote zile, za kungojea nchi ambayo Mungu amemwahidia, akajiuliza kama Mungu anao uwezo wa kunifanya taifa kubwa ndani ya dakika moja, kwanini anakawia hivi kunipa mwana? Sababu nini?..Ibrahimu alitaka kujua kusudi la maisha, nyuma ya haya yote kuna nini?.. Na ndipo akafahamu kuwa maisha yake ni picha ya mambo yatarajiwayo mbeleni yajayo baada ya ulimwengu huu kupita. Alifahamu kuwa maisha yake ni somo, maisha yake ni sauti Mungu anayozungumza naye juu ya mambo ya mbeleni sana..ng’ambo ya pazia..

Na ndio maana tunasoma Ibrahimu licha ya kupewa utajiri wote ule wa kimwilini, bado aliendelea kuishi katika nchi ile ambayo ni kweli ilikuwa ni haki yake kustarehe na kujifurahisha lakini biblia inatuambia aliishi mule kama vile siyo nchi yake, aliishi katika milki yake kama vile sio milki yake, kama vile mgeni nyumbani kwake mwenyewe..aliisha na mke wake Sara kwenye mahema, fikiria Ibrahimu alikuwa ni mtu tajiri sana mwenye mali nyingi alizopewa na Mungu lakini hakuishi kwenye makasri,..hiyo inafunua nini?..Inaonyesha ni jinsi alivyoishi kama mpitaji hapa duniani?.

Unadhani alikuwa hajipendi?. Hapana..Biblia inatuambia ni kwasababu alikuwa anautazama mji ulio bora, alikuwa anautazamia mji wenye misingi, sio ule wa Kaanani aliopewa ambao Mungu kweli alimpa kuwa milki yake, lakini huo ingempasa aweke misingi yeye iliyodhaifu, ingempasa aubuni yeye..Lakini badala yake Ibrahimu hakufanya hivyo bali aliutazamia mji wenye misingi ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu mwenyewe.. Na mji huo si mwingine zaidi ya YERUSALEMU MPYA ya mbinguni HALELUYA!!..

Jambo hilo ndilo lililomfanya Mungu apendezwe na Ibrahimu na kumfanya awe kielelezo cha kuigwa kwa watu wote, ikiwemo mimi na wewe.

Sasa huyo ni Ibrahimu, lakini mashujaa wa imani na watakatifu wote katika biblia waliishi hapa duniani kama wasafiri na wageni, kwani walitambua kuwa hao si wa ulimwengu huu, bali wenyeji wao uko mbinguni na si hapa duniani haijalishi walitajirishwa na Mungu kiasi gani

Waebrania 11:13 “Hawa wote wakafa katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa WAGENI, NA WASAFIRI JUU YA NCHI.

[14]Maana hao wasemao maneno kama hayo waonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe.

[15]Na kama wangaliikumbuka nchi ile waliyotoka, wangalipata nafasi ya kurejea.

[16]Lakini sasa waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao; maana amewatengenezea mji”.

Yohana 15:18 “Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi.

[19]Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia.

Tujiulize je mimi na wewe wenyeji wetu uko wapi? Huwenda tukasema kwa vivywa vyetu sisi ni wa mbinguni, kumbe kwa mioyo yetu sisi ni wa ulimwengu huu…na ishara inayotutambulisha kuwa sisi ni wa ulimwengu huu ni kupendwa na ulimwengu kwasababu ulimwengu unawapenda walio wake. Na watu wa ulimwengu huu mwisho wao ni uharibifu.

Je! unaishi maisha ya kutazama mbinguni, au mambo tu ya duniani?.

Je! umeoshwa dhambi zako, na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi, kama Neno lenyewe “ubatizo” linavyomaanisha, na kwa jina la YESU KRISTO?. na ikiwa umefanya hivyo vyote je! maisha yako yanauhakisi utakatifu? (Waebrania 12:14), maana biblia inasema hakuna mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao huo.

Ikiwa hayo hayapo ndani yako.. angalia bado unao muda mfupi wa kutengeneza maisha yako na Mungu leo, fanya bidii uingie katika orodha ya wasafirio kabla mlango wa neema haujafungwa. Ulimwengu huu na mali zisiwe kisingizio siku ile. Kwasababu wapo waliokuwa na mali zaidi yangu na yako na waliokuwa na mafanikio kupita ya Ibrahimu lakini waliishi kama wapitaji tu hapa dunia.

Isaya 35: 8 “Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; WASAFIRIO, WAJAPOKUWA WAJINGA, HAWATAPOTEA KATIKA NJIA HIYO.

Ni matumaini yangu utatubu leo na Bwana akujalie kuishi katika utakatifu na usafi.

Ubarikiwe sana.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *