WAKATI WA BWANA KATIKA MAISHA YAKO.
Shalom mtumishi wa Bwana karibu tuyatafakari maneno ya uzima ya mwokozi wetu Yesu Kristo.
Wakati wa Bwana ndio uliobeba maswali ya majibu yako,ndio uliobeba kustawi kwako katika maeneo yote unayotamani kustawi katika maisha yako ikiwa ni mambo ya kimaisha nk. ile picha unayoiona katika ufahamu wako namna unavyojiona ndani yako (picha inayokuja katika ufahamu wako japokua haijadhihirika bado nk) nataka nikwambie hayo si Mawazo ya kawaida au yanayokuja na kupita ukiona kuna picha Fulani inakuja ndani yako na unatamani kufikia katika eneo hilo hicho kitu ni kweli kabisa wala sio uongo.
Lakini ili kiweze kutimilika hicho kitu/hiyo picha imefungwa ndani ya “ Wakati wa Bwana ” na inahitaji wakati huo uweze kufika ili hicho kitu kitimilike lakini ukisema ulazimishe utatumia nguvu kubwa sana na bado hakitawezekana kabisa.
Sasa wakati wa Bwana ni muhimu sana kuungoja watu wengi wamejikuta wakiingia katika msongo wa Mawazo, kukata tamaa nk kwa sababu ya kushindwa kutambua jambo kama hili, jambo ambalo unapaswa kulifahamu “ haijalishi Mungu kakuonyesha kitu kikubwa kiasi gani amekuonyesha wewe utakuwa mtu wa namna gani na atakutumia kwa namna kubwa sana hapo mbele tambua kuna majira ya hicho kitu wala sio siku hiyo hiyo au baada ya mwezi au mwaka.”
Watu wengi wamekufa pasipo kujua kwa nini kwa sababu walionyeshwa mambo makuu yaani hatima zao wakashindwa kukaa katika utulivu wakajikuta wanaingia kupambana kuhakikisha hatima zao zinatimia na wakajikuta wanaangamia kwa kushindwa kusubiria wakati wa Mungu ambao ni sahihi kwa wao kuweza kufikia katika hatima zao.
Unaweza ukawa hujanielewa vizuri lakini ikiwa unataka kuwa salama basi endelea kusoma kwa makini kwa kadili Roho Mtakatifu atakavyoniongoza basi atakufunulia siri kuu sana juu ya hili jambo kama alivyonifunulia mimi.
Sasa naomba tumtafakari mtu mmoja anaitwa MUSA kwa kadili Bwana atakavyozidi kutupa neema basi tutaangalia na wengine wengi katika maandiko.
1.MUSA .
Hatima ya Musa ilikua ni kuwakomboa wana wa Israeli kutoka utumwani Misri, na moto ulikua unawake sana ndani yake kuwaokoa wana wa Israeli kuwatoa utumwani ni kweli lilikua ni kusudi ambalo Musa alitakiwa kulifanya na alizaliwa kwa ajili ya kutimiza kusudi hilo “ kila mmoja ameumbwa kutimiza kusudi Fulani maalumu la Mungu hapa duniani.”
Lakini Musa alitaka kufanya hicho kitu nje na wakati wa Mungu ambao Mungu mwenyewe alikua ameukusudia na hii ingeweza kuleta madhara kwa Musa hata angeliuwawa na farao kwa sababu alitaka kufanya jambo hilo nje kabisa na wakati ambao Mungu alikuwa ameukusudia kwa Musa kuwatoa wana wa Israeli. Alitaka kutumia njia zake yeye mwenyewe na akili zake kuwatoa wana wa Israeli utumwani.
Kutoka 2:11-2 “Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo wa ndugu zake.
[12] Basi akatazama huko na huko, na alipoona ya kuwa hapana mtu, akampiga Mmisri yule, akamficha ndani ya mchanga.”
Musa alimuua Mmisiri kwa lengo la kuwasaidia ndugu zake ambao walikua wanatumikishwa kazi ngumu ndani yake alisikia kuumia kweli mpaka kufikia hatua ya kumuua yule Mmisiri yule unaweza ukaona uchungu aliokua nao Musa juu ya ndugu zake.
Maandiko yanasema siku inayofata yaani ya pili akataka kuwaamua ndugu zake juu ya mgogoro uliokua Katikati yao na hivi ndio maandiko yanasema…
Kutoka 2:13-14 “Akatoka siku ya pili, na tazama, watu wawili wa Waebrania walikuwa wakipigana. Akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake, Mbona unampiga mwenzako?
14 Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana.”
Unaona hapo? Kitu alichojibu? Anasema “Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu na mwamuzi juu yetu?” Haleluya sijui kama kuna kitu umekiona hapo ukiangalia Musa alikuja kuwa mkuu juu yao wana wa Israeli na mwamuzi juu yao pia. lakini nataka uone kitu kimoja hapo kwa wakati ambao Musa alitaka kuwa mkuu na mwamuzi juu ya wana wa Israeli haukuwa ni wakati sahihi ambao Bwana ameukusudia na nini basi kilichotokea baada ya jambo hilo??
Kutoka 2:15 “Basi Farao alipopata habari, AKATAKA KUMWUA MUSA ; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima.”
Unaona hapo? Farao alitaka kumwua Musa tafakari vipi kama Musa asingelikimbia au angelikamatwa? Maana yake angeliuawawa na Farao maana yake angekufa kabla ya kusudi lake halijatimia, la kuwaokoa wana wa Israeli.
Na hiyo ikapelekea kukimbilia Midiani ndio kukawa salama na bado hakufanikiwa kuwatoa wana wa Israeli utumwani.
Roho Mtakatifu anataka tujifunze nini hapa? Haijalishi ndani yako kuna wito mkubwa sana wa kumtumikia Mungu, unahisi moto unawaka ndani yako kutaka kutumikia Mungu kama wakati wa Mungu haujafika kukifanya hicho kitu tulia, haijalishi Mungu amekuonyesha utakua mfanya biashara mkubwa sana na idea nyingi za biashara zinakuja ikiwa wakati wa Bwana haujafika tulia haijalishi una hiyo pesa bank ya kuanzisha biashara tulia. Usianze kuhangaika namna ya kufanya kwani hapo utajikuta unaingia mpaka kwenye biashara zisizo faa. Huenda huna kabisa mtaji na Mungu kakuonyesha utakua mfanya biashara mkubwa utafanya biashara kimataifa lakini ukiangalia huna chochote, huna kazi nk,
Mungu huenda kasema na wewe atakupa mke alie sahihi ambaye atakusaidia kubeba maono yako yatimie au wewe mwanamke Bwana kasema na wewe atakupa mume mzuri kwa ajili ya kulitimiza kusudi lake usiaze kuwa mwepesi kwa mwanaume au mwanamke yeyote unaemdhania tulia.
Watu wengi wanashindwa kufika kule Mungu alikowakusudia kwa sababu ya kushindwa kusubiria wakati wa Mungu, wakati wake ukifika na huwa umebeba yote na zaidi ya yale unayoyahitaji.
Katika somo linalofata tutajifuza namna gani ya kuungoja wakati wa Bwana na dalili zitakazokuonyesha unatumia jitihada zako wala hauko kwenye wakati sahihi wa Mungu, tutaona pia nini unapaswa kufanya nk
Usikose sehemu ya pili.
@Nuru ya upendo
Mawasiliano:0613079530
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.