TABIA YA ROHO MTAKATIFU KWA MWAMINI MPYA.

Biblia kwa kina No Comments

TABIA YA ROHO MTAKATIFU KWA MWAMINI MPYA.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo lisifiwe daima, Ni siku nyingine tena Bwana aliyotupa kwa neema zake na leo tutaangalia tabia za Roho Mtakatifu katika kumtakasa mwamini katika hatua za kwanza. Kumbuka mwamini ni mtu aliyemwamini Bwana Yesu na kuamua kumfuata kweli kweli. (Kwa ufupi mtu aliyezaliwa mara ya pili).

Zipo tabia sita (6) za Roho Mtakatifu katika kumuongoza mwamini.. lakini leo tutaangalia tabia moja tu nayo ni tabia ya upepo.

Kama tunavyofahamu tabia ya upepo, kwanza ni kitu kisichoweza kuonekana kwa macho lakini utaisikia sauti yake pale unapovuma, au utauhisi katika mwili wako pale unapopita karibu na wewe, lakini usijue chanzo chake ni wapi na hatma ya safari yake itaishia wapi!!.

Kadhalika Roho Mtakatifu anapoingia ndani ya mwamini tabia hizi za upepo wa Roho huingia ndani yake. Pale mtu alipoamua na kudhamiria kweli kumpa Kristo maisha yake. Basi kuanzia huo wakati na kuendelea ndani yake kunakuwa na nguvu isiyojulikana chanzo chake ni nini kwa nje!

Watu wa nje wanaweza kushangaa mbona huyu mtu tabia yake imebadilika kwa ghafla hivi,wasijue ni nani aliyembadilisha, wakijaribu kachunguza labda ni dini hawaoni, labda ni dhehebu hawaoni, labda ni mwanadamu hawaoni, na ndio hapo utaona maisha ya yule mtu yanabadilika, pengine mambo aliyokuwa anapenda kuyafanya hapo mwanzo yanageuzwa ghafla, maisha aliyokuwa anaishi nyuma yanageuka ghafla, mara nyingine atajikuta anachukia hata kufanya baadhi ya vitu alivyokuwa anavifanya nyuma, anajikuta kiini cha maisha yake ni kumwangalia Bwana YESU tu mahali popote alipo…Baadhi ya mambo yasiyokuwa na maana yataanza kumkera, anaanza kutokujiona kuwa huru akiwa katika vikao vya usengenyaji, tofauti na alivyokuwa hapo mwanzo..

Hii yote inatokea ni kwasababu yule Roho aliye ndani yake humsukuma kufanya vitu ambavyo hata pengine yeye mwenyewe hajui ni kwanini anavifanya, saa nyingine anaweza akadhani ni kwa akili zake anafanya hivyo.Au ni kwasababu ametokea tu kupenda mwenyewe Lakini ukweli ni kwamba sio yeye anafanya hivyo bali ni Roho wa Mungu ndani yake atembeaye kama upepo usioonekana anamwelekeza asikojua yeye.

Atajikuta anaanza kuchukia kupenda pombe, ambapo hapo mwanzo alikuwa anazitamani, anajikuta kuvaa vimini na suruali anajiona kama yupo uchi au anajiaibisha mbele za watu hivyo anajikuta anaanza kupenda kuvaa sketi ndefu ambazo hapo mwanzo alikuwa akivaa anajiona kama mshamba. Anajikuta anatamani kusoma biblia, au kusikiliza Neno la Mungu sana, ambapo hapo kwanza alikuwa hana mpango navyo. Anajikuta kampani za marafiki wa kidunia ni mzigo mkubwa kwake tofauti na jinsi alivyokuwa nyuma. Anajikuta hata akipitia dhiki kubwa kiasi gani kwa ajili ya imani hapepesuki mpaka watu wa nje! Wanashangaa huyu mtu ni wa dizaini gani. N.k.

Na hata baada ya muda mrefu kupita ukimuuliza ilikuwaje kuwaje ukaweza kuacha dhambi na mambo ya kidunia pamoja na majaribu mazito kiasi kile atakwambia kwa kweli sifahamu nguvu hiyo ilitoka wapi,nilijikuta tu ninamsimamo na maamuzi yangu..nilijikuta tu kuna nguvu fulani ndani yangu ikinisukuma kunipeleka sehemu Fulani,sasa huo ulikuwa ni ule upepo wa Roho ambao ulikuwa unampeleka asikotazamia yeye kwenda,.ataishia kukwambia ni neema za Mungu tu.

Bwana Yesu alipomuhubiria Nikodemo habari za kuzaliwa mara ya pili kwa Roho Mtakatifu, Nekodemu alistaajabia sana na kusema inawezekanikaje mtu kuzaliwa mara ya pili lakini Bwana Yesu akamwambia maneno haya:

Yohana 3:7 “Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili.

8 Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho’’.

Hata siku ile ya Pentekoste Roho Mtakatifu alishuka kwa wale watu kama upepo unaovuma kwa kasi.

Matendo 2:1 “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.

2 KUKAJA GHAFULA TOKA MBINGUNI UVUMI KAMA UVUMI WA UPEPO WA NGUVU UKIENDA KASI, UKAIJAZA NYUMBA YOTE WALIYOKUWA WAMEKETI. 

3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.

4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka”.

Unaona umuhimu wa kuzaliwa kwa Roho? Leo hii ni kwasababu gani huwezi kushinda tamaa, na dhambi, ni kwasababu moja tu, nayo ni hii HAUJAZALIWA MARA YA PILI hivyo ule upepo wa Roho hauwezi ukawa na nguvu juu ya maisha yako. Haujamkaribisha Roho ndani ya maisha yako. Kama ungekuwa umezaliwa kwa Roho ile nguvu ingekusukuma mahali usipojua kama vile UPEPO uvumapo na usingeona kuwa dhambi ni jambo gumu kuliacha kwasababu ni Roho mwenyewe angekuwa anatenda kazi ndani yako.. Nguvu ile Ingekusukuma kule usikoweza kufika, ingekusukuma kutenda mapenzi ya Mungu na kumtazama Kristo kila wakati.

Kumbuka Nikodemo alikuwa ni Farisayo wa mtu dini sana, anayejua maandiko sana lakini hakuwa amezaliwa mara ya pili, unaona? kumbe unaweza ukawa wa kidini na usiwe na Roho Mtakatifu ndani yako. Ndugu Usiridhike na dhehebu lako, au kanisa lako ukajiona kuwa tayari umekamilika na huku unaona kabisa maisha yako ya kikristo yanadorora siku baada ya siku..Na ndio maana maandiko yanasema, MTU ASIPOZALIWA KWA MAJI NA KWA ROHO HAWEZI KUUINGIA UFALME WA MBINGUNI hapo hata kama uwe unayafahamu maandiko kiasi gani, huwezi kuuingia ufalme wa mbinguni, Bwana Yesu anasema hivyo.

Lakini Mtu anazaliwaje kwa Roho na kwa Maji?

Ni kwa kukudhamiria kabisa kutubu na kuacha dhambi na maisha ya kale.Wengi hawafanyi hivyo, toba haitoki moyoni bali midomoni na ndio maana inakuwa ngumu Roho wa Mungu kukaa ndani yao. Na maana ya toba sio kuomba msamaha tu, bali ni KUGEUKA AU KUACHA. Hivyo unapogeuka na kukusudia kuacha dhambi hata usiposema kwa mdomo hiyo tayari ni TOBA, na baada ya hapo unatafuta ubatizo wa maji mengi na kwa JINA LA BWANA YESU, Hivyo ukizingatia hayo na Mungu akishaona nia yako yeye mwenyewe atakuosha “roho yako”, kwa maji (ambayo ni DAMU yake na Neno lake) na kukugawia Roho wake ndani yako atakayekuweza kukusaidia kuishinda dhambi siku zote za maisha uliyopo hapa duniani.

Kumbuka tunaishi ukingoni mwa nyakati, parapanda italia muda wowote na watakatifu watanyakuliwa!!

Bwana Yesu akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *