FAHAMU KWA UNDANI KUHUSU JINA LA YESU

Biblia kwa kina No Comments

FAHAMU KWA UNDANI KUHUSU JINA LA YESU

Nakusalimu katika jina kuu lipitalo majina yote mbinguni na duniani JINA LA YESU KRISTO, karibu tujifunze elimu ya ufalme wa Mungu.

Unajua kati ya kitu chenye nguvu kwa mtu ukiacha DAMU ni JINA, mtu mwenye Jina kubwa atakuwa na nguvu nyingi za kiutawala na heshima kuliko mwingine, jina la Mfalme ni tofauti na jina la mtu wa kawaida, na mtu akitaka kushushwa anachafuliwa kwanza jina.

Sasa ili tuweze kuelelewa vizuri mamlaka/nguvu ya jina la YESU, kwanza tujue asili ya hili jina limetoka wapi, Jina hili tofauti na wengi tunavyojua kuwa ni jina la mtu mmoja anayeitwa Yesu.. hili sio jina la mtu kama ilivyo majina mengine kwamba kila mtu ana jina lake la kumtofautisha yeye na mwenzake. Jina la Yesu sio jina ambalo alipewa huyu mwana wa Mungu kumtofautisha yeye na watu wengine. Hili ni jina ambalo limetoka katika koo za kimbinguni, ni jina ambalo linarithishwa kizazi baada ya kizazi kwa wana wa Mungu. Ni jina la ukoo wa Mungu kama vile wewe unaweza ukaitwa kwa jina la ukoo wako badala ya jina lako.

Mbinguni kuna majina mengi… lakini jina la Yesu ni kuu sana, limepita majina yote. Likitajwa tu..malaika wote wanataharuki nini kinaendelea. Ndio maana kuzimu wanaliogopa sana hili jina kuliko kitu kingine… maana ni jina kuu sana, kama tu hapa duniani kuna koo/familia zenye majina ya kuogopwa na kuheshimiwa, si zaidi jina la Yesu ambalo linaogopwa na kuheshimiwa sana kule juu mbinguni.

Lakini jambo lingine tunapaswa kufahamu kuhusu hili jina, ni kwamba jina hili ni la kurithishwa.

Waebrania 1:1-4 ”Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi,

[2]mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.

[3]Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;

[4]AMEFANYIKA BORA KUPITA MALAIKA, KWA KADIRI JINA ALILOLIRITHI LILIVYO TUKUFU KULIKO LAO.”

Umeona hapo anasema “AMEFANYIKA BORA KUPITA MALAIKA, KWA KADIRI JINA ALILOLIRITHI LILIVYO TUKUFU KULIKO LAO.” Zingatia hilo neno ”kuliko lao” maana yake kulikuwa na majina mengine lakini Jina la Yesu lilikuwa juu ya kila jina walilonalo malaika wote. Jina la Yesu Ni jina la Urithi, watoto wote wa Mungu (waliozaliwa mara ya pili) wanalirihi hili jina. Jina la Yesu ndio jina la kimamlaka ambalo Bwana Yesu alilipokea kutoka kwa BABA, na kisha baadaye Baba akaturithisha na sisi tulio watoto wake, Ndio maana jina la Yesu linajulikana kama jina la BABA, na la MWANA na la Roho Mtakatifu..Kwasababu kalipokea kutoka kwa baba yake, ndipo likawa lake, na kisha likawa letu kwa kupitia Roho Mtakatifu.

Yohana 17: 11 “Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, KWA JINA LAKO ULILONIPA UWALINDE HAWA, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. 12 Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda KWA JINA LAKO ULILONIPA, NIKAWATUNZA; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie”

Yohana 17: 6 “JINA LAKO nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu; walikuwa wako, ukanipa mimi, na neno lako wamelishika”.

Yohana 17: 25 “Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua; lakini mimi nalikujua, na hao wamejua ya kuwa ndiwe uliyenituma 26 NAMI NALIWAJULISHA JINA LAKO, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao”.

Umeona! Jina la Yesu lilivyo?..lilitoka kwa Baba, likaja kwa Mwana, na sasa lipo kwetu katika Roho Mtakatifu, tumepewa sisi, watu wa Taifa lake,ndio maana kila tunaposali ile sala ya Baba yetu, hatuachi kusema “Jina lako litukuzwe (Mathayo 6:9)”..Ni kwasababu gani?..Ni kwasababu hakuna jina lingine TULILOPEWA WANADAMU LITUPASALO KUOKOLEWA KWALO, isipokuwa JINA LA YESU (Matendo 4:12). Jina la Yesu ni la kwetu sisi tuliomwamini. Jina la Yesu sio tu la kutolea mapepo kama wengi wetu tunavyodhani, kutoa mapepo na kushindana na wachawi ni elimu ndogo sana ya kulitumia Jina la Yesu. Jina la Yesu ni jina la URITHI.

Ni jina ambalo huyu Mwana wa Mungu ambaye kupitia yeye nasi tunapokea uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu (Yohana1:12) alikirimiwa na Baba kwa jinsi alivyostahili.

Wafilipi 2:5 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;

6 ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;

7 bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;

8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. 

9 KWA HIYO TENA MUNGU ALIMWADHIMISHA MNO, AKAMKIRIMIA JINA LILE LIPITALO KILA JINA;

10 ILI KWA JINA LA YESU KILA GOTI LIPIGWE, LA VITU VYA MBINGUNI, NA VYA DUNIANI, NAVYA CHINI YA NCHI;

11 na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba”

Unaona hapo, Yesu Kristo alikirimiwa jina hilo lipitalo kila jina, na hivyo yeyote atakayemwamini naye ataingizwa katika ukoo wa Yesu na hivyo naye atarithishwa jina hili.

Leo ukijua siri ya jina la Yesu na mamlaka ya hili jina.. nakuambia hutakaa umuogope mchawi yeyote, au pepo lolote… zaidi ya yote utafahamu kuwa umebarikiwa sana kwani hili jina limebeba baraka na neema tele, hautajichukulia tena wa kawaida.Kumbuka wana wa Mungu wote tumerithishwa hili jina, kwahiyo katika roho tunatambulikana kwa jina la Yesu..hii ni siri ambayo unapaswa kuijua kuanzia sasa.

Sasa utajuaje kama wewe ni mmoja wa warithi wa jina hilo, au utajuaje kuwa umepewa mamlaka ya kulitumia jina hilo?. Jibu lipo kwenye biblia.

Matendo 2: 36 “Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo.

37 Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38 PETRO AKAWAAMBIA, TUBUNI MKABATIZWE KILA MMOJA KWA JINA LAKE YESU KRISTO, MPATE ONDOLEO LA DHAMBI ZENU, NANYI MTAPOKEA KIPAWA CHA ROHO MTAKATIFU.

39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”.

Umeona hapo, ukitaka uingie katika Taifa la Mungu watu wa Yesu, unachotakiwa kufanya NI KUTUBU KWANZA kwa kudhamiria kuacha dhambi zako na maisha yako ya nyuma yasiyompendeza Mungu, na kumbuka maana ya kutubu sio kuomba tu msamaha bali ni kugeuka au kuacha kile ulichokuwa unakifanya kisichokuwa sahihi, na baada ya kutubu kwa kumaanisha kabisa, na kwa kutokushurutishwa na mtu, hatua inayofuata ni kubadilishwa jina lako kwa KUBATIZWA KWA HILO JINA…Zingatia hilo!! KWA HILO JINA LA YESU, na sio kwa vyeo vyake hapana bali kwa jina la Yesu, kama maandiko yanavyosema hapo juu! Na kama yanavyosema katika sehemu nyingine katika biblia (matendo 8:16, matendo 10:48, na Matendo 19:5).

Shetani anachokifanya sasahivi ni kuwapofusha watu macho wasione umuhimu wa kubatizwa ubatizo sahihi, anatuma majeshi mengi ya mapepo wabaya yenye ushawishi mkubwa, kwa kusudi la kuwapumbaza watu wasione umuhimu wa ubatizo sahihi, waone ni sawa kwenda kujitosa tu baharini ufukweni kuogolea kwenye maji mengi au kwenye ma-swimming pool hata masaa 7 au 8 na kufurahi lakini wasione sawa kuingia kwenye maji hayo hayo mara moja tu! Kubatizwa kwa jina la Yesu Kristo. Jambo hilo shetani atahakikisha analipiga vita kweli kweli, kwasababu anajua endapo mtu huyo akifanya hivyo atakuwa ameshampoteza moja kwa moja, atakuwa ameingizwa kwenye ukuhani wa kifalme.

Ndugu unayesoma ujumbe huu, Dada/kaka maandiko hayo uliyoyasoma hapo juu! Hayajatoka katika kitabu cha dini fulani wala dhehebu fulani, bali yametoka katika kitabu chako biblia yako. Uamuzi ni wako juu ya hatima ya maisha yako. Kuchagua njia ya uzima au ya Mauti. Kuudharau msalaba au kuuheshimu,Lakini natumaini utaichagua njia ya Uzima.

Mungu akubariki sana.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *