ZAMANI ZILE ZA UJINGA MUNGU ALIJIFANYA KAMA HAZIONI 

Biblia kwa kina No Comments

ZAMANI ZILE ZA UJINGA MUNGU ALIJIFANYA KAMA HAZIONI 

Matendo ya Mitume 17:30 “Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu.

[31]Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu”.

Zamani za ujinga ni zipi? Ni wakati kabla ya Kristo kuja duniani, wakati huo watu walikuwa wanafanya mambo fulani fulani wakidhani ya kwamba Mungu anapendezwa navyo, kumbe mambo hayo yalikuwa yanamchukiza Mungu. Mfano utaona zamani zile kabla ya agano jipya kuoa mke zaidi ya mmoja ni sawa, kulipisa kisasi ni sawa, kutoa talaka ni sawa tu, lakini pia uzinzi ulikuwa unajulikana kuwa ni ule wa kulala tu na mtu, Lakini Yesu Kristo alipokuja akatoa huo ujinga akasema…

Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini;

[28] LAKINI MIMI NAWAAMBIA, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.”(Mathayo 5:27-28)

Akasema tena..

“Imenenwa pia, Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka;

[32] LAKINI MIMI NAWAAMBIA, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini.

[33]Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiape uongo, ila mtimizie Bwana nyapo zako;

[34] LAKINI MIMI NAWAAMBIA, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu;

[35]wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu.

[36]Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi.

[37]Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.

[38]Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino;

[39]Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili.

[43]Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;

[44] LAKINI MIMI NAWAAMBIA, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,

[45]ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.”

Mathayo 5:17 “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, BALI KUTIMILIZA.

Umeona hapo, sasa hivi tupo katika agano bora kuliko lile la kwanza, hatupaswi tena kuendelea kuwa wajinga kwasababu zamani zile Mungu alijifanya kama hazioni maovu yetu.

Lakini pia mbali na hayo, zamani zile watu walikuwa wanaabudu sanamu, wanatoa sadaka kwa miungu, wanashirikiana na mashetani pasipo wao kujua kupitia mila, sheria za kifamilia, n.k lakini kwa rehema za Mungu hatukuangamia. Lakini sasa Mungu anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu (watubie matendo yao ya giza).

Ndugu/kaka huwenda ulikuwa umeoa mke zaidi ya mmoja lakini ulifanya hivyo kwa kutokujua, sasa umejua kuwa ndoa ya kiMungu ni mke mmoja na mume mmoja baki na mke wako wa kwanza na mfunge ndoa ya Kikristo, lakini pia ulitoa talaka pasipo zababu za msingi zinazotambulika kibiblia (uasherati), mrudie mke wako leo..

Halikadhalika ulikuwa unafuata mila na desturi zenu…mnashiriki matambiko, vyakula vilivyotolewa sadaka kwa miungu, mnaabudu miti, jiwe na mambo mengi tu yaliyofungamana na ibada ya miungu, basi leo umeujua ukweli tubu na mrejee Mungu wa kweli.

Dada ulikuwa unajipamba kwa mapambo ya nje (nywele bandia/wigi, kucha bandia, vikuku, bangili, hereni, mekap, lipsticks, n.k) pengine hukuwa unajua lakini leo tubu na ondoa hayo mapambo yote kabatini na mwilini mwako tupa chooni wala usimpe mtu mwingine kwasababu ni machukizo kwa Mungu (1Petro3:3), halikadhalika ulikuwa unavaa suruali, vimini, nguo za kubana lakini biblia inasema..

Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa MAVAZI YA KUJISTIRI, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;

[10]bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu”.(1Timotheo 2:9)

Leo fahamu kuwa suruali yoyote kwa mwanamke sio vazi la kujistiri, hilo ni vazi la kiume tu na ni machukizo kuvaa mavazi yasiyopasa jinsia yako kasome “Kumbukumbu la torati 22:5”. Hivyo choma suruali zote bila kujalisha ulinunua kwa gharama kiasi gani, choma nguo zote sisizostiri mwili wako kwasababu uzinzi wa siku hizi sio tu ule wa kukutana moja kwa moja, lakini hata kwa kutamani unazini moyoni mwako, sasa jiulize ni watu wangapi wamezini na wewe kupitia mavazi yako?

Kijana ulikuwa unanyoa denge, unacheza kamari, unabashiri/unabeti, unacheza magemu, unasikiliza miziki za kidunia, na mambo yote ya kidunia yasiyompendeza Mungu, tubu leo na mgeukie Bwana Yesu kwasababu ulikuwa unayafanya hayo pengine kwa kutokujua.

Ulikuwa unaabudu sanamu ya Maria ukijua labda unamheshimu Mungu!, lakini kusujudia sanamu yoyote iwe ni ya Mungu mwenyewe ni chukizo kubwa.

Kutoka 20:4-5 Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.

[5]Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,

Kwahiyo ndugu, unayesoma ujumbe huu ambaye bado upo nyuma ya wakati (Yaani Kristo yupo mbali na wewe), na unafanya dhambi za makusudi au pengine sio za makusudi bali kwa kutokujua…basi leo jinyenyekeze kwa Mungu, maanisha kutubu toba ya kweli na Mungu atakupokea na kukutengeneza.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Maran atha.(Bwana Yesu anarudi)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *