Ficha watoto wako ndani ya safina
Safina ni nini?
Ni chombo cha majini kilichotumika mahususi kwa ukombozi. Ni mfano wa meli iliyotumika kuokoa watu/wanyama kutoka katika maangamizi fulani. Kwamfano katika biblia tunaona Nuhu aliagizwa atengeneze safina, ambayo ataingia yeye pamoja na familia yake, na wanyama wa nchi.
Lakini pia wakati Musa anazaliwa, tunaona wazazi wake walimtengenezea naye kisafina kidogo, akafichwa ndani yake, ili kunusuriwa na maangamizi ya Farao.
Kutoka 2:1 Mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaondoka akaoa binti mmoja wa Lawi.
2 Yule mwanamke akachukua mimba akazaa mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu.
3 NA ALIPOKUWA HAWEZI KUMFICHA TENA, AKAMPATIA KISAFINA cha manyasi akakipaka sifa na lami, akamtia mtoto ndani yake, akakiweka katika majani kando ya mto.
Sasa wewe kama mzazi/mlezi huna budi kumweka mtoto wako ndani ya safina ili anusurike na machafu ya dunia hii.
Tunafahamu kabisa kuwa dunia tunayoishi sasa..imeharibika kwa kiwango kikubwa, mambo mengi maovu yanatendeka wazi wazi, hivyo usipowaficha watoto wako mahali salama (ndani ya safina) fahamu kuwa hauna watoto… maana ni lazima tu waangamizwe na adui (ibilisi).
Sasa safina inamwakilisha nani?
Ni Yesu Kristo, yeye ndiye mwokozi wa ulimwengu, na ndiye safina yetu ambayo tukiingia ndani yake tunanusurika na mabaya ya kila namna.
Hivyo mahali pekee ambapo watoto wako wanakua salama na kuwa na ulinzi muda wowote ni ndani ya Yesu Kristo, hivyo wewe kama mzazi au mlezi huna budi kuwaficha watoto wako ndani ya Yesu Kristo mwokozi wetu.
Na utawafichaje? Ni kwa kufanya yafuatayo..
1. Kuwafundisha biblia.
Wafundishe watoto wako kujua biblia mapema, wafundishe kukariri vifungu vya biblia, hata kama hataelewa sasahivi lakini vitabaki moyoni mwake kama hazina itakayokuja kumsaidia baadaye. Na hakikisha pia unampelekea kwenye mafundisho ya watoto kanisani.
2 Kuwaombea
Hakikisha unawaombea watoto wako mara kwa mara, unatenga muda mrefu wa kuwaombea, na kuwafundisha pia kusali kila wakati huku mwenyewe ukiwa mfano.
3 Mzuie kufanya/kutazama mambo ambayo hayapasi.
Si lazima kila unachokitazama wewe, mtoto naye akitazame, magemu anayoyacheza mtoto si yote yanamaudhui mazuri, vilevile nguo unazomvisha mtoto si zote ni njema. Hivyo jifunze kumchagulia mtoto vinavyomfaa.
4 Tumia kiboko
Kuna wazazi au walezi wengine wanaogopa na wengine hawataki kabisa kuwaadhibu watoto wao, kwa kisingizio eti tunaishi kazazi kipya kile ni cha zamani kimeshapita, watoto wa siku hizi hawapigwi wanaelekezwa tu…Huo ni uongo wa shetani, ndio inafikia hatua mpaka mtoto anamtukana mtu mzima na mzazi anamwangalia tu, anaiba na mzazi anamwangalia tu, akidhani kuwa akimwadhibu mwanaye atajisikia vibaya au atapata matatizo fulani ya kiafya,..Au ataona kama haonyeshi upendo kwa familia yake..Hivyo anaepuka kabisa kumudhi mwanae.. Lakini biblia inasema..
Mithali 22: 15 “Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto; Lakini fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali”.
Na pia inasema …
Mithali 23: 13 “Usimnyime mtoto wako mapigo; MAANA UKIMPIGA KWA FIMBO HATAKUFA.
14 Utampiga kwa fimbo, NA KUMWOKOA NAFSI YAKE NA KUZIMU”. .
Unaona hapo siku ile wazazi wengi watawajibika kujibu ni kwanini watoto wao wapo kuzimu, angali wasingepaswa kuwepo huko. Tunasema watoto wa siku hizi wamebadilika, lakini ki-ukweli wazazi wa siku hizi ndio waliobadiliaka, watoto ni wale wale.
Hivyo kwa kufanya hivyo utakuwa umemficha mtoto wako ndani ya safina na atakuwa salama siku zote.
Kumbuka hizi ni siku za mwisho, hivyo kama mzazi hujaokoka fahamu ghadhabu ya Mungu imekaribia na pasipo kuingia ndani ya safina wewe na watoto wako mtaangamia katika ile siku ya hasira ya Mungu ambayo ipo karibu.
Luka 21:22 Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa.
23 Ole wao wenye mimba na wanaonyonyesha katika siku hizo! Kwa kuwa kutakuwa na shida nyingi katika nchi, na hasira juu ya taifa hili.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.