MAKANISA SABA NA BIBI ARUSI WA KRISTO

Siku za Mwisho No Comments

MAKANISA SABA NA BIBI ARUSI WA KRISTO

Jina la Bwana Yesu mkuu wa uzima libarikiwe milele na milele.

Karibu tujifunze habari njema.

Lakini kabla hatujaendelea mbele zaidi, nikuulize swali hili ndugu yangu, Je wewe ni bibi arusi wa Kristo?

Nafahamu bila shaka utajibu ndiyo, lakini je unafahamu bibi arusi safi wa Kristo anatakiwa aweje?

Huu ni wakati wa kupigania kwa bidii kuwa bibi arusi wa Kristo kwelikweli, kwasababu kama ukifa leo hii na sio bibi-arusi au unyakuo umekukuta na bado hujafanyika kuwa bibi arusi ujue kuwa unyakuo hautakuhusu hata kidogo, haijalishi utasema mimi ni mkristo wa miaka mingi, hutakwenda popote. kumbuka si wakristo wote ni bibi-arusi, jambo ambalo wengi wetu hatulijui, Wakati huu wa mwisho maandiko yanatuonyesha wazi kuwa kutakuwa na makundi makuu mawili ya watu wanaojiita wakristo. Wanawali warevu na wanawali wapumbavu kasome Mathayo 25.

Sasa ili tumfahamu vyema bibi arusi safi wa Kristo katika nyakati hizi za mwisho, ni vizuri kwanza ufahamu kuwa kanisa la Kristo limekuwa likipitia vipindi saba tofauti tofauti tangu kanisa la kwanza la mitume..na vipindi hivyo ndivyo vinajulikana kama NYAKATI SABA ZA KANISA, na sasa tupo katika nyakati ya kanisa la saba ambalo linajulikana kama LAUDIKIA na ni kanisa la mwisho kulingana na unabii wa biblia. (Kama utahitaji kufahamu kwa undani zaidi tutumie ujumbe inbox tutakutumia somo hilo)

Ukisoma kitabu cha Ufunuo 2 & 3 utaona yale makanisa saba ambazo zinafunua nyakati saba za kanisa.

Sasa kanisa la Kristo ambalo ndiyo bibi arusi ni moja, ila limekuwa likionyesha tabia fulani fulani kwa kila nyakati, kwa mfano katika nyakati hii tunayoishi, tabia ya kanisa hili ni kanisa ambalo ni vuguvugu, sio baridi wala sio moto.. na hapo sasa ndipo tunapata wakristo wa aina mbili, wale ambao wapo katika kundi la wanawali warevu (bibi arusi safi wa Kristo) na wale ambao wapo katika kundi la wale wanawali wapumbavu ambao ndio wanajulikana kama Masuria.

Tukirudi katika Agano la kale, tunamsoma Musa ambaye anafananishwa na Bwana Yesu, kipindi anamkimbia Farao, alikimbilia katika nchi ile ya Midiani na huko akakutana na Yethroni kuhani wa Midiani aliyekuwa na mabinti saba, ambapo kati ya hao saba ndiko alikuja kumpata Sipora akawa mkewe, sasa huyu Sipora anamfunua bibi arusi wa Kristo na wale mabinti wengine wanafunua wale wanawali wapumbavu/Masuria.

Kutoka 2:15 Basi Farao alipopata habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima.

[16]Basi kuhani wa Midiani alikuwa na BINTI SABA, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza birika maji, wapate kunywesha kundi la baba yao.

[17]Wachungaji wakaja wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia, akalinywesha kundi lao.

[18]Walipofika kwa Reueli baba yao, akasema, Imekuwaje hata mkarejea mapema leo?

[19]Wakasema, Mmisri mmoja alituokoa katika mikono ya wachungaji, tena zaidi ya hayo, akatutekea maji, akalinywesha kundi.

[20]Akawaambia binti zake, Yuko wapi basi? Mbona mmemwacha mtu huyo? Mwiteni, ale chakula.

[21]Musa akawa radhi kukaa kwake mtu yule, NAYE AKAMPA MUSA BINTI YAKE, SIPORA.

Sasa tukirudi katika kitabu cha Ufunuo, habari hiyo inafunua pia yale makanisa saba ndio hao mabinti saba, ambao kati yao mmoja ni bibi arusi safi wa Kristo.

Ili tuelewe tena vizuri, tusome unabii wa Isaya 4.

Isaya 4:1 Na siku hiyo WANAWAKE SABA watamshika mtu mume mmoja wakisema, Tutakula chakula chetu, na kuvaa nguo zetu wenyewe, lakini tuitwe tu kwa jina lako; utuondolee aibu yetu.

[2] SIKU HIYO CHIPUKIZI LA BWANA LITAKUWA ZURI, lenye utukufu, na matunda ya nchi yatakuwa mema sana, na kupendeza, kwa ajili ya Waisraeli wale waliookoka.

Kama tunavyojua mwanamke kibiblia anawakikisha kanisa ndio maana anaitwa bibi arusi (2Wakorintho 11:2 & Ufunuo 19:7), kwahiyo hao wanawake saba ni makanisa saba katika vipindi saba vya kanisa kama inavyoonekana katika ufunuo 2 & 3.

Na huyo mtu mume mmoja ni Yesu Kristo,.Lakini hao wanawake wote 7 wanasema watakula chakula chao wenyewe na kuvaa nguo zao wenyewe bali waitwe tu kwa jina la yule mtu mume mmoja ambaye ni Yesu Kristo.Jambo hili la kusema tutakula chakula chetu na kuvaa nguo zetu wenyewe ni tabia za hayo makanisa yote 7 yalivyokuwa, kila kanisa lilikuwa na tabia yake pekee, na yote yanatafuta kumpendeza Yesu Kristo lakini kwa njia zao wenyewe,

kwahiyo hicho “chakula” kinachozungumziwa hapo ni mapenzi yao wenyewe, na mienendo yao wenyewe hawataki chakula cha Bwana wao,(ambalo ni neno la Kristo lisiloghoshiwa), wala hawataki “mavazi” ya Bwana wao (Ambao ni utakatifu na matendo mema soma ufunuo 19:8,) bali waitwe tu kwa Jina la Bwana Yesu aibu yao iwaondoke hii aibu ina maana waiepuke hukumu itakayokuja na ndio maana yale makanisa yote hayakuweza kuoana na Kristo kikamilifu yalikuwa na mapungufu yake, na sisi pia tupo katika kanisa la mwisho la saba la LAODIKIA ni kanisa vuguvugu,na ndilo lililomkinai Bwana wake kuliko mengine yote yaliyotangulia soma Ufunuo 3:14-22.

Lakini tunapaswa wote tushinde ili tuvuke kutoka kuwa masuria na kuwa bibi-arusi safi wa Yesu Kristo waliokubaliwa tayari kwenda kwenye arusi ya mwanakondoo itakayofanyika mbinguni kwa Baba. Kumbuka bibi-arusi sio sawa na suria.

Kwahiyo ndugu watakaoshiri karamu ya mwanakondoo ni bibi-arusi tu, je! wewe ni bibiarusi? umepokea Roho Mtakatifu? umejiweka tayari kumpokea Bwana wako atakaporudi? matendo yako yanastahili wokovu? jibu lipo moyoni mwako. Tubu sasa umgeukie Bwana kumbuka tunaishi kizazi ambacho kitashuhudia kuja kwa pili kwa Kristo.

Ufunuo 19: 7 Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari.

8 Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu.

Shalom: ubarikiwe.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *