ILE SAFINA IKAELEA JUU YA USO WA MAJI.
Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe.
Karibu tujifunze maneno ya uzima.
Je! Umewahi kutafakari ni kwanini ile safina ya Nuhu ambayo ilikuwa imebeba wanyama mbali mbali haikuzama japokuwa walikuwepo wanyama wazito kama tembo, twiga, ngamia n.k, ?
Maandiko yanasema ile safina ikaelea juu ya uso wa maji. Tusome…
Mwanzo 7:17 Ile gharika ilikuwako juu ya nchi siku arobaini; nayo maji yakazidi, yakaieleza safina, ikaelea juu ya nchi. 18 Maji yakapata nguvu, yakazidi sana juu ya nchi; na ile safina ikaelea juu ya uso wa maji.
Kwanini safina haikuzama?
Jibu ni kwamba maji yalizidi uzito wa ile safina, ile safina ikawa kitu chepesi juu ya yale maji hivyo haikuweza kuzama, kwani tunajua kwa kawaida kitu chepesi kinaelea kwenye maji kulingana na ujazo wa maji.
Ila mbali na huo ukweli kwamba hiyo safina haikuzama kwasababu ya maji kujaa juu ya nchi na kuifanya safina ielee juu yake, lipo pia jambo la kiroho ambalo nataka leo tutazame kuhusu habari hiyo.
Tunaposoma biblia hasa matukio yaliyotokea nyuma hatuishii tu kusoma kupata kumbukumbu au kujua tu basi, hatuishii tu kufurahia kusoma matukio yanayosisimua, bali tunatakiwa tutafakari kwa undani zaidi ujumbe ambao hilo tukio limebeba kwa wakati wetu, na hapo ndipo Roho Mtakatifu anatufinulia siri zilizojificha ndani yake.
Sasa tukirudi kwenye hiyo habari ya safina kuelea juu ya maji, kabla hatujafahamu siri ya hiyo safina kuelea juu ya maji pasipo kuzama, (kumbuka tumeshaona kwa namna ya kawaida sababu yenyewe) ila hapa tunatazama kwa jicho lingine la kiroho ili tujifunze somo hapo.
Kuna vitu vitatu nataka tutazame hapo kwamba zinawakilisha nini kwa namna ya rohoni.
Kwanza hiyo safina, na wanyama walioko ndani yake, na hayo maji.
Kama tunavyojua ile safina ilikuwa inamwakilisha Bwana Yesu yeye ndiye safina yetu kwa sasa ambao sisi kama wanyama (kondoo wake) tunapata usalama ndani yake. Na yale maji biblia imetoa tafsiri yake katika Ufunuo 17.
Ufunuo 17:15 Kisha akaniambia, Yale maji uliyoyaona, hapo aketipo yule kahaba, ni jamaa na makutano na mataifa na lugha.
Umeona hapo, yale maji yanawakilisha mkusanyiko wa watu wengi au ulimwengu wote kwa ujumla.
Sasa kwanini safina haikuzama?
Jibu ni lile lile, kwamba uzito wake haikuwa kitu juu ya yale maji, ilikuwa nyepesi kama vile karatasi juu ya maji.
Ni nini tunajifunza hapo?
Kama tulivyoona huu ulimwengu unafanamishwa na yale maji ya gharika, na Yesu Kristo ndiye safina yetu ikielea juu yake. Siku zote fahamu kuwa ukiwa ndani ya Yesu huwezi kuzama wala kugharikishwa na chochote..iwe ni gharika ya wachawi, mapepo, magonjwa au hatari yeyote. Yesu Kristo hawezi kuzama, sasa wewe utazamaje ukiwa ndani yake?
Kuna wakati fulani Yesu aliwatokea wanafunzi wake akitembea juu ya maji, mwanafunzi wake mmoja Petro akataka kumfuata ila akiwa anatembea juu ya maji akaona hofu akata kuzama ila Yesu akamshika mkono akatembea naye juu ya maji.
Mathayo 14:23 Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake.
24 Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho.
25 Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari.
26 Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu.
27 Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope.
28 Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji.
29 Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu.
30 Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe.
31 Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika…”
Ukiwa ndani ya Yesu usione hofu kabisa, haijalishi utaona upepo wa aina yeyote, haijalishi mawimbi yatakupiga, Yesu yupo na wewe akushike mkono pale ambapo utataka kuzama..we mwamini tu na kumtegemea.
Kumbuka tupo kwenye ulimwengu ambao umeharibika na ulimwengu huu unafananishwa na maji hivyo kama utakuwa nje ya safina (Yesu Kristo) uwe na uhakika kuwa utazama muda wowote, huko nje hakuna usalama kabisa ni lazima tu utachukuliwa na gharika na upepo na wawimbi ya kila namna.
Hii dunia imeshahukimiwa na imewekwa akiba kuangamizwa kwa moto na sio gharika ya maji tena soma 2Petro3:6-7.
Hivyo kama bado upo nje ya safina (Yesu Kristo) huu ndio wakati wako wa kuingia ndani kabla mlango haujafungwa.
Fahamu kuwa muda wowote utaenda kufungwa na kama vile watu wa siku za Nuhu walihubiriwa na Nuhu waingie ndani ya safina kabla ya gharika, lakini wakaipuizia ile injili na mwisho mlango ulifungwa, baadaye ndio wakaja kutaka kuingia wasiweze maana tayari walishachelewa, mlango ulifungwa siku saba nyuma kabla hata ya gharika. Na wote wakaangamia (Mwanzo 6), na Yesu alisema kuja kwake itakuwa kama siku za Nuhu, ni wachache tu watakaokolewa kama tu ilivyo kuwa kipindi cha Nuhu ni watu nane tu, hivyo Bwana anasema..
Luka 13:24 Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.
25 Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako;
28 Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno,. “
Je umeingia ndani ya safina, umempokea Yesu kwa kumaanisha kweli kweli au bado unaishi maisha ya uvuguuvugu, bado unaendelea kuipuuzia injili inayokufikia kila siku.
Mpe Yesu maisha yako leo uokoke na ghadhabu ya Mungu ambayo ipo karibu.
Unajua maana ya kumpa Yesu maisha yako, sio kusema nimemwamini na nampenda, au naendaga kanisani kila siku, ni kweli unaweza ukawa unafanya hayo yote ila bado hujampa Yesu maisha yako.
Kumpa Yesu maisha yako tafsiri yake ni kwamba kuanzia huo wakati maisha yako yanakuwa milki ya Yesu, na maisha ni uhai wako pamoja na vitu vyote unavyovitegemea kuishi, unavikabidhi kwa Yesu. Kwa mfano kazi yako, biashara yako, elimu yako, familia yako, nafsi yako.. maisha yako yote unayoyaishi ikiwemo ulaji wako, uvaaji wako, faraha yako, viungo vyako na mwili wako kwa ujumla unampa Yesu akuongoze na akutawale, yeye ndiye akuambie ule nini, uvae nini, uende wapi na usiende wapi, utazame nini na usitazame nini, ufanye nini na usifanye nini, uzungumze nini na usizungumze nini, n.k, hiyo ndiyo tafsiri ya kumpa Yesu maisha yako.
Kwa ufupi maisha yako yote yanaongozwa na Yesu kupitia Roho wake Mtakatifu, kiasi kwamba watu wakikuona wanamwona Yesu, ukizungumza watu wanasema we ni mkristo.
Je umempa Yesu maisha yako? Au bado unaye yule Yesu wa kidini, kama maisha yako hayaendani na Neno la Mungu, tabia zako na mwenendo wako ni wakidunia, uvaaji wako ni wa kidunia, mazungumzo yako ni ya kidunia na bado unasema umeokoka fahamu kuwa bado hujampa Yesu maisha yako na uko hatarini kuzama na kupotea kabisa kwenye hii dunia iliyoharibika.
Ghadhabu ya Mungu ipo juu yako, ukiishi nje ya Yesu ni sawa na chuma kuelea juu ya maji, kitazama tu. Ukiwa na Yesu wa kidini utakuwa tu na hofu ya maisha, wachawi watakusumbua, utakuwa makao ya kila roho chafu, ndoto za kipepo zitakusumbua tu, na utabaki tu kutumikishwa na adui, kwasababu haujampa Yesu maisha yako.
Muda wowote utakuwa hatarini kuzama maana haupo ndani ya safina, hicho chombo unachotumainia, haitakusaidia kitu, ijapokuwa utasema unaye Yesu ndani ya chombo chako ila kama hujamweka moyoni mwako bali umemweka tu kwenye mahitaji yako fahamu kuwa huyo yesu hatakusaidia, utabakia tu kutaabika kwenye huu ulimwengu, utapelekwa huku na huku, utachukuliwa na upepo wa kila namna, utapata tu hofu kwasababu haujamweka Yesu kwenye moyo wako bali umembeba tu kama kisaidizi akusaidie njiani.
Ndicho kilichowatokoea wale wanafunzi wakati fulani wakiwa njiani wanaenda kwenye safari yao walimchukua Yesu wakambeba kwenye chombo chao, na njiani wakakumbana na dhoruba kali wakiwa wanavuka bahari.
Kwasababu hawakuwa na imani na Yesu walifadhaika sana wakaona wanaenda kuzama ndipo wakamwamsha na kumwambia tusaidie tunaangamia.
Marko 4:35 Siku ile kulipokuwa jioni, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo.
[36]Wakauacha mkutano, WAKAMCHUKUA VILE VILE ALIVYO KATIKA CHOMBO. NA VYOMBO VINGINE VILIKUWAKO PAMOJA NAYE.
[37]Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji.
[38]Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?
[39]Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu.
[40]Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?
[41]Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?
Jiulize ile chombo ingewezaje kuzama ilihali Yesu mkuu wa uzima yupo ndani? Ni kwasababu walikuwa na Yesu wa kidini, hawakuamini kama dhoruba ingetulia tu yenyewe pasipo Yesu kuamka na kukemea.
Mpe Yesu maisha yako..achana na ukristo jina, toka kwenye ulimwengu ulioharibika ingia ndani ya Yesu ambaye ndiye safina yetu. Fahamu kuwa hizi ni siku za mwisho na muda wowote mlango wa neema utafungwa,
Weka kando mizigo yako ya dhambi ili uwe mwepesi ndani ya ulimwengu huu unaofananishwa na maji, kumbuka ukiwa mzito utazama na kupotea.
Waebrania 12:1 Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, NA TUWEKE KANDO KILA MZIGO MZITO, NA DHAMBI ILE ITUZINGAYO KWA UPESI; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu,
[2]tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.