Mtu akiipenda dunia kumpenda Baba hakumo ndani yake.

Biblia kwa kina No Comments

Mtu akiipenda dunia kumpenda Baba hakumo ndani yake.

Nakusalimu katika jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo karibu tuyatafakari maneno ya uzima.

 

Tofauti na inavyodhaniwa na watu wengi kuwa mstari huu unawazungumzia Watu ambao hawajaokoka, la! Mstari huu ni mahususi kabisa na kwa watu ambao tayari wameshamwamini Yesu Kristo.

Walaka huu unamhusu Mkristo yeyote ulimwenguni ni walaka ambao umebeba maonyo tahadhari juu ya manabii wa uongo na namna tunavyotakiwa kutembea kama waamini.

1 Yohana 2:15“Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.”

Maandiko yanasema “….mtu akiipenda dunia kumpenda Baba hakumo ndani yake

Wakati mwingine labda umewahi kusikia au kufikiri kwamba kuupenda ulimwengu labda nikuangalia mipira,kuvaa nusu uchi au kusuka kidunia, kuweka lipstick nk kwamba ndio kuupenda ulimwengu,  ndugu sivyo hayo yote ni matokeo ya kuupenda ulimwengu,  mtu anapoupenda ulimwengu hayo ndio matokeo yake.

Lakini hasa tutaangalia kwa kina maandiko yanaposema kuupenda ulimwengu hasa maana yake ni nini?.

1.Tamaa ya mwili.

Maandiko yanaposema tamaa ya mwili si moja kwa moja ni uzinzi au uasherati,  ndio haya mambo yote ni matokeo ya tamaa ya mwili. Na hapa tamaa hasa inayozungumziwa ni tamaa ya muda mfupi.

Tamaa ya mwili ni nini?Ni tamaa ya kutaka kujiridhisha mwenyewe kwa muda mfupi tu baada ya hapo unakuwa kwa muda huo hutaki tena.

Kati ya mambo hayo ni Hasira, Kutafuta utukufu wa kibinadamu/kufanya jambo lolote zuri kwa lengo la kusifiwa au kutukuzwa, uasherati, kusema uongo ili kutafuta sifa au utukufu fulani nk.

Hizi ni njia za watu wa mataifa ambao wao hutimiza tamaa zao kwa muda mfupi. Kwako wewe Mkristo zina madhara makubwa sana katika ukuaji wako wa kiroho.

Jambo hili lilimkuta Musa wakati alipokuwa Misri na hakuchukuliana nalo mwandishi anasema hivyo wa kitabu cha Waebrania.

Waebrania 11  Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao;

25  akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo;

Unaona hapo kwenye mstari wa 25 anasema “…….Kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo;”

Musa aliliona hili angejifurahisha katika kiti cha ufarao Misri na watu wangempenda sana lakini mwisho angekufa na angeenda kuzimu na tusingekuwa na mtu anaitwa Musa kwenye biblia na kama mfano wa kuigwa.

Hivyo ndugu yangu kataa kutimiza tamaa za mwili ambazo ni za kitambo tu. Soma Wagalatia 5:18-21 hayo yote ni matendo ya mwili.

2.Tamaa ya macho.

Tamaa ya macho hapa hamanishi kuangalia miziki ya kidunia,tamthilia,picha za uchi. Ndio haya yote ni matokeo ya tamaa ya macho na ni dhambi na mwisho mauti. Lakini maana halisi ni nini pale maandiko yanaposema tamaa ya macho?.

Tamaa ya macho ni mvuto,ushawishi au majaribu ya kitu/vitu fulani vinavyopendeza kwa nje. Lakini mwisho wa siku huleta madhara au kumtoa mtu katika njia sahihi.

Hivyo ni mvuto au ushaawishi juu ya Anasa,utajiri(si kitu kibaya utajiri lakini kama Mkristo unataka utajiri kwa matakwa yako mwenyewe(watu wakuone nk) ndugu utaangamia ni kitu kinaonekana vizuri tu na ndio maana maandiko yanasema “..kufanikiwa kwa mpumbavu kutamuangamiza”)  umarufu,fasheni au mitindo ya kidunia. Vyote hivi ni vitu ambavyo havina thamani ya milele bali ni vya muda mfupi.

Hivyo tamaa ya macho ni hali ambapo mtu anashawishika na kuvutiwa na maisha ya kidunia, kwa kufikiri ataridhika kupata mambo ya ulimwengu huu kama mavazi,pesa,starehe na kutukuzwa na watu lakini kumbe ndani ni mtu ambae anapotea kiroho. 

Sisemi mavazi,pesa, ni mambo ya kidunia la! Lakini mfumo wa kidunia unapoanza kuufata utaangamia.

Na ndio maana Leo hii wanawake wengi wa Kikristo wanashindana mavazi makanisani,misuko nk sio kwamba ni vibaya wanapovaa mavazi la! Lakini nia na kusudi si kwa ajili ya Mungu bali kwa ajili ya watu wanapowatazama wavutiwe nao na watu wawatukuze.

Epuka tamaa ya macho inaamsha mashindano na chuki na wivu na inaharibu kanisa la Kristo.

3.kiburi cha uzima.

Kiburi cha uzima hamaanishi pumzi tuliyonayo hii la! Lakini hapa anazungumzia kuwaza sana,kutamani sana kupita kiasi, na kupigania/kupambana kwa nguvu kubwa ili kuonekana kuwa mtu wa maana zaidi mbele za watu kiasi kwamba hilo linakuwa lengo kuu la maisha/kusudi lako kuu la maisha.

Kutaka kuonekana wewe ni wa maana kuliko wengine, na kuona thamani yako ipo katika kila kitu ulichonacho badala ya kuona thamani yako iko kwa Kristo.

Utakutana na Wakristo wengi leo wanatabia hii kila wanapofika ni kuanza kusema mafanikio yao,utajiri wao wana miliki hiki na hiki, wamesoma sana nk. Na lengo lao wanataka watu wawaone kwa thamani na kuwaheshimu kutokana na hadhi walionayo lakini si kwamba wamtukuze Mungu kupitia wao.

Hivyo haya yote Mkristo hutakiwi kuruhusu yamee katika maisha yako anza leo kupiga hatua ikiwa unaona kuna moja kati ya haya nakuomba anza kubadilisha mtazamo wako na muangalie Mungu kama msaada wa peke na kubali kirekebika.

Mwambie Yesu..

Eh Yesu ninaomba uniondolee ndani yangu tamaa ya mwili,tamaa ya macho, kiburi cha uzima ndani yangu, nahitaji kufanana na wewe,kukupenda wewe na si ulimwengu huu,maana nimejua iliyo kweli. Asante Yesu nami naamini kuanzia leo naanza kupiga hatua na nitafanikiwa kwa kadiri ya neema na upendo wako mwingi kwangu ninakushuru Baba ni katika Jina la Yesu Kristo Amen.”

Ubarikiwe sana.

Mawasiliano 0613079530.

@Nuru ya upendo.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *