Nawezaje kumfahamu Mungu?.
Nakusalimu katika Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo. Karibu tuyatafakari maneno ya uzima.
Kila mtu aliemwamini Yesu Kristo yaani Mkristo anatamani kumfahamu zaidi Mungu na anatamani Mungu ajifunue kwake azidi kumfahamu zaidi.
Lakini bahati mbaya Wakristo wengi wanaishia kumjua tu Mungu lakini wengi hawamfahamu Mungu. Utajiuliza ni kwa namna gani? Kabla ya kuendelea mbele ni muhimu sana tujifunze kuyatofautisha maneno haya mawili yanaonekana kama hayana tofauti lakini yanatofauti kubwa kama utakaa na kujifunza.
Tutatazama tofauti iliyopo kati ya KUJUA NA KUFAHAMU.
Kujua maana yake ni nini? Ni kuwa na taarifa au maarifa machache juu ya jambo fulani. Kujua kwa maana rahisi kunahusinana na ukweli wa kawaida tu au taarifa za jumla kuhusu jambo fulani.
Mfano unapojua jina la mtu mfano Paulo hapo unakuwa unamiliki taarifa hiyo bila kufahamu kwa undani zaidi.
Mfano mtu anaweza akasema “najua leo mvua itanyesha kutokana na mawingu ninayoyaona..” Lakini hajui kwa undani ni mchakato gani umefanyika mpaka ikawa hivyo.
Kufahamu ni nini maana yake? Hii ni hatua ya juu zaidi ambayo inajumuisha kuelewa kwa kina zaidi juu ya taarifa,kuoanisha,na uwezo wa kutumia maarifa hayo ili kuleta matokeo. Kwa maana nyingine ni kwamba kufahamu kuna husisha kuelewa sababu,mantiki au athari ya jambo fulani.
Mfano kufahamu jinsi mvua inavyotokea kunahitaji kuelewa mchakato wa hali ya hewa(mvukizo,unyevunyevu,Baridi husababisha matone ya mvua kuanguka).
Sasa Wakristo wengi wanaishia kuwa na taarifa za Mungu tu yukoje lakini hawafahamu kwa undani.. hii ni hatari sana. Ndio maana tunakwama katika maeneo mengi na shetani anatutaabisha kwa sababu hatuna ufahamu kuhusu Yesu Kristo.
Jambo hili Paulo aliliona kwa watakatifu waliokuwa Efeso akaomba kwa ajiri yao ufahamu wao(wafumbuliwe macho wamuelewe Kristo kwa kina).
Waefeso 1:17“Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye;”
Sasa ukisoma hapo utaona limetumika neno KUMJUA. Sasa ili kuelewa vizuri hapa tusome version ya kiingereza ili tuelewe vyema..
Ephesians 1:17
[17][For I always pray to] the God of our Lord Jesus Christ, the Father of glory, that He may grant you a spirit of wisdom and revelation [of insight into mysteries and secrets] in the [deep and intimate] knowledge of Him,
Maana yake…
Waefeso 1:17
[Kwa maana daima naomba kwa] Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, kwamba awajalieni roho ya hekima na ufunuo [wa kuelewa siri na mafumbo] katika [maarifa ya kina na ya karibu] juu Yake.
Unaona hapo mwisho anasema “deep and intimate “
Yaani deep maana yake ni kina yaani kuwa na uelewa wa ndani kwa kina zaidi au sawa sawa na kuwa na uhusiano wa ndani kabisa na Mungu kwa kumuelewa zaidi.
Na intimate ni kwa ukaribu zaidi yaani ubaribu sio kuwa wa kawaida kwa maana ukaribu wenye mahusiano ya ndani sana kama mke na mume au (Kristo na kanisa lake).
Sawa Wakristo wengi wanakesha wanalia na wanakuwa na shauku tu ya kumfahamu Mungu lakini haiwi hivyo.. wakati mwingine wanapeleleza peleleza huenda kwa watumishi ili kumfahamu zaidi Mungu lakini bado kunakuwa na pengo kubwa mioyoni mwao.
Sasa ni kwa namna gani tunaweza kumfahamu Mungu ziko njia nyingi sana lakini tutaangalia chache na kwa ufupi ikiwa utazifata basi utaanza kuona uelewa wako kuhusu Mungu unaanza kuwa mkubwa zaidi.
Hatua hizi ukizifuata basi utaanza kumfahamu Mungu na kuwa na mahusiano naye ya Karibu sana.
1.Kusoma Biblia na vitabu.
Wakristo wengi wanataka kumjua Mungu ilihali hawataki kushika biblia kusoma.. ni wavivu Mkristo anakaa na biblia wiki nzima anakuja kuifungua jumapili ibadani tena kwa muelekezo ya mtoa somo labda fungua kitabu fulani na fulani akimaliza hapo hasomi hata ukurasa wote kupata Muktadha wa Habari yote anapoishia mchungaji nae anaishia hapo hapo.
“Ukitaka kumfahamu Mungu soma biblia.. utamuona sana na utamuelewa sana” hatuwezi kumuelewa Mungu nje na biblia wala hatuwezi kupata taarifa zake,upendo wake nk nje na biblia.
Kama si mtu wa kusoma vitabu mbali mbali wa watumishi wa kweli hutaweza kumuelewa Mungu katika maeneo mengi pia.
“Usipuuzie kusoma usikubali kukosa maarifa kwa sababu ya uzembe amua leo” maarifa mengi yapo kwenye vitabu yamevuchwa humo.
2.kuomba na kutafakari.
Wakristo wa siku za Mwisho ni wavivu wa kuomba ili hali maandiko yametutaka tukeshe katika kuomba na tuwe macho tusiwe kama wa usiku. Maombi ni nguzo muhimu ya wewe kusimama lakini ni sehemu Muhimu Mungu anayosema na sisi kupitia tafakari Roho Mtakatifu anatufundisha vitu vingi sana.
Usiwe mvivu katika Maeneo haya ni Muhimu sana.
3.Epuka uovu.
Hii ni njia ya Mungu kujifunua kwako na kumfahamu zaidi pale unapokuwa ni mtu wa kuepukana na uovu. Kama vile Ayubu alikuwa ni mtu anaemcha Bwana na kuepukana na uovu kwa kipindi hakuwa anaona chochote lakini Mungu baadae anamtokea na kujifunua kwake kwa namna isiyokuwa ya kawaida.
Naimani ukifata hatua hizi ambazo kila siku unazisoma na kuzisikia utaanza kuona mabadiliko makubwa sana. Utaanza kumfahamu Mungu katika viwango vikubwa kabisa.
4.kuwashuhudia wengine habari njema.
Unapotii agizo la kwenye Mathayo 28:19 huko huko katika uinjilisti utaanza kupata ufahamu mkubwa kuhusu Mungu. Mungu anapokutumia kumfundisha na kumhubiria mwingine hakuachi hivyo hivyo anakufundisha pia maandiko yanasema…
Warumi 2:21.“basi wewe umfundishaye mwingine, je! Hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe?”
Nimekuombea na Mungu wa Mbinguni atakutia nguvu kuyatimiliza yote haya katika furaha amani na upendo na zaidi sana amani itazidi kutawala ndani yako maana utakuwa unaufahamu mkubwa na Mwokozi.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.