Silaha anazotumia shetani kumaliza nguvu za mwamini.

Biblia kwa kina No Comments

Silaha anazotumia shetani kumaliza nguvu za mwamini.

Mwamini ni mtu aliyemwamini Bwana Yesu Kristo na kuzaliwa mara ya pili (kuokoka).

Sasa ifuatayo ni silaha ambayo shetani anaitumia kumaliza nguvu za rohoni kwa mwamini (zipo silaha nyingi lakini leo tutazame baadhi tu).

1.Uzinzi na uasherati.

Unapofanya uzinzi au uasherati baada ya kuzaliwa mara ya pili, au unapojihusisha na mahusiano yoyote ya kipepo, hapo tayari unakuwa umejiuza kwa shetani moja kwa moja.. Na hicho ndicho kilichomwangusha Samsoni…Biblia inasema katika Mithali 31:3 “Usiwape wanawake nguvu zako;…”. Na inasema pia..

1Wakorintho 6:18 “Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe”.

Hapo inasema, ikimbieni sio ikemeeni…

Siku hizi ni fashion kila kijana kuwa na girlfriend, na binti kuwa na boyfriend, tena hayo yanafanyika kanisani, na kila mtu anajua..halafu huyo huyo analalamika siku hizi nguvu za kusali zimeisha, anasumbuliwa na mapepo, anaota ndoto mbaya, akisoma neno dakika mbili anasikia usingizi, anashindwa kujizuia kutenda dhambi, mambo yake hayaendi sawa n.k..Sasa hizo nguvu zitatoka wapi wakati tayari umeshampa shetani?…tayari shetani kashamaliza nguvu zako kwa uasherati wako huo, hiyo nguvu ya kuomba utatolea wapi?, hiyo nguvu ya kusoma neno utatolea wapi, hiyo nguvu ya kwenda kuhubiri utatolea wapi, hiyo nguvu ya kufunga utatolea wapi?, utakemea pepo gani litoke?..kwaufupi katika roho, shetani ameshakupofusha macho na anakusagisha ngano katika gereza lake kama alivyomfanya Samsoni. (Waamuzi 16:21).

2.Ibada za sanamu.

Hii ni silaha ya pili, shetani anaoutumia kumaliza nguvu za mkristo, (kumbuka hapa tunamzungumzia yule mkristo wa kweli na sio yule mkristo jina). Siku zote mtu anapozaliwa mara ya pili, hapaswi kumwambudu mtu yeyote wala kitu chochote, au kitu Fulani kilichotengenezwa kwa mikono yetu kichukue nafasi ya Mungu.. ukifanya hivyo tayari umemfungulia shetani mlango wa kukuondolea nguvu zako za kiroho.

Utafutaji mali kupitiliza kiasi kwamba hauna muda wa kufanya ibada ni sawa na kuabudu sanamu/miungu, kukesha mitandaoni kutazama vichekesho, na kuperuzi ni kutumikia mungu mwingine na ni hatari sana kufanya hivyo kama umeokoka.

Vilevile kupenda kula mara kwa mara kiasi kwamba huwezi hata kuwa na ratiba ya kufunga na kuomba kila week, tumbo inakuendesha..basi tumbo yako tayari ni mungu mwingine ndio maana kila ukiamka unawaza kula tu (Wafilipi3:19). Na hii ni silaha madhubuti anayoitumia shetani kudhoofisha nguvu za mwamini kwa kiasi kikubwa sana, CHAKULA!!.

Unakumbuka kule jangwani katika ile safari ya wana wa Israeli, shetani alipoona ameshindwa kuwaloga kwa uchawi wa Balaamu, aliwaandalia karamu ya vyakula na habari yao ikawa imeisha.

Hesabu 25:1-3 Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu;

[2]kwa kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; WATU WaKALA CHAKULA, wakaisujudu hiyo miungu yao.

[3]Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori; hasira za BWANA zikawaka juu ya Israeli.

Na hii ni moja ya jaribu pia alilolitumia shetani kutaka kumuangusha Bwana Yesu akidhani kuwa yeye ni kama sisi.

Mathayo 4:2-4 Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa.

[3]Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate.

[4]Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.

Kama mkristo epuka kupenda kula kula kila wakati, epuka kualikwa alikwa kwenye maparty, jifunzeni kuuweza mwili wako kwa habari ya tumbo.

Na mambo mengine yote yaliyosalia yaliyo kinyume na Neno la Mungu ni mlango wa adui kumuangusha mwamini. Mfano wa mambo hayo ni yale tunayoyasoma katika..

Wagalatia 5:19-21 Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,

[20]ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,

[21]husuda, ulevi, ulafi, NA MAMBO YANAYOFANANA NA HAYO, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.

Hapo anasema mambo yanayofanana na hayo, ikiwa na maana yapo mengi… mfano kusikiliza miziki ya kidunia, kutazama filamu zenye maudhui ya uzinzi na uongo, kutazama picha chafu mitandaoni, kushabikia mipira ya kidunia, kucheza magemu na kubeti/kamari, usengenyaji, uvaaji mbaya, mapambo ya nje, kwa ufupi kuupenda ulimwengu kwa ujumla ni mlango anaoutumia shetani kumaliza nguvu za mwamini.

Silaha ya tatu na ya mwisho kwa leo.. Kujitenga na wenzako.

Mbinu ya kwanza shetani anayoitumia kuwaangusha watu, ni kuwatoa katika kundi!..(kuwatenga na kundi), atanyanyua kisa tu , ambacho kitamfanya huyo mtu akereke na aache kwenda kanisani. Na yule mtu kwa kudhani kuwa “kujitenga na wenzake, ndio atakuwa salama, kumbe ndio kajimaliza”.

Ukishaanza kuona au kusikia hii sauti ndani yako inayokuambia kuwa “ibada ndefu sana”..au mwamini mwezako ni mbaya, waumini wenzako hawakujali n.k basi jua ni shetani anakuhubiria kutaka kukutoa katika kundi, ili akumalize nguvu zako za kiroho vizuri. Biblia inasema..

Waebrania 10:25 “WALA TUSIACHE KUKUSANYIKA PAMOJA, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia”.

Tena inasema..Mhubiri 4:9 “Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao.

10 KWA MAANA WAKIANGUKA, MMOJA WAO ATAMWINUA MWENZAKE; LAKINI OLE WAKE ALIYE PEKE YAKE AANGUKAPO, WALA HANA MWINGINE WA KUMWINUA!

11Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto?

12 Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi”.

Unaweza kusema nikiwa peke yangu, ninaweza kusimama… lakini nataka nikuambia..mtu anayelala hajui dakika aliyoingia usingizini, vile vile mtu aliye pekee yake siku za kwanza atajiona nafuu lakini ndivyo anavyozidi kupoa kidogo kidogo na mwisho kupotea kabisa..

Hivyo kamwe usijitenge na wenzako. Mithali18:1 “Ajitengaye na wenzake hutafuta matakwa yake mwenyewe; Hushindana na kila shauri jema”.

Kumbuka ijapokuwa tunaitwa wakristo, bado hatutakosa kasoro kabisa, mchungaji hawezi kuwa mkamilifu saa zote, muumini mwanzako hawezi kuwa Malaika.. hivyo viwango unavyovitaka uvione hutaviona katika kanisa lolote lile duniani, unachopaswa kufanya ni kuwa mvumilivu, na kuendelea kudumu pale ukiomba na kupambana kurekebisha hizo kasoro..ili hatimaye zipotee kabisa ndani ya kanisa na si kuondoka..

Hizo ni baadhi ya silaha au mbinu anazotumia shetani kumaliza nguvu za mwamini.

Hivyo..tunachopaswa kufanya ni kuvaa silaha zote za Mungu ili kuweza kupinga hila za shetani.

Waefeso 6:10-18 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.

[11]Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.

[12]Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

[13]Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.

[14]Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,

[15]na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;

[16]zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

[17]Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;

[18]kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;

Jitenge na dhambi, jitenge na ulimwengu, lakini usijitenge na wenzako wenye imani moja na wewe. Lakini pia dumu katika kuomba na kusali.. kuwa na kiasi katika vitu unavyovitazama na kusikiliza, lakini pia na kufanya (kazi), pamoja na kula.

1Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze”.

Bwana Yesu akubariki.

Maran atha!

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *