USIWEKE TUMAINI LAKO HAPA DUNIANI.
Yeremia 45: 5 “Je! Unajitafutia mambo makuu? Usiyatafute; kwa maana tazama, nitaleta mabaya juu ya wote wenye mwili, asema BWANA; lakini roho yako nitakupa wewe iwe nyara, katika mahali pote utakapokwenda”
Shalom: Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe.
Karibu tujifunze maneno ya uzima.
Mtume Paulo kwa ufunuo wa Roho aliandika…
1Wakorintho7:29 Lakini, ndugu, nasema hivi, muda ubakio si mwingi; basi tokea sasa wale walio na wake na wawe kama hawana;
30 na wale waliao kama hawalii; na wale wafurahio kama hawafurahi; na wale wanunuao, kama hawana kitu.
31 Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita.
Wakolosai 3:1 Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.
2 Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi.
Je! tumaini lako umeweka wapi?
Je! moyo wako uko wapi?
Hazina yako umewekeza wapi?
Je! Ni hapa duniani au katika ule ulimwengu ujao!
Unafahamu kuwa muda ulio bakia ni mfupi sana, unafahamu kuwa kuanzia sasa Kristo anaweza akarudi muda wowote!!
Je! atakuta moyo wako wapi?
Ni kwenye mali au kwenye ibada?
Leo Bwana anakushauri kuwa usiweke tumaini lako hapa duniani, kwamaana hii dunia inaenda kuharibiwa hapo mbele. Ni heri ukaweka tumaini lako kwa Kristo na kuitazamia ile mbingu mpya na nchi mpya ambayo itakuja kufunuliwa, Bwana Yesu alisema…
Mathayo 6:19-21″Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba;
[20]bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi;
[21]kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.”
Je! hazina yako umeweka wapi, ni huko mbinguni au hapa duniani? kumbuka moyo wako uliko ndiko na hazina yako iliko pia, yaani kama moyo wako upo kwenye ufahari wa mambo ya duniani, majumba, magari, mali, ndoa, n.k, ujue huko ndiko fungu lako lipo, (kuwa na mambo hayo sio vibaya ila hupaswi kuweka moyo wako kwenye mambo hayo) kiasi kwamba unakosa muda wa kufanya ibada, muda wote unawaza hayo. Habari za unyakuo, na kwenda mbinguni hutaki kusisikia kabisa, mipango yako ni hapa tu duniani, Unataka tu uendelee kufurahia na kuutumia ulimwengu.
Basi, ukiwa ni mmojawapo wa watu hao, Roho Mtakatifu anakushauri leo kuwa…
“..Usijitafutie mambo makuu? Usiyatafute; kwa maana tazama, Bwana analeta mabaya juu ya wote wenye mwili.” (Yeremia 45:5)
Weka hazina yako mbinguni na moyo wako pia utakuwa huko, anza kuujenga mji wako huko mbinguni, anza kufikiri yaliyo juu Kristo aliko, tafuta kufanya mapenzi ya Mungu kwa muda huu kidogo uliobakia, kama Bwana amekupa mali, nyumba nzuri, mume/mke mzuri basi.. hekima ya Roho Mtakatifu inakuambia uwe kama asiye navyo, Kwamaana hizo vyote vinaharibika ila yale uliyoyawekeza mbinguni hayawezi kupotea wala kuharibika..
Ila iwapo utakataa hii hekima ya Roho Mtakatifu, ukachagua kufurahia anasa na starehe za dunia hii, na kujitumainisha kwa hayo..basi fahamu kuwa haitakufaidia kitu maana utakuwa umepoteza nafsi yako.
Marko 8:36 Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?
Mali zako unazitumiaje, je! Unajenga ufalme wa Mungu kwa kuhubiri injili, au unajitumainia na utajiri pamoja na utukufu wako, fahamu kuwa siku ukifa au unyakuo ukija hautaondoka na kitu. Biblia ndivyo inavyosema..
Zaburi 49:16 Usiogope mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya nyumba yake itakapozidi.
17 Maana atakapokufa hatachukua cho chote; Utukufu wake hautashuka ukimfuata.
Yatafakari yaliyo juu Kristo aliko wala si yaliyo chini duniani shetani aliko, fahamu kuwa ukifa..vyote ulivyotaabikia havitakufuata bali matendo yako yatakufuata huko uendako.
Huu si wakati wa kulemewa na mambo ya dunia hii, fahamu kuwa tunaishi katika muda wa nyongeza, Kristo anarudi muda wowote. Ni heri utafute kusalimisha roho yako kwa Kristo na yeye anasema..
Yeremia 45:5 “….. lakini roho yako nitakupa iwe nyara, katika mahali pote utakapokwenda.”
Kama hujampa Yesu maisha yako.. yaani hujaokoka. Basi, fahamu kuwa umechelewa sana, usiendelee kukawia..mara moja amua kutubu dhambi zako na kumgeukia Kristo kabla mlango wa neema haujafungwa.
Tubu kwa kumaanisha kuacha dhambi kabisa na utafute ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo sawa sawa na “Matendo 2:38”
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.