
TAFUTA KUWEPO KATIKA UFUFUO WA KWANZA
Nakusalimu katika jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo. Karibu tujifunze maneno ya uzima.
Biblia inasema ana heri mtu yule ambaye atakuwa na sehemu katika ufufuo wa kwanza, ikiwa na maana kuna ufufuo wa kwanza na ufufuo wa pili.
Tunasoma..
Ufunuo wa Yohana 20:4 “Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu.
[5]Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu.
[6]Huo ndio ufufuo wa kwanza. HERI, NA MTAKATIFU, NI YEYE ALIYE NA SEHEMU KATIKA UFUFUO WA KWANZA; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu”.
Huu ufufuo wa kwanza na wa pili ni upi?
Ufufuo wa kwanza, umejumuisha wale watakatifu waliofufuka na Bwana Yesu ukisoma (Mathayo 27:52) utaona..,pamoja na watakatifu watakao fufuka katika unyakuo, na watakao fufuliwa wakati wa kuingia kwenye ule utawala wa miaka 1000 (Ufunuo 20:4) haya ni makundi matatu yanayotengeneza aina ya kwanza ya ufufuo.
Na ufufuo wa pili utakuja mara tu baada ya utawala wa miaka 1000 kuisha..ambapo wafu wote ambao hawakuwepo katika ufufuo wa kwanza watafufuliwa na kuhukumiwa na Kristo mwenyewe katika hukumu ya kile kiti cheupe cha Enzi cha Yesu Kristo tukisoma
Ufunuo 20:11 “Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana.
12 Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.
13 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.
14 Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto.
15 Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.”
Kwahiyo ndugu biblia inasema wana heri wale watakaokuwepo katika ule ufufuo wa kwanza. kwasababu mauti ya pili haitakuwa na nguvu juu yao. Na mauti ya pili ni ziwa la moto. Hivyo tujitahidi hata kama Bwana atakupokuja akatukuta tumelala(tumekufa), basi tuwe na nafasi katika ule ufufuo wa kwanza.
Kumbuka mtu anapokufa sasa hivi nje ya Yesu Kristo (yaani bila kutubu dhambi na kumpokea Yesu) moja kwa moja anashuka kuzimu mahali pa mateso, kusubiria ufufuo wa pili na hukumu ya ziwa la moto. Lakini mtu akifa leo katika Bwana, ana heri kwasababu atakwenda mahali pema peponi kusubiria siku ya unyakuo ambao watakatifu wote waliolala watasikia sauti ya parapanda kisha watafufuliwa wataungana na watakatifu walio hai na wote watanyakuliwa juu kumlaki Bwana Yesu mawinguni.
1Wathesalonike 4:15 “Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti.
[16]Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza.
[17]Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.”
Je! Umesikia injili Ya toba na kutubu dhambi, je! Umepokea muhuri wa Roho Matakatifu?
Kama bado unasubiri nini na muda tuliobakiwa nao ni kidogo sana. Na wewe mwenyewe hujui saa utakayoiaga hii dunia. Ni heri ukatubu dhambi leo na kudhamiria kumfuata Yesu kwa gharama zote.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.