
ONDOKA !!!
Kuna dhambi zingine huwezi ukaviacha mpaka uamue kuchukua hatua ya kuondoka katika hiyo dhambi kwa miguu yako kabisa.
Kwa mfano huwezi kusema umetubu na bado ukaendelea kukaa hapo kijiweni na wahuni, au ukaendelea kukaa hapo kilabuni, au ukaendelea kukaa na huyo mwanaume/mwanamke unayezini naye,…hapo haijalishi utaomba toba na kusalishwa sala ya toba mara mia, haijalishi utalia kwa machozi na kuapa kutorudia tena kufanya uliyoyafanya. Kama hujaamua kuondoka hapo ni kazi bure tu wala bado hujatubu.
Tunasoma kwa habari yule mwana mpotevu aliyepewa mali na baba yake..akaenda kutapanya huko mbali, kwa maisha ya uasherati… lakini baadaye mambo yaliyopokuwa magumu akawaza moyoni mwake kumrudia baba yake, na alipozingatia moyoni mwake, akaamua kuondoka hapo alipo katika maisha ya tabu na mateso.
Luka 15:13 “Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati.
[14]Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji.
[15]Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe.[17]Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa.
[18]NITAONDOKA, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako;
[19]sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.
[20] AKAONDOKA, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana”.
Unaona hapo, “AKAONDOKA ” na alipoondoka ndipo akaenda kukutana na baba yake tena, na maisha yake yakabadilika.
Na leo na wewe…hebu tafakari maisha ya tabu na mateso ambayo unayapata kwa shetani, fikiria hiyo pombe, sigara, bangi, mirungi, tangu ulipoanza kutumia umepata faida gani?
Kwanini leo usiamue kuondoka hapo na kuacha hivyo vitu ambavyo vinaharibu mwili wako na hatima ya maisha yako.
Ondoka!! Kimbia ulevi, kimbia uasherati!! Ondoka kwenye kampani za wasengenyaji, Ondoka mara moja na usirudi tena.
Futa picha zote chafu, futa miziki na video zote za kizinzi, left magroup yote ya misahaa, katiza mahusiano yote ya kipepo, choma mavazi yote yasiyo na adabu, ondoa mapambo yote ya kidunia kwenye mwili wako…kisha nenda mbele za Mungu muombe akurehemu. Hapo ndipo utakuwa umetubu na Bwana atakupa nguvu za Roho Mtakatifu atakayekusaidia kuendelea mbele.
Ukiwa unahitaji kuongozwa sala ya toba, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.