
KUTOA KAMA SEHEMU YA UTUMISHI.
Nakusalimu katika jina kuu sana la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tuyatafakari maandiko. Sisi kama wakristo, ili tuweze kukua kutoka utukufu hadi utukufu, na imani hadi imani, hatuna budi kuyatafakari maneno ya Mungu sana kwa kadiri tuwezavyo.
Leo tutajifunza umuhimu wa kumtumikia Mungu kwa njia ya matoleo. Watu wengi wamekariri kuwa utumishi ni ule tu wa kusimama madhabahuni kama mchungaji, au kwenda kuhubiri kama munjilisti au watu wengine wanaojulikana kama watumishi wa Mungu. Lakini hawajui kuwa hata kuwahudumia watakatifu na watumishi wa Mungu ni utumishi kama tu utumishi mwingine.
Hebu tusome maandiko haya…
2Wakorintho 9:11 “mkitajirishwa katika vitu vyote mpate kuwa na ukarimu wote, umpatiao Mungu shukrani kwa kazi yetu.
[12] MAANA UTUMISHI WA HUDUMA HII hauwatimizii watakatifu riziki walizopungukiwa tu, bali huzidi sana kuwa na faida kwa shukrani nyingi apewazo Mungu;
[13]kwa kuwa mkijaribiwa kwa utumishi huo, wanamtukuza Mungu kwa ajili ya utii wenu katika kuikiri Injili ya Kristo, na kwa ajili ya ukarimu wenu mliowashirikisha wao na watu wote”.
Umeona hapo, anasema “utumishi wa huduma hii” yaani huduma ya utoaji. Una faida nyingi sana.
Unapotoa sadaka zako madhabahuni au kwa watumishi wa Mungu wa kweli wanaohubiri injili, unakuwa umeshiriki ule utumishi sawa tu na wao. Kama ni mtu mmoja ataenda kuokolewa mahali fulani…na wewe unakuwa miongoni mwa waliomuokoa yule mtu na hivyo dhawabu yako haitakupotea. Ndivyo Neno la Mungu linavyosema…
1 Wakorintho 3:6 Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu.
[7]Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye.
[8] BASI YEYE APANDAYE, NA YEYE ATIAYE MAJI NI WAMOJA, lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa na taabu yake mwenyewe.
Hivyo usione ugumu kuchangia injili kwa namna yoyote ile, usisubiri mpaka ukumbushwe kuchangia, unapopata nafasi ya kuwasafirisha watumishi wa Mungu wakahubiri injili vijijiji au mijini usiwe mzito kufanya hivyo maana ni huduma yako.
Warumi 10:14-15 “Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri?
[15]Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!
Halikadhalika unapoona mtumishi wa Mungu wa kweli ana uhitaji Fulani, nawe unauwezo wa kumsaidia usisubiri mpaka akuambie…we Fanya tu yakupasayo maana huo ni utumishi wako. Na sio watumishi tu, hata watakatifu wote wenye uhitaji, wahudumie kwa mahitaji yao kwa kadri uwezavyo (kwa moyo wa upendo).
Lakini pia jambo lingine la kujua ni kwamba utoaji wako mbali tu na kuwa ni sehemu ya utumishi, lakini pia ipo faida kubwa sana utakayoipata pale unapojitoa kuwasaidia watakatifu na watu wote. Na faida hiyo ni ile shukurani zinazomfikia Mungu kupitia watu hao uliowasaidia.
2Wakorintho 9:11 “mkitajirishwa katika vitu vyote mpate kuwa na ukarimu wote, UMPATIAO MUNGU SHUKRANI KWA KAZI YETU.
12 Maana utumishi wa huduma hii hauwatimizii watakatifu riziki walizopungukiwa tu, bali HUZIDI SANA KUWA NA FAIDA KWA SHUKRANI NYINGI APEWAZO MUNGU;”
Nataka uone hilo neno.. “HUZIDI SANA KUWA NA FAIDA”… Maana yake ni kwamba pamoja na faida hiyo iliyotajwa hapo ya “kuwatimizia watakatifu riziki zao”..lakini pia Faida iliyo kubwa kupita yote ni hiyo kwamba “MUNGU ATAPEWA SHUKRANI NYINGI”.
Unawasaidia mayatima, wale mayatima watamshukuru MUNGU SANA KWA KILE WALICHOKIPOKEA… Na ndicho Mungu anachokihitaji sana.. SHUKRANI… shukrani.
Unaweza kuona kama shukrani ni jambo dogo!.. lakini kwa MUNGU ni jambo kubwa…
Mungu anapendezwa na shukrani kuliko maombi mengi tuyapelekayo mbele zake… Unaweza kutumia lisaa limoja kumshukuru tu MUNGU kwa mema yake na ukapata faida kubwa kuliko kupeleka mahitaji orodha ya mahitaji kwa muda huo.. (Shukrani ni darasa pana sana na lenye faida kubwa sana kiroho).
Na hapa Neno la Mungu linasema kuwa “shukrani atakazopewa MUNGU kutoka kwa wale waliopokea, basi hizo ni faida kubwa”.
Mtu akimshukuru Mungu kwaajili ya kile ulichotoa, hiyo ni faida kubwa kwako, Maskini akimshukuru Mungu kwaajili ya kile ulichotoa hiyo ni faida kubwa kwako, Mtumishi wa Mungu akimshukuru Mungu kwaajili ya kile ulichotoa hiyo ni faida kubwa kwako, Yatima akimshukuru Mungu kwaajili kile ulichotoa hiyo ni faida kubwa kwako, Mnyonge akimshukuru Mungu kwaajili ya kile ulichotoa hiyo ni faida kubwa kwako.
Penda kuwa mtoaji sana…daima kumbuka haya maneno la Bwana Yesu..
Matendo ya Mitume 20:35 Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, NI HERI KUTOA KULIKO KUPOKEA.
Maran atha (Bwana Yesu anarudi)
Shalom
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.