
ALAMA KWA WATEULE WA MUNGU KABLA YA MAANGAMIZI.
Jina kuu la BWANA YESU mkuu wa uzima libarikiwe. Karibu tujifunze biblia.
Kabla maangamizi hayajaja Mungu huwa anawatenga waovu na wema katikati ya watu wake kwa kuwatia ALAMA.
Katika biblia tunasoma, kuna wakati ulifika maovu yalizidi sana katika nyumba ya Israeli ndipo Mungu akamuonyesha Ezekieli maono ya mambo yaliyokuwa yanaendelea kwa siri katikati ya watu wake. Alionyeshwa watu wakiabudu JUA katika ya nyumba yake, wengine walikuwa wanamlilia TAMUZI (miungu ya wakaldayo), wengine wanaabudu vinyago kwa siri katika nyumba zao, na makuhani wanavukiza uvumba kwa miungu migeni,(Ezekieli 8:1-18), alionyeshwa dhuluma katika mji na umwagaji damu,na upotoshaji hukumu umejaa, na zaidi sana kulinyanyuka manabii wa uongo waliokuwa wanawatabiria watu amani wakati hamna amani. Yote haya yalimchukiza Mungu sana mpaka kuifikia kilele cha Mungu kuleta hukumu kwa watu wake wote.
Lakini kabla ya hukumu, kuna watu wachache ambao walikuwa wanaugua na kuomboleza Kwasababu ya maovu yanayotendeka, hivyo Mungu akawatenga kwanza kwa kuwatia alama katika nyuso zao, Tunasoma…
Ezekieli 9:1-6 Kisha akalia kwa sauti kuu masikioni mwangu, akisema, Waamuru wale wanaousimamia mji wakaribie, kila mmoja na awe na kitu chake cha kuangamiza mkononi mwake.
[2]Na tazama, watu sita wakaja, wakitokea kwa njia ya lango la juu, lielekealo upande wa kaskazini, kila mmoja ana kitu chake cha kufisha mkononi mwake; na mtu mmoja kati yao amevaa bafta, naye ana kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. Wakaingia, wakasimama karibu na madhabahu ya shaba.
[3]Na huo utukufu wa Bwana wa Israeli ulikuwa umepanda juu kutoka kwa kerubi, ambaye ulikuwa juu yake, mpaka kizingiti cha nyumba; akamwita mtu yule aliyekuwa amevaa bafta, mwenye kidau cha wino cha mwandishi kiunoni.
[4]BWANA akamwambia, Pita kati ya mji, kati ya Yerusalemu, UKATIE ALAMA KATIKA VIPAJI VYA NYUSO VYA WATU WANAOUGUA NA KULIA KWA SABABU YA MACHUKIZO YOTE YANAYOFANYIKA KATI YAKE.
[5]Na hao wengine aliwaambia, nami nalisikia, Piteni kati ya mji nyuma yake, mkapige; jicho lenu lisiachilie, wala msione huruma;
[6]Waueni kabisa, mzee, na kijana, na msichana, na watoto wachanga, na wanawake; lakini msimkaribie mtu ye yote mwenye hiyo alama; TENA ANZENI KATIKA PATAKATIFU PANGU. Basi, wakaanza kwa wazee waliokuwa mbele ya nyumba.
Kumbuka watu hawa waliotiwa alama, walitoka miongoni mwa watu wa Mungu na sio katikati ya watu wote wa ulimwengu, hapana bali ni katikati ya watu wake(ISRAELI)..watu wa ulimwengu tayari Mungu alishawawekea hukumu yao katika siku ile.
Ndivyo ilivyo hata sasa hivi, Maovu makubwa yanayopelekea hasira ya Mungu kumwaga sio yatokanayo na watu wasiomjua Mungu.Hapana bali ni kwasababu ya maovu yanayoendelea katika nyumba ya Mungu (yaani kanisa), Katikati ya WAKRISTO aliowanunua kwa damu ya thamani nyingi wivu wake ndimo ulimo. Kumbuka wana wa Israeli walidhani kuwa Mungu haoni waliyokuwa wanayafanya kwa siri, japo aliwapa muda mrefu wa kutubu lakini hawakugeuka mpaka kikombe cha ghadhabu kilipojaa hata kukawa hakuna kusamehewa tena, pale walipotengwa WEMA kati ya WAOVU.
Na katika kanisa la Kristo vivyo hivyo maovu yanayoendelea sasa hivi ni mengi mno vitu kama Siasa, ibada za sanamu (sanamu za watakatifu waliokufa zamani mfano bikira Maria zikiabudiwa n.k.), kanisani kuna vichekesho na mizaha, mchungaji ni mlevi, mwasherati, na mpenda fedha, mtu anajiita mkristo lakini ni vuguvugu, leo yupo kwa Mungu kesho yupo kwa shetani, leo anaenda kanisani kesho disko, leo anavaa vizuri kesho kimini,.leo anamwimbia Mungu kesho anaimba nyimbo za kidunia, leo anasali kesho anasengenya. n.k. Sasa mambo kama haya ndiyo yanayochochea ghadhabu ya Mungu, ni heri haya yangetendeka kwa mtu asiye mkristo kuliko mtu anayesema yeye ni mkristo na kakombolewa na damu ya Mungu na bado anatenda mambo kama hayo huko ni kumtia Mungu wivu mkubwa sana.
Lakini pamoja na hayo kabla Mungu hajashusha ghdhabu yake huwa anawatia ALAMA kwanza WATU WAKE waaminifu katikati ya wanaojiita wakristo, hawa anawatenga na kuwaepusha na mabaya yanayokuja mbeleni. Ndio kitu kinachoendelea sasahivi katika kanisa. Japo yanaonekana mambo ya ajabu na yasiyofaa katika Kanisa, Mungu anaendelea kuwatia muhuri wale waliojazwa Roho na waliowaaminifu na kuwaepusha na ile ghadhabu kwa KUWANYAKUA mbinguni kisha baadaye wale waliosalia wasiotiwa muhuri/alama wataangamizwa, katika siku ile kuu ya Bwana inayotisha. Biblia inasema Nuhu na Luthu walikuwa ni watu wenye haki wakilia juu ya maovu yaliyokuwa yanaendelea katika nchi, hivyo Bwana akawaepusha na Hukumu iliyokuwa inakuja..Kadhalika Bwana YESU pia alisema kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu na Luthu ndivyo itakavyokuwa kuja kwake mwana wa Adamu.
Hivyo ndugu, huu ni wakati wa kufanya IMARA WITO wako na UTEULE wako. Kitu kinachoendelea sasahivi katika roho ni BWANA kuwatia alama wale wanaenenda katika ukamilifu na UTAKATIFU, wasiojitia unajisi na mambo ya ulimwengu huu, walioamua kumwishia Bwana tu na si kingine. Iogope ghadhabu ya Mungu inayokuja tubu sasa uyaweke mambo yako vizuri unyakuo usikupite.
Kumbuka parapanda italia muda wowote, na watakatifu watanyakuliwa…kwani dalili zote zimekwisha timia. Unasubiri nini mpaka sasa usiamue kuokoka kweli kweli??
Mlango wa neema utafungwa muda wowote!!
Maran atha (Bwana Yesu anarudi)
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.