KAMA MIMI NIISHIVYO, ASEMA BWANA.

Biblia kwa kina No Comments

KAMA MIMI NIISHIVYO ASEMA BWANA.Karibu tuyatafakari maandiko matakatifu.

Kwa wale wasomaji wa biblia, mara nyingi sana tumekutana na maneno kama haya “Kama mimi niishivyo, Asema Bwana.” Au mahali pengine imeandikwa “Kama Bwana aishivyo”.

Nini maana ya maneno haya?

‘Kama mimi niishivyo, ASEMA BWANA” Neno hili mara kadhaa limeonekana wakati BWANA akitoa hukumu Fulani kwa mtu au watu, kuthibitisha hukumu hiyo kwamba jambo hilo alilolikusudia kulitenda haliwezi kubadilika daima.

Pia neno hili yaweza kumaanisha ukuu wa Mungu usioweza kujulikana, ahadi zake sisizoweza kubadilika, uaminifu wake..

Na ni vigumu kukutana na neno hili likitumiwa na wanadamu, kwasababu wanadamu siku zote hawaaminiki..ni vigeugeu. Lakini MUNGU yeye habadiliki badiliki kama kinyonga, akisema amesema.

Kwa mfano, neno hili kwa mara kwanza tunasoma katika ile habari ya wana wa Israeli wakiwa jangwani, baada ya kumjaribu Mungu mara kumi..BWANA aliwahakikishia kuwa hawataiona hiyo nchi ya ahadi imiminikayo asali na maziwa..kwasababu ya ugumu wa mioyo yao. Tunasoma..

Hesabu 14:21  “lakini hakika yangu, KAMA NIISHIVYO, tena kama dunia hii nzima itakavyojawa na utukufu wa BWANA;

[22]kwa sababu watu hawa wote, ambao wameuona utukufu wangu na ishara zangu, nilizozitenda huko Misri, na huko jangwani, pamoja na haya WAMENIJARIBU MARA HIZI KUMI, wala hawakuisikiza sauti yangu;

[23]hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona.

26]Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

[27]Je! Nichukuane na mkutano mwovu huu uninung’unikiao hata lini? Nimesikia manung’uniko ya wana wa Israeli, waninung’unikiayo.

[28]Waambieni, KAMA NIISHIVYO, ASEMA BWANA, hakika yangu kama ninyi mlivyonena masikioni mwangu, ndivyo nitakavyowafanyia ninyi;

Pia Bwana alisema kwa kinywa cha Nabii Yeremia juu ya hukumu ya Konia mfalme wa Yuda akisema..

Yeremia 22:24 “KAMA NIISHIVYO MIMI, ASEMA BWANA, hata Konia, mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, angekuwa pete yenye muhuri katika mkono wangu wa kuume, ningekung’oa wewe hapo;

[25]nami nitakutia katika mikono ya watu wale wakutafutao roho yako, na katika mikono yao unaowaogopa, naam, katika mikono ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, na katika mikono ya Wakaldayo.

[26]Nami nitakutupa nje, wewe na mama yako aliyekuzaa, mwende nchi nyingine ambayo hamkuzaliwa huko, nanyi mtakufa huko..

Soma pia

Yeremia 46:18 “KAMA MIMI NIISHIVYO, ASEMA MFALME, ambaye jina lake ni BWANA wa majeshi, hakika yake, kama Tabori katika milima, na kama Karmeli karibu na bahari, ndivyo atakavyokuja.

Unaweza pia ukasoma neno hili katika maandiko haya..Ezekieli 5:11, Ezekieli 14:16, Ezekieli 17:19, Ezekieli 35:11, Sefania 2:9.

Ni nini tutajifunza kutokana na kauli hii ya BWANA?

Bwana Mungu, muumba wa mbingu na nchi anasema katika..

Malaki 3:6-7 “Kwa kuwa mimi, BWANA, sina kigeugeu; ndio maana ninyi hamkuangamizwa, enyi wana wa Yakobo.

[7]Tokea siku za baba zenu mmegeuka upande, mkayaacha maagizo yangu, wala hamkuyashika. Nirudieni mimi, nami nitawarudia ninyi, asema BWANA wa majeshi. Lakini ninyi mwasema, Turudi kwa namna gani?

Bwana hana kigeugeu kama sisi tulivyo, akisema mtu mwovu ataadhibiwa katika jehanumu ya moto!!, anamanisha ataathibiwa kweli!. Akisema waasherati, wazinzi, wachawi, walevi, watukanaji, wasengenyaji, waongo, wafiraji, walawiti, wahuni, waabuduo sanamu wote hawataurithi ufalme wake (Wagalatia 5:19-21), bali sehemu yao ni lile ziwa liwakalo moto na kibiriti sawa sawa na Ufunuo 21:8. Fahamu kuwa maneno hayo hayabadilika daima, bali ndivyo ilivyo.

Lakini pia, Bwana akisema nitakubariki wewe mwenye haki, basi fahamu kuwa ahadi za Bwana hazina kigeugeu, utabarikiwa tu hata kama wachawi wote watasimama juu yako, akisema utafanikiwa ni swala la muda tu, utafanikiwa kweli.

Lakini wewe uliye nje ya wokovu, fahamu kuwa Bwana hafurahii kufa kwake mwenye dhambi. Bwana hafurahii ufe katika ulevi, au katika uzinzi, ukahaba, usagaji, n.k, ni heri leo ukaamua kutubu dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha kabisa na kuamua kumuishia Mungu.

Ezekieli 33:11 “Waambie, KAMA MIMI NIISHIVYO, ASEMA BWANA MUNGU, sikufurahii kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi. Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa, Enyi nyumba ya Israeli?

Mgeukie BWANA YESU leo akuoshe dhambi zako na kukupa Roho Mtakatifu bure atakayekusaidia kuushinda ulimwengu na tamaa zake. Kumbuka tunaishi katika siku za mwisho kabisa na watakatifu watanyakuliwa muda wowote… Bwana alisema kizazi hiki hakitapita!!…itakufaidia nini ukifurahia raha za kidunia ambazo ni za kitambo kidogo tu, na kisha ukakosa uzima wa milele.

Bwana Yesu atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *