LANGO HILI LITAFUNGWA MUDA WOWOTE!!

Biblia kwa kina No Comments

LANGO HILI LITAFUNGWA MUDA WOWOTE!!

Ezekieli 44:1-2 Kisha akanirudisha kwa njia ya lango lile la nje, la mahali patakatifu lililoelekea upande wa mashariki; nalo lilikuwa limefungwa.

[2]BWANA akaniambia, LANGO HILI LITAFUNGWA, HALITAFUNGULIWA, wala mtu awaye yote hataingia kwa lango hili, kwa maana BWANA, Mungu wa Israeli, ameingia kwa hilo; basi kwa sababu hiyo litafungwa.

Kama kuna majira ambayo si ya kufanya mchezo na masuala ya wokovu wetu hata kidogo basi ni haya. Kwani moja ya hizi siku tutashuhudia mabadiliko makubwa sana na ya ghafla katika kanisa la Kristo,..wakati ambao Bwana Yesu anakwenda kuchukua hatua ambayo hakuwahi kuichukua tangu aondoke hapa duniani.. Na hatua yenyewe ni Kuingia na kuufunga mlango wa hekalu lake.

Hayo mambo pengine utayashuhudia kwa macho yako siku si nyingi,..Kumbuka biblia inalifananisha kanisa la Kristo na hekalu lake (Waefeso 2:19-22)..Sasa ukisoma kitabu cha Ezekieli utaona anaonyeshwa matukio yanayoambata na hekalu la Mungu, Na utaona akionyeshwa malango mengi ya hekalu yakiwa wazi, lakini ukisoma ile sura ya 44 utaona Ezekieli anaonyeshwa ghafla lango la mashariki likiwa limefungwa..Na anaambiwa halitafunguliwa tena, wala mtu awaye yote hataingia kwa kupitia lango hilo.

Ndipo Ezekieli akaambiwa sababu ya lango hilo kufungwa, na sababu yenyewe ilikuwa ni hii..tusome..

Ezekieli 44:2 “Bwana akaniambia, Lango hili litafungwa, halitafunguliwa, wala mtu awaye yote hataingia kwa lango hili, kwa maana Bwana, Mungu wa Israeli, ameingia kwa hilo; basi kwa sababu hiyo litafungwa”.

Unaona, sababu ni kuwa Bwana, Mungu wa Israeli (KRISTO), ameingia kwa lango hilo.. Hii ni kuonyesha kuwa mlango huo uliwekwa mahususi kwa ajili yake na si mwingine, yeye ndiye aliyekuwa amewekewa wazi mlango huo mpaka atakapofika,. Hivyo wale waliokuwa wanaingia kabla ya hapo ni neema tu, lakini haukuwekwa wazi kwa ajili yao..

Hivyo Habari hiyo jambo kwa sehemu limetimia lakini ni unabii wa siku za mwisho, wakati ambao Mlango wa Neema utafungwa.

Ndugu, huu mlango ambao tunauita wa neema tulio nao leo hii, Mungu kauacha wazi si kwasababu yetu, bali kwasababu ya Yesu Kristo, Ni mlango wa Kristo Yesu mwenyewe na sio wetu, na moja ya siku hizi, hivi karibuni atasimama, kisha ataupita, na akishaingia, basi utafungwa na ukishafungwa, Habari imeishia hapo hautafunguliwa tena milele..

Mambo yatakayokuwa yanaendelea humo ndani ni siri yake na wale watakaokuwa humo.. Kwahiyo usione unahubiriwa injili, usione unapigiwa kilele utubu dhambi ukadhani Mungu anakuangalia wewe sana, hilo jambo halipo! Mungu anamtazama Kristo tu!, achukue hatua yake, na akishaichukua, hapo ndipo kutakuwa na kilio na kusaga meno kama alivyosema, hakutania alimaanisha kweli wapo watu watalia kweli kweli wakitamani hata nusu saa nyuma lirudi watengeneze mambo yao lakini watakuwa wameshachelewa.

Luka 13:24 “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.

25 Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako;

26 ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu. 27 Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu.

28 Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno…

Hivyo wokovu sio wa kukwepwa, injili si ya kudharauliwa wala kupuuziwa kabisa, huu si wakati wa kumwangalia jirani, au ndugu, au mzazi, katika suala lako la wokovu, Ni wakati wa kumkimbilia Kristo na kumwangalia yeye tu, kwasababu muda uliobakia ni mchache, nani ajuaye lango hilo litafungwa leo usiku, au kesho asubuhi. Jiulize Unyakuo ukipita leo halafu ukabaki, na injili zote hizo ulizosikia, na mafundisho yote hayo uliyofundishwa na kujifunza, utaenda kujibu nini mbele ya kiti cha hukumu.

Usikubali kusongwa na jambo lolote, usikubali kuwa katika kundi lile la wale wanawali wapumbavu, ambao walishindwa kuingia kwenye karamu kwasababu ya upumbavu wao.

Mathayo 25:7  “Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao.

[8]Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika.

[9]Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie.

[10]Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, NAO WALIOKUWA TAYARI wakaingia pamoja naye arusini; MLANGO UKAFUNGWA.

[11]Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie.

[12]Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi.

[13]Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa.

Kama hujaokoka kweli kweli, amua leo kutubu dhambi zako na kumaanisha kuziacha kabisa kisha nenda katafute ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa JINA LA YESU KRISTO sawa sawa na Matendo 2:38 ili upokee Roho Mtakatifu atakayekuongoza katika kweli yote na kukusaidia kuishi maisha ya utakatifu.

Unyakuo umekaribia sana..ni wakati wowote huu mlango wa neema utafungwa kwani dalili zote zimekwisha timia mpaka sasa.

BWANA YESU ANARUDI!!

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *