
YESU MCHUNGAJI MWEMA
Yohana 10:11-16 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.
[12]Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya.
[13]Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake.
[14]Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi;
[15]kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.
[16]Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja”.
Kondoo siku zote anahitaji kuchungwa.. hawezi kujichunga wenyewe, lakini pia hawezi kujilinda na maadui zake kama fisi, mbwa mwitu n.k, hivyo hana budi kuchungwa. Na sisi katika roho kama tumemwamini YESU, sisi ni kondoo na Yesu ni mchungaji, tena sio mchungaji tu bali ni mchungaji mwema, wengine ni wachungaji Lakini sio wema, lakini YESU ni mchungaji mwema tena MCHUNGAJI MKUU…anatuchunga kwa fimbo ya chuma, na kutulinda na maadui wote wanaotufuatilia (wachawi, mapepo, magonjwa n.k). Lakini kama hatupo ndani ya YESU sisi ni kondoo waliopotea na Yesu mchungaji mwema anatutafuta…kwa maana huku tuliko hatupo salama kabisa.
Waebrania 13:20-21 “Basi, Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu,
[21]awafanye ninyi kuwa wakamilifu katika kila tendo jema, mpate kuyafanya mapenzi yake, naye akifanya ndani yetu lipendezalo mbele zake, kwa Yesu Kristo; utukufu una yeye milele na milele. Amina.
Je! Umempokea Yesu leo?.. Je Bwana Yesu ni mchungaji wako?.. kama hujampokea Yesu, bado wewe ni kondoo uliyepotea, ambaye Bwana Yesu, mchungaji mwema ANAKUTAFUTA!!!, kwasababu hapo ulipo haupo salama, mbwa-mwitu wanasikia harufu yako toka mbali na wanakusogelea kwa kasi, fisi na dubu, wanasikia harufu yako na wanakukaribia ili wakudhuru, wakufanye kitoweo… Leo hii umemwona Mchungaji mwema Yesu Kristo, mkimbilie huyo uwe salama, ili hatimaye useme kama Daudi..
“BWANA ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu.
[2]Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
[3]Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
[4]Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.”(Zaburi 23:1-4).
Huko kwenye ulevi ulipo, umepotea, huko kwenye uzinzi, na uasherati ulipo umepotea, huko kwenye dansi ulipo na kwenye miziki, fasheni, na anasa za kidunia umepotea!.. haupo salama!.. Maisha yako yapo hatarini, wewe ni windo bora la mapepo yote, ni windo bora la wachawi, ni windo bora la mauti. Na vyote hivyo vinakutafuta.. Haupo salama kabisa!..kimbilia kwa Yesu…

Kama bado hujaokoka na unahitaji kuokoka ili uwe salama ndani ya Mchungaji mwema Yesu, basi wasiliana nasi inbox tuweze kuomba nawe, sala fupi ya kumkaribisha Bwana Yesu, maishani mwako.
Maran atha!.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.