
VUA VAZI LA UONGO
Waefeso 4:25 “Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake”.
Uongo ni vazi kama ilivyo ukweli…nao ni vazi la haki, lakini uongo ni vazi la uovu… hivyo ni vazi la kuvuliwa.
Mkristo yeyote hapaswi kuvaa vazi hili, ni vazi lenye harufu mbaya sana kwa Mungu. Moja ya vitu sita anavyovichukia Mungu ni uongo.
Mithali 6:16-19 Kuna vitu sita anavyovichukia BWANA; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake.
[17]Macho ya kiburi, ULIMI WA UONGO, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia;
[18]Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu;
[19]Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.
Na uongo siku hizi imerahisishwa kupitia simu, kiasi kwamba kusema uongo imekuwa kawaida kama tu kusalimia. Lakini ni dhambi inayomgusa moyo wa Mungu sana.
Siku moja nilikuwa nasafiri kwenye gari, mama mmoja akapigiwa simu kuulizwa amefika wapi, akasema uongo kabisa wazi wazi kwamba nimefika sehemu fulani kumbe hata hajakaribia hapo, kwa kweli nilishindwa kujizuia maana nilisikia ndani yangu kuwaka, nikamgeukia na kumwambia ”unajua uongo ni dhambi”,.. lakini akoona tu kawaida, (“..wameuzoeza ulimi wao kusema uongo..” Yeremia 9:5), jambo hilo ilimhuzunisha sana Roho Mtakatifu kiasi kwamba nilijihisi mimi ndio nimefanya hilo kosa, hivyo nikawa natubu tu hata niliposhuka.
Ndugu yangu, tuchunge ndimi zetu, tujihadhari na neno “uongo” hakuna uongo mzuri, wala hakuna uongo una faida, na wala hakuna uongo kidogo, uongo ni uongo tu. Kuna kitu mtu anaweza akafanya akoona ni kawaida tu, kwa mfano unaweza ukasema naomba dakika moja nifike, au nifanye jambo fulani ilihali unajua kabisa unaweza hata ukatumia nusu saa huo tayari ni uongo, ni heri hata ingekuwa hujui na kwanini basi utoe muda, huoni ni uongo wa makusudi.. Bwana atusamehe.
Kama watoto wa Mungu tujihadhari na uongo wa aina yoyote, unapoandika ujumbe kwenye simu hakikisha ni ukweli..usiseme hakuna mtu anayesikia au anayesoma… Mungu anakuona, kumbuka Amina na Safira walisema uongo mbele ya watumishi wa Mungu wakidhani hakuna mtu anawafahamu… kumbe Roho Mtakatifu anawashuhudia, unajua kilichowapata…walikufa pale pale kuonyesha jinsi Bwana anavyochukia UONGO”
Ni kweli katika maisha haya jinsi dhambi ilivyoonea duniani, kuna mazingira mengine itakugharimu kuingia hasara ili uwe mkweli, utaonekana mjinga, utacheleweshwa mambo yako, utachukiwa kwasababu tu ya kuwa mkweli, lakini hiyo ndio maana ya kuwa mkristo lazima upitie dhiki kama hizo, hizo ndizo dhiki Bwana alisema tutakutananavyo.
Tuvue leo uongo tuvae kweli, tumuachie ibilisi na watoto wake maana yeye ndiye baba wa uongo, sisi kama watoto wa Mungu aliye wa kweli siku zote tuseme ukweli, kumbuka waongo wote hawana sehemu katika ufalme wa Mungu bali sehemu yao ni lile ziwa liwakalo moto na kibiriti (Ufunuo21:8).
Je! Umefanyika mwana wa Mungu? Kama bado unasubiri nini mpaka sasa?? muda umekwenda sana, hivyo leo mwamini Bwana Yesu na utubu dhambi zako zote na umaanishe kuziacha kisha tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina lake Yesu ili upokee uwezo wa kufanyika mwana wa Mungu sawa sawa na Yohana1:12 “..Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu..”
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.