
NJIA PANA NA NJIA NYEMBAMBA
Nitatambuaje ile njia pana na njia nyembamba?
Bwana Yesu alisema…
“Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, NA NJIA NI PANA iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo.
Bali mlango ni mwembamba, NA NJIA IMESONGA iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.” (Mathayo7:13-14)
Sasa tutajuaje hii ndio njia nyembamba na hii ndio pana ili tuweze kuchangia njia sahihi, tusije tupita katika njia pana huku tukidhani tunapita njia nyembamba!! Kwasababu biblia inasema…
“Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti”. (Mithali14:12)
Kwanza kabisa njia nyembamba hapa biblia inafafanua kuwa ile iliyosonga…ambayo ni wachache tu wanaona na kupita, lakini ile pana anasema ni WENGI wanaopita!! Na kwanini ni wengi wanapita?
Kwasababu haijasonga na haina gharama ya kuikana nafsi, hivyo mtu anaweza akapita tu apendavyo wala hakuna kukemewa na kuonywa bali siku zote ni kufarijiwa tu. Ndio maana wengi wanapita… lakini mwisho wake ni upotevuni.
Hivyo ndugu, angalia ni njia gani umechagua kupita, je ni ile pana au ile nyembamba ambayo wengi hawataki?
Njia nyembamba ni ile inayosema msiipende dunia wala mambo yaliyomo duniani lakini ile njia pana inasema duniani kuna usalama (inahubiri tu mafanikio ya hapa duniani na kumfariji mtu mwenye dhambi aendelee kuishi hivyo),
Lakini ile nyembamba inasema watu watendao mambo ya jinsi hiyo..uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, ulevi n.k hawataurithi ufalme wa Mungu na kwamba wasipotubu sehemu yao ni lile ziwa liwakalo moto na kiberiti sawa sawa na Ufunuo 21:8.
Vilevile ile njia pana inahubiri kwamba mwanamke kuvaa suruali, nguo fupi, na zinazoonyesha maungo yake ni sawa tu maana Mungu anaangalia moyo.. Lakini ile njia nyembamba inasema Mungu anaangalia moyo na mwili (2Wakorintho7:1) hivyo mwanamke kuvaa suruali ni machukizo kwa Mungu (kumbukumbu 22:5).. mwanamke wa kikirsto anapaswa avae kwa kujistiri maana yeye ni nuru ya ulimwengu. (Mathayo5:16)
Njia pana inasema mwanamke kujipamba ni urembo na ni kumpendeza mumewe.. Lakini njia nyembamba inasema kujipamba kwenu kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, KUSUKA NYWELE; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi; bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu. Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao. (1Petro3:3-5),
Kwa maana hiyo kuvaa hereni, mikufu, vipini, nywele za bandia, kucha za bandia, kuweka rangi mdomoni/lipustick na kujipodoa/make up ni machukizo kwa Mungu maana miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu (1Wakorintho6:9)
Njia pana inahubiri ubatizo wa maji na Roho Mtakatifu hauna umuhimu..ukishapokea Roho imetosha, lakini njia sahihi inasema mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho hawezi kuuona ufalme wa Mungu (Yohana 3:5) na kuzaliwa kwa maji ni kubatizwa kwa kuzamishwa kwenye maji mengi na ni kwa jina la Yesu Kristo, na kuzaliwa kwa Roho ni kubatizwa kwa Roho Mtakatifu. Na vyote vina umuhimu.
Swali! Ni Je! Umechagua kupita njia ipi?
Maamuzi ni yako, Mungu ametuwekea njia ya uzima na mauti mbele kwamba sisi tuchague.
“… Tazama naweka mbele yenu njia ya uzima, na njia ya mauti.”(Yeremia 21:8)
Hivyo usiangalie kiongozi wa dini yako au dhehebu lako, au ndugu yako, au mzazi, hebu amua kujikana nafsi na kuchukua msalaba wako na kupita kwenye ile njia iendayo uzimani ambao wengi hawapendi… kumbuka ni wachache waionao, fanya hivyo ili uokoe nafsi na roho yako.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.