SHUKA KILINDILINI UKITAKA KUMSIKIA MUNGU 

Biblia kwa kina No Comments

SHUKA KILINDILINI UKITAKA KUMSIKIA MUNGU 

Nakusalimu katika jina la mwokozi wetu Yesu Kristo. Karibu tutafakari pamoja Neno la Mungu.

Je umekuwa ukitafuta kusikia sauti ya Mungu na hausikii, basi leo kupitia somo hili utaenda kujua ni kwanini hauisikii sauti ya Mungu ingawa Mungu anasema kila siku.

Isaya 50:2 “Basi, nilipokuja, mbona hapakuwa na mtu? Nilipoita, mbona hapakuwa na mtu aliyenijibu? Je! Mkono wangu ni mfupi, hata nisiweze kukomboa? Au je! Mimi sina nguvu za kuponya? Tazama, kwa kukemea kwangu naikausha bahari, mito ya maji naifanya kuwa jangwa; samaki wao wanuka kwa sababu hapana maji, nao wafa kwa kiu”.

Unaona, Mungu anaita lakini watu hawasikii, kwasababu gani? Kwasababu ili uisikie ni lazima uzame mpaka kilindini, (Uingie rohoni) kumbuka Mungu ni Roho hivyo ili tumuone na kumsikia hatuna budi kuingia rohoni… ndio maana ya andiko hili..

Zaburi 42:7 Kilindi chapigia kelele kilindi kwa sauti ya maboromoko ya maji yako, Gharika zako zote na mawimbi yako yote yamepita juu yangu.

kilindi ni mahali pa katikati kabisa mwa bahari. Sasa mwandishi wa zaburi anatumia mifano ya kitu halisi kana kwamba kinaongea… anasema Kinaita chapigia kelele kilindi. Na cha kushangaza ni kwamba hakiiti eneo lingine lolote la maji labda ufukweni.. au kwenye rasi, au ghuba.. hapana bali kinapigia kelele kilindi chenzake.

Kilindi chapigia kelele kilindi

Maana yake ni nini?

Tukitaka mambo ya ndani ya Mungu, mambo ya vilindini, lazima na sisi tuwe vilindini. Ni muunganiko wa ki-Mungu. kila kiwango kina sauti yake. kamwe hizo sauti haziingiliani, ni sawa na mbwa amwite tai kwa sauti yake ya kubweka, haiwezekani kuja inahitaji, ajifunze sauti yake ili yule tai aelewe, vinginevyo atakuwa anapiga kelele tu.

Na sisi vivyo hivyo kwa Mungu, wengi tunatamani tumwone Mungu kwa undani katika maisha yetu, lakini hatutaki tuzame ndani yake. Na tunazamaje ndani/kilindini? hakuna njia nyingine isipokuwa kwa kuwa waombaji na kusoma Neno lake kwa undani huko ndiko kilindini na tukiwa hivyo tutamsikia Mungu wazi wazi.

Lakini sio hilo tu, hata katika maisha ya kawaida, kuna mambo ili tuvipate ni lazima tushuke vilindini. Kwa mfano unataka mwenzi sahihi wa kuingia naye kwenye ndoa kanuni ni hiyo hiyo kuzama kilindini.

Kumbuka ikiwa unatafuta mtu sahihi kutoka kwa Mungu, mwenye sifa unazotaka..fahamu pia upande wa pili kuna mwingine anatafuta mtu sahihi kutoka kwa Mungu mwenye sifa hizo hizo unazozitaka. Sasa ni kitu gani kitawakutanisha ni kushuka kilindini..huko ni lazima tu ukutananaye, kwasababu kilindi chapigia kelele kilindi.

Lakini ukitaka mume/mke sahihi kutoka kwa Mungu mwenye sifa unazotaka lakini wewe mwenyewe hauna hizo sifa, hapo utasubiri sana kwasababu ni kama mbwa anamuita kuku kwa sauti yake ya kubweka kamwe kuku hawezi kuelewa.

Sasa hapa utazamaje kilindini?

Fuata hatua hizi tano.

Hatua ya kwanza ni kuokoka.

Namaanisha wokovu wa kweli wa kumpokea Yesu kweli kweli na sio ule wokovu wa kidini (wa kuwa vuguvugu). Hii ndio hatua ya msingi kwasababu unayemtafuta awe mume/mke wako ameokoka yupo kilindini naye anatafuta mtu aliyeokoka kweli kweli. Na Mungu ni wa haki hawezi kumpa vinginevyo.

Hatua ya pili:kuwa mtakatifu.

Kama unataka Mungu akupe binti anayeishi maisha masafi, halafu wewe unaishi maisha machafu ya kidunia, hapo utaomba sana lakini mwisho utampata tu aliye kama wewe, kwasababu huyo binti naye anaomba Mungu ampe kijana aliyeokoka na anayeishi maisha masafi ya utakatifu na Mungu hawezi kumpa vinginevyo. Na halikadhalika we ni binti unaomba Bwana akupe kijana mwenye heshima anayependa utakatifu halafu wewe mwenyewe unamuonekano wa kidunia, unavaa nguo za nusu uchi, masuruali, unajipodoa na kupamba mwili wako kwa vitu bandia hapo huwezi kumpata huyo kijana mwenye sifa ya utakatifu, utaishia kumpata tu wa kidunia kama wewe, kwani kijana aliyeokoka anaomba Mungu ampe binti aliyejitambua na kuacha udunia, hivyo Mungu mwenye haki hawezi kumpa vinginevyo.

Hatua zingine ni kuwa mwombaji na msomaji wa biblia, kuwa na upendo, kuwa na bidii ya kufanya kazi/kumtumikia Mungu n.k

Kupitia hatua hizi utampata mtu wako sahihi. Kumbuka kilindi chapigia kelele kilindi.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *