ZITAFAKARINI NJIA ZENU

Biblia kwa kina No Comments

ZITAFAKARINI NJIA ZENU

Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia.

Kwanza kabla hatujaendelea mbele, ni vizuri kufahamu kuwa si kila tatizo linasababibishwa na ibilisi kama wengi wanavyomsingizia shetani, ni kweli shetani anahusika kwa kiasi kikubwa kusababisha matatizo kwa watu, lakini pia yapo matatizo mengine tunajisabibishia sisi wenyewe.

Kwamfano tusome maandiko yafuatayo tuelewe..

Kumbukumbu la Torati 28:15 “Lakini itakuwa USIPOTAKA KUISIKIZA SAUTI YA BWANA, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata.

[16]Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani.

[17]Litalaaniwa kapu lako na chombo chako cha kukandia.

[18]Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, maongeo ya ng’ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.

[19]Utalaaniwa uingiapo, utalaaniwa na utokapo,

[20]BWANA atakuletea laana na mashaka, na kukemewa, katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya, hata uangamie na kupotea kwa upesi; kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo.

[21]BWANA atakuambatanisha na tauni, hata atakapokwisha kukuondoa katika nchi uingiayo kwa kuimiliki.

[22]BWANA atakupiga kwa kifua kikuu, na kwa homa, na kwa kuwashwa, na kwa hari ya moto, na kwa upanga, na kwa ukaufu, na kwa koga; navyo vitakufukuza hata uangamie.”

Sasa ukianzia kusoma mwanzo, utaona BWANA MUNGU anaanza kutangaza baraka zitakazompata mtu atakayetii na kusikiliza maagizo yake, lakini kuanzia mstari wa 15 na kuendelea utaona ni laana zitazowapata watu wasiotaka kutii.

Sasa hapo hata mtu avuche vipi laana, haziwezi kuondoka.. atazunguka sana, ataombewa sana lakini bado matatizo yatakuwa pale pale..na hapo sio shetani bali ni yeye mwenyewe amejisababishia laana kwa kukataa kutii maagizo ya Mungu (nazungumzia watu waliookoka na ambao hawajaokoka), shetani hapa huwa anatumika tu kama chombo cha kuwaletea watu matatizo waliokataa kumsikiliza Mungu.

Kwahiyo matatizo ya namna hii hayaondolewi kwa kuomba tu au kuombewa, yanaondolewa kwa mtu kutii maagizo ya Mungu(Neno lake).

Mfano mwingine, Neno la Mungu linasema..

Malaki 3:8-11 “Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu.

[9]NINYI MMELAANIWA KWA LAANA; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote.

[10]Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.

[11]Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi.

Leo hii mtu anahangaika kutafuta mchawi katika kazi zake, uchumi wake hauwendi sawa, lakini anasahau kuwa kutolipa sehemu ya Mungu (fungu la kumi/zaka) ni kujisababishia laana. Hapo shetani hajahusika kuharibu kazi yako, mazao yako, wala sio chuma ulete, wala hakuna mchawi…ni wewe ndio umejiloga mwenyewe kwa kumwibia Mungu, hivyo umelaniwa…hapo hauhitaji kuombewa bali unahitaji kuomba rehema na kuanza kumtii Mungu na kumheshimu.

Kipindi wana wa Israeli waliporudi kutoka utumwani Babeli, waliagizwa kumjengea Mungu nyumba baada ya lile hekalu la kwanza kuharibiwa, lakini walipoaanza tu kujenga maadui zao wakawadhoofisha kwa vitisho, na hivyo wakaacha kujenga, wakaenda kujenga nyumba zao na kutulia vizuri…huku nyumba ya Bwana ikiwa katika hali mbaya, ndipo neno la Mungu likawajia kupitia Nabii Hagai kusema..

Hagai 1:3-12 Ndipo neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema,

[4]Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika?

[5]Basi sasa, BWANA wa majeshi asema hivi, ZITAFAKARINI NJIA ZENU.

[6]Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka.

[7]BWANA wa majeshi asema hivi, ZITAFAKARINI NJIA ZENU.

[8]Pandeni milimani, mkalete miti, mkaijenge nyumba; nami nitaifurahia, nami nitatukuzwa, asema BWANA.

[9]Mlitazamia vingi, kumbe vikatokea vichache; tena mlipovileta nyumbani nikavipeperusha. Ni kwa sababu gani? Asema BWANA wa majeshi. Ni kwa sababu ya nyumba yangu inayokaa hali ya kuharibika, wakati ambapo ninyi mnakimbilia kila mtu nyumbani kwake.

[10]Basi, kwa ajili yenu mbingu zimezuiliwa zisitoe umande, nayo nchi imezuiliwa isitoe matunda yake.

[11]Nami nikaita wakati wa joto uje juu ya nchi, na juu ya milima, na juu ya nafaka, na juu ya divai mpya, na juu ya mafuta, na juu ya kila kitu itoacho nchi, na juu ya wanadamu, na juu ya wanyama, na juu ya kazi zote za mikono.

[12]Ndipo Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, pamoja na hayo mabaki yote ya watu, wakaitii sauti ya BWANA, Mungu wao, na maneno ya Hagai nabii, kama BWANA, Mungu wao, alivyomtuma; nao watu wakaogopa mbele za BWANA.

Unaona hapo, mbingu kuzuiliwa (baraka za Mungu), na hayo matatizo yote sababu ni kuacha nyumba ya Bwana katika hali ya kuharibika, wakati nyumba zao zimekaa katika hali nzuri..ni kutomheshimu Mungu na hivyo ni laana.

Kwahiyo ndugu unayesoma ujumbe huu, hebu leo TAFAKARI NJIA ZAKO, wote tutafakari njia zetu, kabla hatujakimbilia kuombewa kwasababu ya afya zetu. Pengine leo upo kitandani ujumbe huu unakufikia kukumbusha utafakari njia zako je upo sawa na Mungu? Je unatii Neno lake?

Isaya 38:1 “Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, BWANA asema hivi, TENGENEZA MAMBO YA NYUMBA YAKO; maana utakufa, wala hutapona.

Unaona, magonjwa na matatizo mengine yanasababishwa na sisi wenyewe, kutokutii Neno la Mungu. Leo hii watu wengi wanaokufa kwa magonjwa ni kwasababu hiyo hiyo kutokutii,

2 Mambo ya Nyakati 21:18-19 Na baada ya hayo yote BWANA akampiga matumbo kwa ugonjwa usioponyeka.

[19]Ikawa baada ya siku, ikiisha miaka miwili, matumbo yake yakatokea kwa sababu ya ugonjwa wake, akafa akiugua vibaya. Wala watu wake hawakumfukizia mafukizo kama ya baba zake.

Lakini sio magonjwa tu, hata matatizo mengine asilimia kubwa tumejisababishia wenyewe kwa kutokutii, leo hii unalia haupati faida kwenye kazi yako, hauongezeki, haushibi, unalima unavuna kidogo, unapata fedha ni kama umeweka kwenye mfuko uliotoboka, ni kwasababu gani? Bwana anasema..

Ni kwa sababu ya nyumba yangu inayokaa hali ya kuharibika, wakati ambapo ninyi mnakimbilia kila mtu nyumbani kwake”.

Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka.

[7]BWANA wa majeshi asema hivi, ZITAFAKARINI NJIA ZENU.

[9]Mlitazamia vingi, kumbe vikatokea vichache; tena mlipovileta nyumbani nikavipeperusha. Ni kwa sababu gani? Asema BWANA wa majeshi. Ni kwa sababu ya nyumba yangu inayokaa hali ya kuharibika, wakati ambapo ninyi mnakimbilia kila mtu nyumbani kwake.” (Hagai 1:6-7)

Leo hii nyumba ya Bwana ni kanisa lake, hebu jiulize je umewahi kufanya jambo kwa ajili ya nyumba ya Bwana? Ukasema leo nikapambe hata kwa maua, au kwa mapazia… pengine hujawahi kufikiria hivyo, lakini kwako umezungushia kila aina ya maua hayo ni mambo madogo lakini yanazuia baraka za Mungu.

Leo hii mtu anaweza akawa radhi kuchangia mchango wa harusi hata milioni moja, lakini kuchangia injili hatoi hata nusu ya laki moja!! TAFAKARINI NJIA ZAKO.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *