
MAANA TU KAZI YAKE
Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze biblia, kitabu chenye muongozo wa maisha yetu na maneno ya uzima wa roho zetu.
Neno la Mungu linasema..
Waefeso 2:8-10 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;
[9]wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.
[10] MAANA TU KAZI YAKE, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.
Kila kitu tunachokiona hapa duniani kimetengenezwa aidha na wanadamu au na Mungu mwenyewe, kwa mfano simu yako imetengenezwa na wanadamu, nyumba, gari, ni kazi ya Mwanadamu, lakini milima, maji, hewa ni kazi ya Mungu (Mungu ndiye aliyeziumba/aliyetengeneza)
Vivyo hivyo na sisi ni kazi ya Mungu!! tuliumbwa/tulitengezwa kwa ajili ya kutimiza kusudi fulani, kama ilivyo kwa simu unayoitumia ni kazi ya mwanadamu ilitengenezwa kwa kusudi la kuwasiliana japokuwa inaweza ikatumika kufanya vitu vingine lakini kusudi kuu ni mawasiliano.
Kwahiyo na sisi pia lipo kusudi la kuumbwa na Mungu ukiacha yale makusudi mengine tunayoyajua sisi, lengo kuu kabisa la sisi kuumbwa ni kutenda matendo mema.. hilo ndio kusudi kuu, hayo mengine ni ya ziada tu kama ilivyo kwa simu unaweza ukasikiliza redio lakini hilo sio kusudi kuu. Na haya matendo mema, Mungu aliyabuni kwanza tokea awali ili tuje tuyatende, kama ilivyo kwa kifaa hichi (simu), au gari kabla haijatengenezwa mwanadamu alifikiria kwanza akabuni wazo la mawasiliano, usafiri n.k ndio akatengeneza kifaa kinachoweza kufanya hiyo kazi. Na vivyo hivyo na sisi kabla hatujaumbwa Mungu aliwaza kwanza matendo mema ni yapi, alipoyabuni ndio akafikiria tena ni kitu gani kinaweza kwenda kuyatenda haya matendo mema, je mnyama anaweza, au, malaika akoona hapana, ni kitu kinachofanana na yeye. Ndio akatuumba sisi kwa mfano wake na sura yake ili tuje tuyatende hayo matendo mema… kwahiyo hatujabahatishwa kuumbwa, na hamna mtu aliyezaliwa kwa hasara.. haijalishi amezaliwa kwa njia gani halali au siyo halali..maadam unamfano na sura ya Mungu, basi hapo unafaa kutenda matendo mema ya Mungu…we ni kazi ya Mungu.
Leo hii watu wanahangaika kutafuta kusudi la kuwekwa hapa duniani lakini hawajui kusudi kuu ni kutenda matendo mema ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuje tuyatende.
Sasa haya matendo mema ni yapi??
Turudi nyuma kidogo, tusome…
Waefeso 1:3-4 Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo;
[4]kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe WATAKATIFU, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo.
Ukitaka kujua kusudi la wewe kuumbwa na Mungu ni hapo mstari wa 4, anasema alituchagua kabla ya kuwekwa misingi wa ulimwengu, ili tuwe WATAKATIFU, hilo tu basi. Hatujaumbwa ili tuje kumsaidia Mungu kazi kama maroboti, tumeumbwa tuje tuishi maisha ya utakatifu na hiyo ndio kazi ya Mungu.
Waefeso 2:10 Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende MATENDO MEMA, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo
Hayo matendo mema yanayozungumziwa hapo ni zaidi ya yale tunayoyajua kwamba ni kusaidia yatima, maskini n.k, matendo mema haswa ni kuishi maisha ya UTAKATIFU. Na utakatifu sio kutokuwa na makosa kabisa bali ni kuongozwa na Roho Mtakatifu katika mambo yote.
Maana yake Roho Mtakatifu akiwa ndani yako atakuongoza katika upendo ule wa kiMungu, atakuongoza kumfanyia Mungu ibada katika Roho na kweli, atakuongoza kuishi kulingana na mapenzi ya Mungu, atakufundisha namna sahihi ya kuvaa na kuweka mwili wako, kwa ufupi Roho Mtakatifu ndio muhuri wa utakatifu na mtu asiye na Roho Mtakatifu hawezi kutenda matendo mema haijalishi atajitahidi kwa nguvu zake zote.
Ndio maana anasema tuliumbwa katika KRISTO YESU ili tuyatende matendo mema ambayo Mungu aliyatengeneza tangu awali.
Hivyo leo fahamu kabisa hili kwamba hatuwezi kumpendeza Mungu kama hatujapokea Roho wake Mtakatifu haijalishi tutamfanyia nini!! Yeye anatupenda lakini sisi hatuwezi kumpenda iwapo hatuna Roho Mtakatifu ndani yetu.
Hivyo Roho Mtakatifu ni bure na ni ahadi kwa kila mmoja atakayenyekea na kutubu kwa kumaanisha kabisa kugeuka, na ishara kuu kabisa ya kuwa umepokea Roho Mtakatifu ni maisha yako kuanza kubadilika…unaanza kuchukia dhambi, udunia, kiu ya dhambi inakufa, ile hasira, chuki, kutokusamehe inaanza kuisha ndani yako mpaka wewe mwenyewe unajishangaa, unakuwa unatamani tu kufanya mapenzi ya Mungu, unaanza kuwa mwombaji, unaanza kupenda kusoma maneno ya Mungu na kufuatilia mafundisho ukiona hivyo ujue ni Roho Mtakatifu anakuongoza kutenda matendo mema ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuje tuyatende. Hivyo we ni kazi ya Mungu na wewe na Mungu ni kitu kimoja.
“Mimi na Baba tu umoja” (Yohana10:30) andiko hili halimhusu tu YESU KRISTO mwenyewe lakini pia linawahusu watoto wote wa Mungu. Sisi ni kazi ya Mungu, na sehemu nyingine anasema tu watenda kazi pamoja na MUNGU. Hallelujah.
Je! wewe ni kazi ya Mungu??
Kama bado hujazaliwa mara ya pili, basi fahamu wewe ni kazi ya mwingine, au ni chombo kilichoharibika, hivyo unapaswa leo uzaliwe mara ya pili ili ufanyike chombo bora kwa ajili ya kazi ya Mungu. Na unakuwa mara ya baada ya kutubu dhambi kwa kumaanisha kabisa kuacha na kwenda kubatizwa kwa maji mengi na kwa jina la Yesu…hapo utakuwa umekamilisha hatua ya kuzaliwa mara pili na kuanzia wakati huo Roho Mtakatifu ataingia ndani yako na kukusadia kuyatenda matendo mema yaliyokusudiwa na Mungu toka mwanzo tuyatende.
Mungu akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.