JE! NIMFICHE IBRAHIMU JAMBO NILIFANYALO,

Biblia kwa kina No Comments

JE! NIMFICHE IBRAHIMU JAMBO NILIFANYALO,

Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze biblia Neno la Mungu..chakula cha roho zetu.

Ibrahimu ambaye tunamuita baba wa imani, kutokana na imani yake ya kumwamini Mungu kwa asilimia yote, ikamfanya apendwe sana na Mungu na akawa rafiki mkubwa wa Mungu.

Siku moja Ibrahimu akiwa amepumzika zake mlangoni mwa hema yake wakati wa jua, aliona watu watatu wamesimama mbele yake, kwakuwa alikuwa na mahusiano ya karibu na Mungu alijua kabisa hawa watu sio wakawaida, lazima atakuwa ni Mungu mwenyewe alimtembelea, Hivyo akaenda kuwalaki na kuwakaribisha nyumbani, ili wapate walau maji…wanywe waendelee na safari yao. Tunasoma…

Mwanzo 18:1-19 “BWANA akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari.

[2]Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi,

[3]akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako.

[4]Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu.

[5]Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema.

[6]Basi Ibrahimu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate.

[7]Ibrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng’ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa.

[8]Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala”.

Sasa baada ya watu hao kula na kunywa, wakaendelea na safari yao na Ibrahimu akawasindikiza, wakafika mahali pa kutengana, mmoja akabaki akiongea na Ibrahimu wakati wengine wawili wakaendelea mbele, kumbe huyu aliyebaki ni ELOHIMU mwenyewe, na wale watu aliokuwanao ni malaika wake ambao walikuwa wanaenda kuangamiza ule mji wa Sodoma na Gomora kwasababu ya maovu kuwa mengi katika huo mji. Sasa jambo hili Ibrahimu hakulijua, na kule Sodoma alikuwepo Lutu ndugu yake, lakini Bwana hakuona vema kumficha Ibrahimu adhima ya moyo wake, BWANA akasema..

Mwanzo 18: 16 “Kisha watu hao wakaondoka huko wakaelekeza nyuso zao Sodoma. Ibrahimu akaenda pamoja nao awasindikize.

[17]BWANA akanena, JE! NIMFICHE IBRAHIMU JAMBO NILIFANYALO,

[18]akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa?

[19]Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya BWANA, wafanye haki na hukumu, ili kwamba BWANA naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake.

Ukiendelea kusoma, utaona BWANA alimwambia Ibrahimu mambo yanayoenda kutendeka Sodoma, lakini nataka tuangalie neno hili alilolisema Bwana, kwamba JE! NIMFICHE IBRAHIMU JAMBO NILIFANYALO,

Kuna mahali unaweza ukafika katika mahusiano yako na Mungu, ukatembea na Mungu kama kipenzi chake, yaani ukaingia ndani ya moyo wa Mungu haswa, ukishafika mahali hapo, uwe na uhakika kwamba Mungu hawezi kufanya jambo lolote la kukuumiza pasipo kukushirikisha kipenzi chake.

Hapo ndipo kilele cha upendo, unafika mahali unapendwa na Mungu kiasi hicho, mpaka Mungu anasema ”je! nimfiche Hana/Maiko jambo nilifanyalo,

Na wewe unasema je! nikufiche BABA jambo niliwazalo/nilitakalo, mnakuwa pamoja na Mungu…kama vile baba na mwanawe mpendwa.

Haya ni mahusiano ambayo Bwana Yesu alikuwa nao na Baba yake, mpaka Baba akamshudia akisema..

“...Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye.” (Mathayo 17:5).

Hebu tujitathimini na sisi, je! mahusiano yetu na Mungu yapoje? Je! tupo ndani ya moyo wa Mungu na Mungu yupo ndani ya mioyo yetu? Kiasi kwamba wewe na Mungu ni kitu kimoja, mnaamua pamoja, unachokiwaza unamshirikisha Mungu na pia Mungu anakushirikisha mambo anayotaka kuyafanya juu yako,

Bwana Yesu alisema maneno haya..

Yohana 15:7 ”Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.”

Ikiwa na maana, ukikaa ndani ya moyo wake na yeye akakaa ndani yako, mnakuwa kitu kimoja, ndio maana mahali fulani maandiko yanasema aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye, kama vile ilivyo kwa wanandoa ni mwili mmoja. Sasa ukifikia mahali hapo, hautataabika sana na masumbufu ya maisha haya, hautaumizwa sana na adha za dunia hii, kwamaana kinachokuumiza, kitamuumiza pia Mungu, na halikadhalika kitakachokufurahisha kitamfurahisha pia Mungu.

Sasa jiulize, unangalia filamu za kidunia, unasikiliza miziki ya kidunia, unapata furaha kwenye starehe za kidunia, unashabikia mipira na kufurahi mpaka unahisi kupasuka moyo!! hebu jiulize Mungu unayemuita Baba yako anafurahiswa na hayo mambo?

Kwakweli mtu wa namna hii hana ushirika kabisa na Mungu, hajaungwa pamoja naye bali amejiungamanisha na miungu mingine.

Lakini aliyeungwa na Bwana, moyo wake wote upo kwa Mungu, kila analoliwaza anamshirikisha Mungu, kila alifanyalo au atakalo kulifanya anauliza kwa Baba yake, maamuzi yake yote yanategemea kwa Baba yake, hana siri na Mungu… mambo yake yote yapo wazi Kwa Mungu.

Hana hofu na maisha kwasababu anamwamini Baba yake, njia zake zote zinaongozwa na Mungu, maneno ya Mungu yanaishi ndani ya moyo wake, mtu wa namna hii..kwanini Mungu asiseme “huyu ni mwanangu ninayependezwa naye” kumbuka unaweza ukawa mwana wa Mungu na usiwe mwanawe uliyependezwa naye.

Ili ufike mahali Mungu akushuhudie kuwa huyu ni mwanangu niliyependezwa naye..ni lazima umchukukulie Mungu kama Baba yako na umwamini kwa mambo yote na umtegemee kwa kila kitu na maneno yake yawe ndani yako. Hapo ukiomba lolote uwe na uhakika kupokea.

Na ukifikia mahali hapo, Mungu anasema je! nimfiche mwanangu Sara jambo nilifanyalo, je nimfiche mwanangu John jambo nilifanyalo, kama alivyosema je! nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo.

Leo anza kutengeneza mahusiano yako na Mungu, na Mungu atakupenda kweli kweli, ichukie dhambi, chukia udunia, ishi kwa imani na kwa upendo, mfanye Mungu rafiki yako na Baba yako pia.

1 Yohana 3:1 Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.

Je! umeokoka ipasavyo? Kama bado hujaokoka kweli kweli unasubiri nini mpaka sasa? Hujui muda uliobakia ni mfupi sana, ni heri leo leo ufanye maamuzi sahihi ya kuokoka kabla mlango haujafungwa..kwa maana muda wowote utafungwa.

Mungu akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *