
JE! UMEKUWA KIUMBE KIPYA
Maandiko yanasema..
2 Wakorintho 5:17 “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya”.
Ishara kuu kabisa inayomtambulisha mtu kuwa ameokoka kweli kweli ni maisha yake baada ya kuokoka kubadilika, na si kubadilishwa jina na kupewa la Kikristo, au kupewa cheti fulani.
Mtu anapoamua kumpa Yesu maisha yake, akamaanisha kabisa kutubu dhambi zake na kuacha udunia…anapewa uwezo wa Mungu ndani yake. (uwezo wa kufanyika mtoto wa Mungu), hivyo anakuwa amezaliwa upya katika roho, anakuwa kiumbe kipya.
Yohana 1:12-13 Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;
[13]waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.
Kwahiyo mtu huyu aliyezaliwa upya, anaanza kuonyesha tabia za kiungu…kwa kuwa amezaliwa kwa Mungu, anaanza kuchukia ulimwengu na anakuwa adui wa dhambi kwasababu amezaliwa katika ulimwengu wa Mungu usio na dhambi, hivyo mambo ya ulimwengu huu kwake yeye anaona hayana maana, anaanza kutamani kujua zaidi mambo ya kiMungu, anaanza kutafuta huku na huku na kufuatilia mafundisho, kiu ya kusoma biblia inaongezeka, kiu ya kumtafuta Mungu zaidi ya mambo mengine inaongezeka.. kidogo kidogo anakua na hatimaye anakuwa mtu mzima aliyekomaa kiroho. Huyu ndiye mtu aliyeokoka/aliyefanyika kiumbe kipya.
Lakini ukimuona mtu anasema ameokoka na ana mwaka au miaka katika wokovu, lakini hana mabadiliko yoyote, maisha yake ni yale yale, bado tu anavaa kidunia, anaenenda kidunia, bado anatazama pornography, anasikikiza miziki ya kidunia, anajipodoa, anajichua, bado anaishi katika dhambi, huyo mtu hajaokoka bado, hajazaliwa mara ya pili kwa Mungu, bado ni mwana wa ulimwengu huu…hata kama anaimba kwaya kanisani, au ananena kwa lugha gani, au anafanya nini huyo bado anahitaji msaada wa Mungu apate kuokoka.
Tujiulize mimi na wewe, je! tumefanyika viumbe vipya, je! maisha yetu yanaaksi wokovu wa kweli au bado maisha yetu ni yale yale ya kale na huku tunadai tumeokoka.
Bwana Yesu atusaidie.
Unyakuo umekaribia sana!! (Ile siku inazidi kukaribia, huwenda ikawa hata ni leo.. Bwana Yesu anarudi)
Shalom.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.