MAZUNGUMZO MABAYA HUHARIBU TABIA NJEMA.

Biblia kwa kina No Comments

MAZUNGUMZO MABAYA HUHARIBU TABIA NJEMA.

Jihadhari na mazungumzo mabaya,

1 Wakorintho 15:33 “Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema.

Ukitaka kuharibu tabia yako (tabia ya kiungu), njia rahisi ni kujiingiza katikati ya mazungumzo mabaya, ukishakuwa kwenye mazungumzo hayo uwe na uhakika kuwa tabia yako itaporomoka tu, inaweza isiwe muda huo huo lakini ni swala la muda tu lazima ubadilike hata kama hutaki.

Kwa mfano nikuonyeshe baadhi ya watu waliojiingiza kwenye mazungumzo mabaya mwisho wao wakajikuta pabaya,

Mwanzo 34:1-2 Basi Dina, binti Lea, ambaye Lea alimzalia Yakobo, AKATOKA KUWAONA BINTI ZA NCHI.

[2]Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, mkuu wa nchi, akamwona akamtwaa, akalala naye, akambikiri.

Sasa huyu Dina yeye pengine alienda tu kuwaoana mabinti wengine huko nje (mabinti wa kidunia), alikuwa ni binti mwenye tabia njema tu, hakuwahi kukutana na wanaume, alikuwa amejitunza kwa wakati wote, lakini alipotoka tu na kujiingiza katikati ya mabinti wa kidunia wasio na mwelekeo wa kiMungu, ambao muda wote wanazungumzia wanaume, Dina naye akaanza kusikiliza yale mazungumzo, pengine wakawa wanamwambia yaani binti mzuri namna hii hauna hata boyfriend, Vaa basi hata mavazi ya kujiachia kidogo vijana wakuone, onyesha hata maungo yako kidogo, achana na hayo mavazi ya kizee, jipake basi hata poda kidogo, wakamwambia maneno mengi ya kizinzi, pengine Dina alikataa mwanzoni, lakini mwisho wa siku akajikuta amebadilishwa na yale mazungumzo.. shetani akamletea yule kijana akamharibu. Tabia yake njema ikawa imeharibiwa namna hiyo.

Mwangaliye tena kijana mwingine anayeitwa Amnoni alisikiliza ushauri wa rafiki yake Yonadamu (2Samweli 13), akafanya maamuzi mabaya sana ya kumbaka dada yake.. lakini chanzo ni mazungumzo mabaya kutoka kwa rafiki yake.

Hiyo ni mifano michache tu lakini ipo mifano mingi ya namna hiyo kwenye biblia, na sisi wenyewe ni mashuhuda jinsi watu leo wanavyoharibiwa tabia zao njema kupitia mazungumzo mabaya.

Siku zote fahamu hili mazungumzo mabaya huharibu tabia njema, jitenge na mazungumzo mabaya. Usiseme ninasikiliza tu lakini siwezi badilika, ni kweli unaweza usibadilike wakati huo huo, lakini nakuambia ni swala la muda tu, ukiendelea kusikiliza kama ni umbeya utajikuta tu na wewe hiyo tabia imehamia kwako, kama ni uongo, matusi, na tabia zingine mbaya kadri unavyosikiliza automatiki hizo tabia itahamia tu kwako hata kama ulikuwa hutaki, yaani kitendo tu cha kusikiliza ndio kidogo kidogo umeruhusu kubadilishwa tabia. Ndio maana kama unasikiliza pia na kufuatilia sana mafundisho ya kiroho, au unazungumza mara kwa mara na mtu mwenye tabia njema na wewe utajikuta umeiga tabia zake…mpaka usemi wake.

Unachokisikiliza ndiyo inaamua tabia yako iwe njema au mbaya, ukisikiliza mazungumzo ya kichawi kichawi na mashetani moja kwa moja tabia za kichawi/kishetani itaanza kuingia ndani yako, ukisikiliza mazungumzo ya kihuni tabia za kihuni utakuwanayo tu, ukisikiliza mazungumzo ya kiuasherati..uwe na uhakika uasherati huwezi kuikwepa, halikadhalika ukisikiliza mazungumzo ya kiMungu utakuwa na tabia za kiungu.

Chagua leo aina ya mazungumzo utakayosikiliza, kwani maamuzi ni yako. Kama unataka kuwa salama na kudumu katika utakatifu jihadhari na mazungumzo mabaya, jitenge na marafiki wa kidunia, ukiona mazungumzo ambayo masaa yote karibu siku nzima mnazungumza tu lakini hakuna hata neno moja la kiMungu jihadhari na hayo mazungumzo ni mazungumzo mabaya, jihadhari na mazungumzo yenye maudhui ya uzinzi hata kama ni mchumba wako hampaswi kuzungumzia hayo mambo mpaka mfunge ndoa halali.

Jiepue…kaa mbali na mazungumzo mabaya, kata mawasiliano na watu wanaozungumzia mambo maovu, tafuta mazungumzo mema (yenye Mungu ndani yake).

Bwana Yesu akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *