NINA KUFA KILA SIKU 

Biblia kwa kina No Comments

NINA KUFA KILA SIKU 

Mtume Paulo alikuwa na maana gani kusema katika 1Wakorintho 15:31″…NINAKUFA KILA SIKU?

1 Wakorintho 15:31 “Naam, ndugu, kwa huku kujisifu kwangu niliko nako juu yenu katika Kristo Yesu Bwana wetu, NINAKUFA KILA SIKU”.

Safari ya wokovu ni safari ya kujikana nafsi kila siku na sio siku ile tu ulipookoka, ni kila siku tunajikana na kuchukua misalaba yetu, ni kila siku tunakufa kwa habari ya ulimwengu, unakufa kila siku kwa habari ya fashion za ulimwengu huu, unakufa kila siku kwa kampani za marafiki wabovu, unakufa kila siku kwa habari ya matusi, kila siku unakufa kwa habari ya uasherati na tamaa zake kwa kujiweka mbali nazo, unakufa kwa habari ya rushwa, unakufa kwa habari ya usengenyaji, na anasa n.k.

Fashion mpya ikiingia unakuwa hujui kinachoendelea, filamu mpya ikitoka huna habari nayo, ukiulizwa ni timu gani inayoongoza kwa sasa unakuwa kama mtoto aliyezaliwa leo hajui chochote, wakiongelea habari za wanamiziki wa dunia hii ndio kabisa wamekupoteza hujui hata mziki unaotrend mtandaoni, yaani unakuwa mjinga mjinga katika vitu vya kidunia… isipokuwa yale yanayokupa faida na kujenga roho yako.

Ukiweza kuwa mkristo wa namna hii, hapo ulimwengu unakuwa umesulibiwa kwako na wewe kwa ulimwengu.

Wagalatia 6:14 Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ULIMWENGU UMESULIBISHWA KWANGU, NA MIMI KWA ULIMWENGU.

Lakini ukijiona wewe na huu ulimwengu ni marafiki, kila taarifa mpya isiyo na maana ni yako, commed za vichekesho havikupiti, channel zako unazofuatilia ni zile za mpira, miziki ya kidunia, na hata ukifungua za mahubiri unasikiliza yale mahubiri yanayokuhubiria tu mambo ya dunia hii, we ni mtu unayelazwa na movies, unakesha kuperuzi peruzi kutazama vitu visivyo na maana, unawajua wasanii wote, unajua rekodi zote za wachezaji, lakini hata hujui biblia ina vitabu vingapi!!

Hapo fahamu kuwa bado unaupenda ulimwengu na hujaokoka, hivyo unapaswa kujikana nafsi yako leo na kuokoka kweli kweli… baada ya hapo unaendelea na safari ya wokovu kwa kuchukua msalaba wako kila siku na kufa kwa mambo ya kidunia yasiyomtukuza Mungu… lakini ukiona ni sheria ngumu basi usijaribu kuwa mkristo jina, ni heri ubaki kuwa mpagani kweli kweli, usiwe hapo katikati ni hatari sana, amua kuwa moto au baridi, usiwe vuguvugu kabisa.

Luka 9:23-24 “Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake KILA SIKU, ANIFUATE.

[24]Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha.

Maran atha (Bwana anarudi)

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *