Mhubiri 10:15 “Kazi yao wapumbavu huwachosha kila mmoja, Maana hajui hata njia ya kuuendea mji.”
Kama tunavyojua ni wazi kuwa Kila mtu anatamani kuishi mjini kuliko mashambani; Hii ni kwa sababu mjini kuna huduma zote kwa urahisi zaidi, pia ni mahali pa raha kiasi kwamba watu hufanya kazi zao mashambani ili wakaziuze mijini, kadhalika nakufaidi matunda yao huko.
Lakini jaribu kufikiri juu ya mtu aliyejitaabisha kufanya kazi zake ili akazifurahie mjini, lakini hajui njia ya kufika huko. Badala yake anakosea njia na kwenda mabondeni au Jangwani, ni dhahiri mtu huyu hatopata raha ya kazi yake; kwasababu alikosa malengo na maarifa sahihi hivyo kukosa faida ya taabu yake!
Sasa tunapata ufunuo gani nyuma ya hilo?
Sisi tuliomwamini Yesu tunao mji tunaoutarajia kuingia nao ni YERUSALEMU MPYA ushukao kutoka Mbinguni
Tusome..
Ufunuo wa Yohana 21:2-3
2 “Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe.
3 Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.”
Anaendelea zaidi…
Ufunuo wa Yohana 22:14-15
14 “Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake.
15 Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya.”
Huu ndio mji ule ambao hata Ibrahim aliutazamia, na kumfanya aishi maisha kama mpitaji tu wa Dunia hii..
Waebrania 11:8-10
8 “Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako.
9 Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.
10 Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.”
Sasa kumbe na sisi ili tuonekane kustahili kuingia mji huo wa Mbinguni hatuna budi kuwa tumeokolewa na Yesu Kristo, maana ni yeye pekee njia ya kuuingia mji huo.
Ukiwa nje ya Yesu hakika wewe ni mpumbavu, Maana taabu yako yote ya hapa duniani haitokufaidisha kwa lolote!
Wala haikupeleki mji wa Mungu zaidi ya kukuchosha tu.
Huenda ukawa na maghorofa, miradi mikubwa, makampuni, nyumba, magari n.k lakini mwishowe ukafa na kuishia kaburini.
Lakini Leo nakutangazia habari njema ya kuwa ikiwa ukiiona njia ya kuiendea Yerusalemu basi kazi yako SI Bure, maana kwa kujiwekea hazina yako kule unafanya kazi ya kuchosha, na hakika utafaidi matunda yake nayo ni Uzima baada ya Kifo.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.