SHETANI NI KAMA SIMBA ANGURUMAYE

Biblia kwa kina No Comments

SHETANI NI KAMA SIMBA ANGURUMAYE

Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze biblia Neno la Mungu lililo taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu (Zaburi 119:105).

Simba anapokwenda kuwinda katika kundi la wanyama, mara nyingi hutazama na kutambua yule anayeonekana dhaifu, aliyechoka, aliyejeruhiwa au aliyeanza kutengana na kundi lake. Halikimbilii tu bila malengo kundi la nyati analoliona mbele yake na kwenda kumrukia yoyote tu ampendaye hapana, vinginevyo hataambulia chochote lakini kinyume chake utamwona anatulia katika eneo zuri la utulivu na la maficho ambalo litamsaidia kuchora mpango wake kichwani na pia litakalompa wigo wa kuchomoka kwa kasi na haraka kumrukia mnyama kabla hata hajaanza kuongeza kasi ya kukimbia.

Simba anaweza kuingia katikati ya kundi, kulishtua kundi lote, na katika vurugu hiyo akapata nafasi ya kumfuatilia yule dhaifu na kumtenga na wenzake. Akifanikiwa kumtenga, inakuwa rahisi zaidi kumshambulia na kumfanya kitoweo chake.

Na ndivyo ilivyo kwa shetani, biblia inamtaja kama simba aungurumaye, anayezunguka-zunguka akitafuta mtu wa kummeza.

1 Petro 5:8“Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu, Ibilisi, kama simba aungurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.”

Shetani hutumia udhaifu wa mkristo kumshambulia.

Moja ya mbinu zake za hatari ni kumshambulia Mkristo katika hali yake ya udhaifu, kisha kumfanya ajitenge na ushirika wa waamini, mpaka anapoteza nguvu ya kujengwa, kuonywa, kuombewa na kutiwa moyo.

Shetani haanzi moja kwa moja kwa kumfanya mtu aache wokovu, anaanzia mbali kupunguza moto wake, anaanza kupunguza kiu yake ya Mungu, anamfanya apoteze hamu ya ibada, maombi, Neno na ushirika. Mambo hayo yanapopungua, mtu anaweza kujikuta akirudi nyuma taratibu.

Simba anapotazama kundi, mnyama dhaifu anaweza kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kushambuliwa. Ndivyo ilivyo katika vita vya kiroho; udhaifu wa kiroho usipotibiwa unaweza kuwa nafasi ya mashambulizi ya shetani, Mkristo anapoanza kulegeza maombi, kupunguza kusoma Neno, kupuuza ibada na kupoteza kiu ya Mungu, anaweza kuwa katika hali ya udhaifu wa kiroho. Shetani hutafuta nafasi katika hali hiyo ili kuendeleza kumdhoofisha zaidi.

Wakati mwingine mtu hajui kwamba amedhoofika, kwa sababu bado anajiona kuwa ni Mkristo. Lakini ndani yake, kiu ya Mungu imepungua, moyo wa kutafuta uwepo wa Mungu umelegea na mambo ya dunia yanaanza kuvutia zaidi kuliko mambo ya Roho.

Hapo ndipo shetani anaanza kutumia udhaifu ambao Mkristo ameupuuza ili kuendeleza mashambulizi yake, ndiyo maana Biblia inatuonya tukeshe. Usisubiri mpaka udhaifu wako uwe mkubwa ndipo uanze kutafuta msaada wa Mungu. Kiu ya maombi inapopungua, anza kuomba zaidi; hamu ya Neno inapopungua, rudi kulisoma; moyo unapolegea, mtafute Mungu kwa bidii.

𝟮. 𝗦𝗛𝗘𝗧𝗔𝗡𝗜 𝗛𝗨𝗧𝗨𝗠𝗜𝗔 𝗞𝗨𝗧𝗘𝗡𝗚𝗔𝗡𝗔 𝗡𝗔 𝗨𝗦𝗛𝗜𝗥𝗜𝗞𝗔 𝗞𝗔𝗠𝗔 𝗠𝗧𝗘𝗚𝗢 𝗪𝗔 𝗞𝗨𝗞𝗨𝗧𝗘𝗡𝗚𝗔𝗡𝗜𝗦𝗛𝗔 𝗡𝗔 𝗨𝗟𝗜𝗡𝗭𝗜 𝗪𝗔 𝗞𝗜𝗥𝗢𝗛𝗢.

Simba anapofanikiwa kumtenga mnyama na kundi lake, anakuwa amepunguza uwezekano wa mnyama huyo kupata msaada kutoka kwa wenzake. Ndivyo shetani anavyoweza kutumia kujitenga kwa Mkristo na ushirika kama mtego. Shetani anaweza kuanza kukujengea mawazo kwamba huna haja ya kwenda ibadani, huna haja ya kukaa na Wakristo wenzako, huna haja ya kushiriki maombi ya pamoja, na unaweza kuendelea kumtumikia Mungu ukiwa peke yako.

Lakini ushirika wa waamini si jambo la kupuuza. Mungu anaweza kutumia waamini wengine kukutia moyo, kukushauri, kukuonya, kukuombea na kukusaidia kusimama katika imani.

Waebrania 10:25“Wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.”

Ushirika ni sehemu ya kujengana katika Kristo. Unapojitenga bila sababu ya msingi na kuacha kujengwa na wengine, unaweza kujikuta ukipambana na vita ambavyo ungeweza kupata msaada wa kuvishinda.

Shetani anapokufanya uone ushirika hauna umuhimu, anaweza kuwa anakutengenezea mazingira ya kukaa peke yako katika udhaifu wako, usikubali kukosa kiu ya ushirika kuwa jambo la kawaida. Mkristo anahitaji ibada, mafundisho, maombi na ushirika wa waamini, ingawa ushirika huo lazima uwe wa afya, unaomjenga katika kweli ya Kristo.

𝟯. 𝗦𝗛𝗘𝗧𝗔𝗡𝗜 𝗔𝗞𝗜𝗞𝗨𝗗𝗛𝗢𝗙𝗜𝗦𝗛𝗔 𝗡𝗔 𝗞𝗨𝗞𝗨𝗧𝗘𝗡𝗚𝗔𝗡𝗜𝗦𝗛𝗔 NA KUNDI, ANAKURUDISHA 𝗞𝗪𝗘𝗡𝗬𝗘 𝗠𝗔𝗜𝗦𝗛𝗔 𝗬𝗔 𝗭𝗔𝗠𝗔𝗡I.

Shetani anapofanikiwa kumdhoofisha Mkristo na kumfanya ajitenge na mambo yanayomjenga kiroho, shambulio lake linaweza kuendelea kuelekea kumrudisha katika maisha ya zamani.

Mtu aliyeanza kupoteza kiu ya Mungu, aliyeacha ushirika na aliyelegeza maisha ya maombi anaweza kuanza kurudia tabia ambazo Mungu alimtoa. Anaweza kurudia marafiki waliokuwa wakimvuta kwenye dhambi, tamaa za zamani, ulevi, uasherati, chuki, uongo na mwenendo wa dunia.

Hii ndiyo hatari ya kutokuchukulia kwa uzito hali yako ya kiroho. Shetani anataka udhoofike kiasi kwamba yale mambo uliyokuwa unayakataa kwa sababu ya Kristo, uanze kuyakubali tena, akijua mtu akisharudia maisha ya dhambi na udunia hali yake inakuwa mbaya zaidi ya alivyokuwa hapo kabla hajaokoka, ndicho Neno la Mungu linasema katika..

2 Petro 2:20 “Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza”.

Kama Mkisto uliyeokoka kweli kweli, unapaswa kulinda wokovu wako, kwa kuogopa na kuitetemekea kama biblia inavyotufundisha (Wafilipi 2:12), usikubali kurudi nyuma kwa namna yoyote ile, usikubali kupunguza ratiba ya maombi, ratiba ya kufunga, kukesha, kusoma Neno, usikubali kujitenga na wenzako.

Usikubali udhaifu wowote ndani yako, unapoona kuna hali ya kuwa dhaifu katika eneo lolote la kiroho, labda eneo la maombi au kusoma Neno..haraka sana fanya bidii kuhakikisha unaendelea mbele. Shetani ni simba aungurumaye, huzunguka-zunguka akitafuta mtu ammeze. Anaweza kutumia udhaifu wako, anaweza kukushawishi kujitenga na ushirika, na anaweza kutafuta kukurudisha kwenye maisha ya zamani.

Lakini usikubali mtego wake, kesha katika imani, linda kiu yako ya Mungu, dumisha ushirika wa waamini na usiruhusu udhaifu wako uwe sababu ya kuacha kusimama katika Kristo.

Bwana Yesu akubariki.

Maran atha!

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *